Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na. Timothy Mwakyenda – MAELEZO Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewataka Watanzania kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini ili kukuza viwanda vya ndani, kulinda ajira, kuongeza mapato ya taifa na kuimarisha uchumi wa wananchi. Ameyasema hayo tarehe 4 Novemba, 2026 jijini Dodoma, alipokuwa akizindua Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Ujasiriamali Mdogo na wa Kati ya mwaka 2003, toleo la mwaka 2025, ambapo alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Amesema kuwa sera hizo zinatarajiwa kuimarisha uzalishaji wa bidhaa nchini, kupanua fursa za biashara na uwekezaji na kuwezesha wajasiriamali kukua kutoka biashara ndogo kwenda za kati na kubwa, hatua itakayochochea upatikanaji wa ajira na kuongeza kipato cha wananchi na kusisitiza kuwa watanzania wana wajibu wa kuunga mkono viwanda vya ndani kwa kununua bidhaa zake. Viwanda vinapopata soko la uhakika vinaweza kuongeza uzalishaji, kuajiri watu wengi zaidi na kuchangia mapato ya serikali kupitia shughuli za kiuchumi. Amesema ni muhimu kubadili mtazamo kuhusu wawekezaji na wafanyabiashara kwa kuwachukulia kama washirika muhimu wa maendeleo ya taifa, badala ya kuwawekea mazingira yanayokwamisha shughuli zao na kueleza kuwa sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika uwekezaji, uzalishaji na ajira kwa vijana. Aidha ameongeza kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, huku akizitaka wizara na taasisi husika kuondoa vikwazo visivyo vya lazima vinavyoweza kudhoofisha shughuli za biashara na kusistiza kuwa kama sheria zinapokuwa kikwazo kwa maendeleo ya wananchi, zinapaswa kufanyiwa marekebisho ili ziendane na mahitaji ya sasa ya uchumi. Pamoja na hayo Dkt. Nchemba amezitaka sekta ya viwanda na biashara, kwa kushirikiana na wizara nyingine na sekta binafsi, kusimamia utekelezaji wa sera hizo kwa kuweka mikakati inayopimika na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mara kwa mara na kusisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na rasilimali nyingine za nchi kabla ya kuuzwa katika masoko ya ndani na nje. Pia, amesema kuwa serikali itaendelea kuboresha miundombinu wezeshi, ikiwemo nishati, maji, barabara na reli, ili kupunguza changamoto za uzalishaji na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kubainisha kuwa mazingira bora ya uzalishaji yatawezesha viwanda kuongeza tija na ushindani, huku wananchi wakinufaika kupitia bidhaa zinazopatikana kwa uhakika na fursa nyingi zaidi za kiuchumi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuimarisha usimamizi wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini kwa kuongeza ufuatiliaji wa masuala yanayohusu haki za wananchi badala ya kutegemea malalamiko pekee. Akizungumza Novemba 2, 2026, alipokuwa akiwaapisha viongozi wateule katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Mhe. Rais amesema Tume hiyo inapaswa kuwa na utaratibu wa kubaini na kufuatilia changamoto za ukiukwaji wa haki za binadamu katika taasisi na sekta mbalimbali na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa. Amesema Tume hiyo pia inapaswa kufuatilia tuhuma na shutuma zinazoikabili Tanzania kuhusu haki za binadamu katika majukwaa ya kimataifa na kutoa majibu kwa kuzingatia ukweli na hali halisi ya ndani ya nchi. Nawaambieni sana ninyi vijana, mna uwezo wa kuperuzi mitandao yote na kuona yanayotokea duniani, mkaona shutuma tunazopewa na mkaweza kuzijibu. Ameongeza kuwa jukumu la Tume hiyo halipaswi kuishia katika kupokea malalamiko ya wananchi, bali pia kufuatilia maeneo ambayo kuna viashiria vya ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili kuhakikisha haki zinalindwa. Katika hatua nyingine, Mhe. Rais amewataka viongozi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Migogoro ya Wafanyakazi kusimamia haki za wafanyakazi na waajiri kwa kuzingatia sheria, akisisitiza kuwa maamuzi yao yanapaswa kutolewa bila chuki, hila wala upendeleo. Amesema ukuaji wa uwekezaji na shughuli za sekta binafsi unaweza kuongeza migogoro ya kikazi, hivyo wanapaswa kujiandaa kukabiliana nayo kwa weledi. Miongoni mwa viongozi walioapishwa ni Bw. Dunford George Mpelumbe, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; Bw. Omar Ali Omar, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo; Bi. Angeline Lubala Mabula, Mkuu wa Mkoa wa Tabora; pamoja na Jaji Mstaafu Wilfred Peter Dyansobera, Mwenyekiti wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Migogoro ya Wafanyakazi, na makamishna wa Tume hiyo. Mhe. Rais amewapongeza viongozi wote walioapishwa na kuwatakia mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa Serikali ina matarajio makubwa ya kuona wanatekeleza dhamana walizopewa kwa uadilifu na kuzingatia maslahi ya wananchi.