SGR na Meli Mpya Zaibadili Kigoma Kuwa Lango la Biashara Afrika Mashariki na Kati
Na Scolastica Sambi – MAELEZO
Mkoa wa Kigoma umekuwa na nafasi ya kimkakati katika biashara ya kikanda kutokana na mwambao wake katika Ziwa Tanganyika na ukaribu wake na Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia. Hata hivyo, changamoto za miundombinu ya usafirishaji zimekuwa zikizuia mkoa huo kutumia kikamilifu fursa hiyo, huku gharama za usafirishaji zikiwa kubwa na safari za mizigo kuchukua muda mrefu.
Sasa hali hiyo imeanza kubadilika kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali, ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Tabora–Kigoma, uzinduzi wa meli nne mpya za mizigo katika Ziwa Tanganyika pamoja na maboresho ya Bandari ya Kigoma.
Miradi hiyo inatarajiwa kuibadili Kigoma kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku ikiimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la biashara kwa nchi zisizo na bandari.
Katika kuonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya uchukuzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua meli nne mpya za mizigo, akaweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Tabora–Kigoma na kukagua maendeleo ya maboresho ya Bandari ya Kigoma. Hatua hizo zinaakisi mkakati wa Serikali wa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ili kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara.

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, anasema Kigoma itaendelea kuwa lango kuu la biashara kuelekea Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia kutokana na nafasi yake ya kipekee katika Ziwa Tanganyika.
Anasema kukamilika kwa Reli ya Kisasa ya Tabora–Kigoma, meli mpya za mizigo na maboresho ya Bandari ya Kigoma kutaifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Kwa nafasi yake ya kipekee katika Ziwa Tanganyika, Kigoma itaendelea kuwa lango kuu la biashara kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Zambia. Miradi hii ya SGR na meli mpya za mizigo itaifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” anasema Prof. Mbarawa.
Meli hizo nne mpya, ambazo kila moja ina uwezo wa kubeba tani 2,000 za mizigo, zinatarajiwa kuongeza uwezo wa Bandari ya Kigoma kuhudumia zaidi ya tani 832,000 za mizigo kwa mwaka. Mbali na kuongeza ufanisi wa usafirishaji, uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali, kuchochea biashara na kuzalisha takribani ajira 600 za moja kwa moja katika sekta mbalimbali.
Kwa wakazi wa Kigoma, uwekezaji huo una maana zaidi ya kujengwa kwa miundombinu. Ni mwanzo wa zama mpya za fursa za kiuchumi, ajira na uwekezaji. Kuimarika kwa usafiri wa reli na majini kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa, kupanua masoko na kuvutia wawekezaji ndani na nje ya nchi.
Bi. Asha Mussa, mkazi wa Kibirizi, anasema wananchi wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu maendeleo ya aina hiyo.
“Tunaamini meli mpya na reli ya kisasa zitafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi. Kuimarika kwa miundombinu ya usafiri kutasaidia wafanyabiashara, vijana na wajasiriamali kupata nafasi zaidi za kujikwamua kiuchumi.”
Hisia kama hizo zinaungwa mkono na wananchi wengi wanaoamini kuwa miradi hiyo itakuwa suluhisho la changamoto zilizokuwa zikiikabili sekta ya usafirishaji kwa miaka mingi.
Bw. John Mwakalinga, mkazi wa Kigoma Mjini, anasema gharama kubwa za usafirishaji zimekuwa zikikwamisha biashara na kupunguza ushindani wa bidhaa katika masoko.
“Kwa miaka mingi usafirishaji wa bidhaa ulikuwa na changamoto nyingi na gharama kubwa. Tunaamini SGR pamoja na maboresho ya bandari utarahisisha usafirishaji wa bidhaa kwenda masoko ya ndani na nchi jirani, kuongeza ushindani wa wafanyabiashara na kuinua kipato cha wananchi.”
Mradi wa Reli ya Kisasa wa Tabora–Kigoma wenye urefu wa kilometa 506 unajengwa kwa gharama ya takribani dola za Marekani bilioni 2.7. Mradi huo utaunganisha Kigoma na mtandao wa reli ya kisasa unaofika Dar es Salaam, hivyo kuimarisha Ushoroba wa Kati kwa kurahisisha usafirishaji wa mizigo kati ya Tanzania na Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na Zambia.

Faida za miradi hiyo hazitaishia katika kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo na abiria pekee. Pia zinatarajiwa kuongeza ushindani wa biashara za kikanda, kuvutia uwekezaji, kuchochea uzalishaji wa bidhaa na kuongeza mchango wa sekta ya uchukuzi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kadri miradi hiyo inavyoendelea kukamilika, Kigoma inaelekea kujidhihirisha kama kitovu kipya cha biashara katika Afrika Mashariki na Kati. Uwekezaji wa Serikali katika reli, bandari na usafiri wa majini unaweka msingi imara wa maendeleo endelevu, kuongeza fursa za ajira na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Kwa hakika, kukamilika kwa Reli ya Kisasa ya Tabora–Kigoma, kuanza kwa huduma za meli mpya za mizigo na maboresho ya Bandari ya Kigoma kutafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kiuchumi. Kigoma itaimarika kama lango kuu la biashara katika ukanda huu, huku Tanzania ikiendelea kujijengea nafasi kama kitovu muhimu cha usafirishaji na biashara Afrika Mashariki na Kati.