Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Tanzania imeweka lengo la kuwa miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza duniani kwa uzalishaji wa chakula, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uchumi, kuongeza ajira na kuhakikisha usalama wa chakula kwa wananchi, kupitia uwekezaji katika sekta ya kilimo. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema azma hiyo imeainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050, inayolenga pia kuifanya nchi kuwa mzalishaji mkuu wa chakula barani Afrika. Akizungumza Oktoba 22, 2026, jijini Des Moines, Iowa, Marekani, wakati akiwasilisha mada kuu kuhusu mustakabali wa kilimo barani Afrika katika Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue), Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea kukipa kilimo kipaumbele kutokana na mchango wake katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa. Amesema chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi shilingi trilioni 1.241 mwaka 2025/2026, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kukifanya kilimo kuwa injini ya mageuzi ya kiuchumi, uzalishaji wa ajira, ukuaji wa viwanda na upanuzi wa masoko ya nje. Matokeo ya uwekezaji huo yanaonekana katika kiwango cha utoshelevu wa chakula nchini, ambacho kimefikia asilimia 130, hali inayoiwezesha Tanzania kukidhi mahitaji yake na kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya kikanda na kimataifa. Aidha, mauzo ya nje ya mazao ya kilimo yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 2.1 mwaka 2021/2022 hadi dola bilioni 3.7 mwaka 2024/2025, hatua inayoonesha nafasi inayozidi kuimarika ya kilimo katika kukuza biashara na mapato ya taifa. Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba anaeleza kuwa kilimo ni moja ya nguzo kuu za uchumi wa Tanzania, kikichangia asilimia 24.6 ya Pato la Taifa, kuajiri asilimia 65 ya nguvu kazi na kuzalisha takriban asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje, huku kikiendelea kutoa malighafi muhimu kwa viwanda vya ndani. Pamoja na mafanikio hayo, anasema Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza kilimo kinachozingatia usalama na ubora wa chakula. Katika mkutano huo, Dkt. Mwigulu amempongeza Prof. Huub Lelieveld, mshindi wa Tuzo ya Chakula Duniani ya mwaka 2026, kwa mchango wake katika masuala ya usalama wa chakula. Amesisitiza kuwa usalama wa chakula haupimwi kwa upatikanaji pekee, bali chakula kinapaswa kuwa salama kwa matumizi, kuwa na virutubisho vinavyohitajika na kupatikana kwa bei nafuu ili wananchi waweze kumudu mahitaji yao ya lishe. Akizungumzia kaulimbiu ya mjadala huo, “Kabla Njaa Haijatushinda,” Waziri Mkuu amesema Afrika ina uwezo mkubwa wa kuwa mchangiaji muhimu wa usalama wa chakula duniani, badala ya kuendelea kuonekana kama bara linalokabiliwa na changamoto za upatikanaji wa chakula. Amesema kufikia azma hiyo kunahitaji uwekezaji zaidi kwa wakulima, vijana na wanawake, pamoja na kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na mifumo imara ya uzalishaji na usambazaji wa chakula. Waziri Mkuu amehimiza mataifa ya Afrika kuchukua hatua za pamoja, kuendeleza ubunifu na kujenga mifumo endelevu ya chakula inayoweza kukidhi mahitaji ya vizazi vya sasa na vijavyo. Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mhariri Mkuu wa Jarida la Afrika la Chakula, Kilimo, Lishe na Maendeleo, Prof. Ruth Oniang’o, amesema anaamini Tanzania inaweza kuwa mfano kwa mataifa mengine kutokana na hatua inazopiga katika sekta ya kilimo. Prof. Oniang’o amesifu jitihada za Serikali, hususan uwekezaji katika miundombinu, utekelezaji wa programu ya Jenga Kesho Bora (BBT) na matumizi ya maafisa ugani kuwasaidia wakulima kuboresha uzalishaji. Kwa ujumla, lengo la Tanzania kuingia katika orodha ya nchi 10 bora duniani kwa uzalishaji wa chakula linaweka msisitizo katika kuendeleza uwekezaji, kuongeza tija na kutumia fursa za masoko ya kimataifa. Utekelezaji wake utahitaji kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao, kupanua fursa kwa wakulima na kuhakikisha chakula kinachozalishwa kinakidhi viwango vya ubora na usalama. Dkt. Mwigulu amehudhuria mkutano huo akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe; Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde; Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie Kanza, pamoja na watendaji wengine wa Serikali.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Sekta ya Kilimo kwa miaka mingi imeendelea kuwa mhimili wa uchumi wa Tanzania na inayotoa uhakika wa usalama wa chakula, kutoa ajira kwa mamilioni ya wananchi na kuchechemua biashara, viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji. Hivyo, kumuwezesha mkulima kuongeza tija katika kilimo na kuimarisha kipato si jukumu la sekta moja pekee, bali ni uwekezaji wa moja kwa moja katika uchumi na mustakabali wa Taifa. Katika miaka ya hivi karibuni, uwekezaji katika sekta ya kilimo umeongezeka. Mathalani Bajeti ya Wizara ya Kilimo imepanda kutoka Shilingi bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi Shilingi trilioni 1.19 mwaka 2025/2026. Ongezeko hilo linaonesha uzito wa sekta ya kilimo katika ajenda ya maendeleo na juhudi za kujenga mazingira yatakayomwezesha mkulima kuongeza uzalishaji. Miongoni mwa hatua zinazomgusa mkulima moja kwa moja ni mfumo wa ruzuku za pembejeo, hususan mbolea na mbegu bora. Lengo ni kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija shambani. Taarifa zinaonyesha kuwa matumizi ya mbolea yaliongezeka kutoka tani 360,000 kabla ya mfumo wa ruzuku hadi tani 840,000 katika msimu uliofuata, huku lengo likiwa kufikisha matumizi hadi tani milioni moja. Lakini kuongeza uzalishaji kunahitaji pia uhakika wa maji. Kutegemea mvua pekee kunaendelea kuwa changamoto katika uzalishaji wa kilimo, hivyo uwekezaji katika umwagiliaji ni hatua muhimu ya kumuwezesha mkulima kuzalisha kwa uhakika zaidi. Kufikia mwaka 2024/2025, Serikali ilikuwa ikitekeleza miradi 780 ya umwagiliaji yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 543,000, huku kukamilika kwa miradi hiyo kukitarajiwa kuongeza eneo la umwagiliaji hadi zaidi ya hekta milioni 1.27. Pamoja na miundombinu hiyo, ushiriki wa wakulima katika usimamizi wa umwagiliaji nao umeongezeka. Idadi ya Vyama vya Umwagiliaji vilivyosajiliwa imepanda kutoka 19 mwaka 2020/2021 hadi 912 mwaka 2024/2025. Hii inaashiria nafasi inayoongezeka ya wakulima katika kusimamia rasilimali muhimu kwa uzalishaji wao. Kilimo pia kinafungua ukurasa mpya kwa vijana. Kupitia programu kama Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), vijana wanahamasishwa kukiona kilimo kama biashara na fursa ya uwekezaji. Mtazamo huu ni muhimu kwa kizazi kinachoweza kutumia teknolojia, ubunifu na maarifa ya kisasa kubadilisha kilimo kutoka shughuli ya kutegemea nguvu kazi pekee na kuwa biashara yenye tija. Hata hivyo, kumuwezesha mkulima hakumaanishi kumuwezesha kuzalisha pekee. Mkulima anahitaji kuwezeshwa kuzalisha, kuhifadhi, kusindika na kuuza kwa thamani inayostahili. Bila soko la uhakika na uwezo wa kuongeza thamani, ongezeko la uzalishaji linaweza lisitafsiriwe moja kwa moja kuwa ongezeko la kipato. Hapa ndipo nafasi ya viwanda inakuwa muhimu. Mazao yanayotoka mashambani yanapaswa kuwa malighafi ya viwanda vya ndani. Alizeti inaweza kuzalisha mafuta, nafaka zikachakatwa kuwa bidhaa mbalimbali, maziwa yakaongezwa thamani na mazao mengine yakahifadhiwa na kusindikwa. Kwa kufanya hivyo, thamani inayotokana na kilimo hubaki zaidi ndani ya nchi, huku ikifungua nafasi za ajira na biashara. Kwa mtazamo huo, Agenda 10/30 inaleta umuhimu wa kuongeza tija, thamani ya mazao, mauzo ya nje, ushiriki wa vijana na upatikanaji wa malighafi kwa viwanda. Kilimo kinapounganishwa na viwanda na masoko, mkulima haonekani tena kama mzalishaji wa malighafi pekee, bali anakuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani unaozalisha utajiri. Hata hivyo, kipimo cha mwisho cha mafanikio ya uwezeshaji kinapaswa kuwa maisha ya mkulima. Bajeti inaweza kuongezeka na miradi inaweza kujengwa, lakini mafanikio halisi yataonekana pale mkulima atakapoweza kuzalisha kwa gharama nafuu, kupata mavuno bora, kuhifadhi mazao, kupata soko na kulipwa kwa thamani inayolingana na jasho lake. Tanzania ina ardhi, maji, nguvu kazi, masoko na malighafi nyingi zinazoweza kuifanya kilimo kuwa injini kubwa zaidi ya uchumi. Kinachohitajika ni kuendelea kujenga mazingira yatakayomwezesha mkulima kutumia fursa hizo kikamilifu na kuwahamasisha vijana, wafanyabiashara na wawekezaji kuingia katika kilimo kwa mtazamo wa biashara. Tanzania yenye mkulima mwenye uwezo wa kiuchumi ni Tanzania yenye msingi imara wa chakula, viwanda, ajira na uchumi shirikishi. Kumuwezesha mkulima si kumsaidia mkulima pekee ni kuijenga Tanzania yenye uwezo wa pato la Taifa lenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja na wastani wa pato la mtu mmoja lenye thamani ya dola za Marekani 7000 kwa mwaka.