Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO Serikali inajenga kituo maalum cha wanahabari jijini Dodoma, kitakachojulikana kama Tanzania Media Center, kwa lengo la kuwawezesha waandishi wa habari kupata eneo salama na rafiki kwa ajili ya kuandaa habari, kufanya mahojiano na kutekeleza shughuli zao za kitaaluma wanapokuwa katika majukumu ya kikazi mjini humo. Akizungumza Oktoba 31, 2026, katika Kongamano la Mwaka la Tathmini ya Huduma za Habari na Mawasiliano Vijijini Tanzania, lililowakutanisha wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini (RUJAT), jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kituo hicho kinajengwa eneo la Mzunguni jijini Dodoma na kitakuwa na ghorofa mbili pamoja na maeneo maalum kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wanahabari. Amesema ujenzi wa kituo hicho unalenga kutatua changamoto ya ukosefu wa eneo maalum la kufanyia kazi inayowakabili waandishi wengi wa habari wanapofika Dodoma kwa shughuli za kikazi, hali inayowalazimu kutumia vyumba vya hoteli au maeneo mengine yasiyo rasmi kuandaa habari na kufanya mahojiano, jambo linaloweza kuhatarisha usalama na usiri wa taarifa. Ameeleza kuwa kituo hicho kitakuwa sehemu ya kukutanisha wanahabari, kufanya kazi na kupokea watu wanaohitaji kutoa mahojiano, hivyo kuwawezesha kutekeleza majukumu yao katika mazingira yanayozingatia mahitaji ya taaluma ya habari. Aidha, amesema ukumbi uliopo katika ofisi za Idara ya Habari utaendelea kutumika kutoa huduma kwa waandishi wa habari wanaofika Dodoma kwa shughuli mbalimbali za kikazi. Katika hatua nyingine, Msigwa amewataka waandishi wa habari kuimarisha weledi na kuandika habari zinazogusa maisha ya wananchi, hususan wanaoishi vijijini, akibainisha kuwa sehemu kubwa ya Watanzania wanaishi katika maeneo ya vijijini, lakini vyombo vingi vya habari vimeelekeza nguvu zaidi katika kuripoti matukio ya mijini. Amesisitiza kuwa wanahabari wanapaswa kufanya uchunguzi wa kina na kufuatilia changamoto zinazowakabili wananchi hadi pale zinapopatiwa ufumbuzi. Akitolea mfano, amesema taarifa za habari kuhusu changamoto za upatikanaji wa maji na dawa zimekuwa zikichochea hatua za kutatua matatizo hayo. Vilevile, amesisitiza umuhimu wa mafunzo endelevu, matumizi ya teknolojia na uandishi unaozingatia ushahidi pamoja na maslahi ya umma. Amewataka wanahabari kujiepusha na vitendo vinavyoweza kushusha heshima ya taaluma ya habari na badala yake kuimarisha ushirikiano kati yao na maafisa habari wa Serikali.