Sekta ya Madini Yaendelea Kuitambulisha Tanzania Kimataifa
Sekta ya Madini inapozidi kuwa muhimu katika uchumi wa dunia, ushindani wa kimataifa haupimwi tena kwa wingi wa rasilimali pekee, bali pia kwa namna zinavyosimamiwa, uwekezaji unaovutwa na manufaa yake kwa wananchi. Mabadiliko haya yanaifanya Sekta ya Madini ya Tanzania kuzidi kujijengea nafasi katika mjadala wa kimataifa, kupitia maboresho ya sekta, ukuaji wa uwekezaji na ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Kwa mujibu wa Tathmini ya Taasisi ya Fraser ya Canada ya mwaka 2025, Tanzania imeendelea kuimarika katika Sekta ya Madini kwa kushika nafasi ya nne barani Afrika na ya 34 duniani katika Kiashiria cha Kuvutia Uwekezaji (Investment Attractiveness Index). Aidha, Tanzania imeorodheshwa nafasi ya 15 duniani katika kipengele cha upatikanaji wa rasilimali madini, ikiwa na alama 75, jambo linalothibitisha utajiri mkubwa wa rasilimali za madini zilizopo nchini.
Hata hivyo, nafasi hizi hazielezi tu uwepo wa madini mengi nchini. Zinadhihirisha pia kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji, usimamizi wa sekta, uwazi wa sera na ongezeko la imani ya wawekezaji kwa Tanzania. Kwa maneno mengine, Tanzania haitajwi katika tathmini hizi kwa sababu ya utajiri wa madini pekee, bali kwa jinsi inavyoendelea kujenga mazingira yanayowezesha rasilimali hizo kuchangia maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi.
Mwelekeo huo unaonekana pia katika upande wa uwekezaji. Kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 2025, Sekta ya Madini imeendelea kuongoza kwa kuvutia Uwekezaji wa Mtaji wa Nje, ambapo mtaji uliongezeka kutoka dola bilioni 8.64 mwaka 2022 hadi dola bilioni 9.15 mwaka 2023 na kufikia dola bilioni 9.79 mwaka 2024.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, anasema kuwa mafanikio hayo yamechochewa na mageuzi yanayoendelea chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na usimamizi wa sekta ya madini.
Ongezeko hili ni matunda ya uhamasishaji wa uwekezaji, mazingira wezeshi kwa wawekezaji, upanuzi wa miradi iliyopo, uwekezaji wa faida zinazozalishwa ndani ya sekta na uunganishaji wa mitaji.
Katika miaka ya hivi karibuni, Sekta ya Madini Tanzania imeendelea kuvutia kampuni mbalimbali za ndani na nje ya nchi ambazo zimeingia katika ushirikiano na Serikali katika maeneo ya utafutaji, uchimbaji na uongezaji thamani wa madini. Mwelekeo huu unaonesha kuwa ukuaji wa sekta si wa bahati mbaya, bali ni matokeo ya sera zilizo wazi, mifumo iliyoboreshwa na imani inayoongezeka kwa mazingira ya uwekezaji nchini.
Mbali na kuvutia uwekezaji, Tanzania pia imekuwa ni sehemu ya rejea katika mijadala ya maendeleo ya sekta ya madini barani Afrika. Nchi mbalimbali zikiwemo Zambia, Uganda, Kenya, Burkina Faso, Sudani ya Kusini, Malawi, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tayari zimefika nchini kujifunza uzoefu wa Tanzania katika maeneo ya usimamizi wa sekta, ushirikishwaji wa wananchi, uendeshaji wa masoko ya madini na namna ya kuongeza mchango wa Sekta katika uchumi wa taifa.
Hali hiyo inaonesha kuwa Tanzania si mnufaika wa mageuzi ya sekta ya madini pekee, bali pia imeanza kuwa chanzo cha uzoefu na maarifa kwa nchi nyingine zinazotafuta namna bora ya kuendeleza rasilimali zao za madini kwa manufaa ya wananchi.
Kupitia hotuba yake ya bajeti aliyoisoma bungeni, Waziri Mavunde anaeleza kuwa, mwelekeo wa siku zijazo utaendelea kujikita katika kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa madini, kuimarisha matumizi ya teknolojia katika uchimbaji na uchenjuaji, kuongeza shughuli za uongezaji thamani wa madini pamoja na kuhakikisha sekta inachangia zaidi katika ajira, mapato ya Serikali na ukuaji wa uchumi wa taifa.
Fauka ya hayo, Tanzania inaendelea kutajwa katika tathmini mbalimbali za kimataifa si kwa sababu ya utajiri wa madini pekee, bali kutokana na mchanganyiko wa rasilimali, sera zinazoendelea kuimarishwa, ongezeko la uwekezaji, ushiriki wa wananchi na usimamizi unaojenga imani kwa wadau wa sekta. Huu ndio msingi unaoifanya Tanzania kuendelea kujijengea nafasi muhimu zaidi katika ramani ya madini duniani na kuifanya sekta ya madini kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa nchi.