Na Mwandishi Wetu – Mbeya Upatikanaji wa maji safi na ya uhakika ni msingi muhimu wa afya bora, ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali inawekeza Shilingi bilioni 119 katika Mradi wa Kimkakati wa Maji kutoka Mto Kiwira, unaolenga kukidhi mahitaji ya maji ya wananchi wa Mbeya na kuchochea maendeleo ya kiuchumi hadi mwaka 2045. Mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuboresha huduma za kijamii na kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu kwa uhakika. Kukamilika kwake kunatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi kutoka asilimia 90 hadi asilimia 100, huku wananchi wa Jiji la Mbeya, Mji wa Mbalizi na maeneo jirani wakitarajiwa kupata maji saa 24 kwa siku. Akikagua maendeleo ya mradi huo katika eneo la Forest Mpya, jijini Mbeya, Oktoba 16, 2026, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka viongozi na watendaji wa Sekta ya Maji kuongeza kasi ya utekelezaji ili mradi ukamilike kwa wakati na kuwawezesha wananchi kupata huduma hiyo ifikapo Julai 2027. Amesisitiza kuwa Mbeya ni mkoa wa kimkakati katika uchumi wa taifa, hivyo huduma ya maji ya uhakika ni muhimu katika kuimarisha biashara, uzalishaji na shughuli nyingine za kiuchumi. Upatikanaji wa maji ya kutosha utasaidia pia kuboresha afya za wananchi na kuweka mazingira bora kwa shughuli za uzalishaji na uwekezaji. Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kusimamia kikamilifu fedha za umma zinazowekezwa katika miradi ya maendeleo, akiwataka viongozi kuhakikisha kila shilingi inayotumika inaleta thamani na matokeo yanayoonekana kwa wananchi. Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, amewahakikishia wananchi wa mkoa huo kuwa Wizara ya Maji itaendelea kusimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, huku akiwataka watendaji na wataalamu kuongeza kasi ya kazi. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWSA), mradi huo umefikia asilimia 49 ya utekelezaji. Ujenzi wa banio la maji umefikia asilimia 98, tenki la maji katika eneo la Forest Mpya asilimia 80, na ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji asilimia 15. Tenki hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni tano za maji. Mradi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa jumla wa uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 78 hadi milioni 195 kwa siku, hatua itakayosaidia kukidhi mahitaji ya wananchi yanayotarajiwa hadi mwaka 2045. Kwa ujumla, uwekezaji huu wa Shilingi bilioni 119 unaonesha umuhimu wa kuunganisha huduma za msingi na maendeleo ya uchumi. Kukamilika kwa mradi kwa wakati kutapanua upatikanaji wa maji, kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha msingi wa maendeleo endelevu ya Mkoa wa Mbeya.