Na Baraka Messa – MAELEZO Watanzania wamejitokeza kwa wingi kumpokea kwa shangwe na nderemo Miss Grand International 2026, Jihan Dimack, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Oktoba 17, 2026, baada ya kutwaa taji hilo katika mashindano yaliyofanyika Bangkok, Thailand. Mapokezi hayo yamekuwa ya kishindo, huku mashabiki wa urembo na wadau wa sanaa wakijitokeza kumpongeza kwa ushindi huo wa kihistoria, unaoendelea kuitangaza Tanzania kimataifa na kuonyesha mshikamano wa Watanzania katika kuunga mkono mafanikio ya mmoja wao. Akizungumza katika mapokezi hayo, Rais wa Shirikisho la Sanaa za Maonyesho Tanzania (SHISAMA) Cythinia Hanjewele amesema ushindi wa Jihan umeongeza wigo wa kuitangaza Tanzania duniani, akibainisha kuwa awali muziki na sanaa za maonyesho ndizo zilizokuwa zikipeleka jina la nchi kimataifa. Tulizoea muziki na sanaa za maonyesho kututangaza duniani, lakini ushindi wa Jihan unaonyesha kuwa tuna fursa nyingine kupitia mashindano ya urembo kuitangaza Tanzania na uwezo wa Watanzania. Naye mtengenezaji wa maudhui ya kidijitali, Vicent Njau maarufu Kiredio, amesema ushindi wa Jihan ni ishara muhimu kuelekea maandalizi ya mashindano ya Miss World yanayotarajiwa kufanyika Tanzania pamoja na michuano ya AFCON 2027, akisisitiza umuhimu wa kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ya taifa. Amesema mitandao ya kijamii ina nguvu kubwa na inaweza kuwa chanzo cha kipato ikiwa itatumika vizuri, hivyo Watanzania wanapaswa kutumia fursa hiyo kuitangaza nchi, kuvutia wageni na kukuza shughuli za kiuchumi kupitia sanaa, utalii na maudhui ya kidijitali.