Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Bilioni 2 za Mirabaha Kuwanufaisha Wasanii Nchini Na Josephina Lupasha – MAELEZO Takribani shilingi bilioni mbili zilizokusanywa kutokana na matumizi ya kazi za wasanii kupitia mfumo wa mirabaha zinatarajiwa kugawiwa kwa wasanii nchini, hatua inayolenga kuhakikisha wabunifu wananufaika na kazi zao na kuongeza mchango wa sekta ya sanaa katika ajira, kipato na uchumi wa Taifa. Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 24, 2026, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji, usimamizi na ugawaji wa mirabaha kwa uwazi na ufanisi, ili wasanii wanufaike ipasavyo na kazi zao. Sheria imeweka utaratibu kupitia COSOTA wa kulinda haki miliki na namna ya kugawa mirabaha. Zipo fedha takribani shilingi bilioni mbili ambazo zinapaswa kutolewa kama gawio kwa wasanii wetu. Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha sekta ya sanaa na kuifanya kuwa chanzo endelevu cha ajira, kipato na fursa za kiuchumi kwa wasanii, huku ikichangia katika maendeleo ya Taifa. Katika hatua nyingine, Waziri Makonda amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), huku ikilenga kuhakikisha mashindano hayo yanakuwa fursa ya kiuchumi kwa Watanzania katika sekta mbalimbali. Amesema maandalizi hayo yanahusisha miundombinu na huduma muhimu, zikiwemo usafiri, malazi, utangazaji, ujenzi wa chapa, huduma za lugha, upigaji picha, uzalishaji wa maudhui ya televisheni, huduma za matibabu na huduma za kiufundi. Amesema fursa zitakazotokana na AFCON 2027 zinapaswa kutumiwa ipasavyo na Watanzania kwa kujiandaa na kushiriki katika huduma mbalimbali zitakazohitajika kabla na wakati wa mashindano hayo. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali2 katika maandalizi ya matukio makubwa ya kitaifa na kimataifa yanayotarajiwa kufanyika nchini katika kipindi cha mwaka 2026/2027, kwa lengo la kuongeza fursa za kiuchumi, ajira na kuitangaza Tanzania kimataifa.