Rais Samia, Lourenço Kutumia SGR ni Ishara ya Maendeleo ya Sekta ya Usafirishaji Tanzania
Na Timothy Mwakyenda – MAELEZO
Safari iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço, kwa kutumia treni ya kisasa inayotumia nishati ya umeme kupitia reli ya SGR kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma, Oktoba 30, 2026, ni hatua yenye ujumbe mpana kuhusu maendeleo ya sekta ya usafirishaji nchini Tanzania. Mbali na kuonesha kuimarika kwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, safari hiyo imeonesha uwezo wa Tanzania kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya reli na kutoa huduma za usafiri zinazokidhi mahitaji ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Viongozi hao walianza safari yao katika Stesheni ya Magufuli jijini Dar es Salaam kuelekea Dodoma kushiriki hafla ya uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba pamoja na barabara zake za lami. Matumizi ya SGR katika safari hiyo yanaonesha namna reli ya kisasa inavyoweza kuwa kiungo muhimu katika kurahisisha usafiri wa watu na usafirishaji wa bidhaa, huku ikitoa fursa kwa viongozi na wageni wa kimataifa kujionea maendeleo ya miundombinu ya usafiri nchini.
Hatua hiyo pia ni kielelezo cha ukuaji na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya usafirishaji Tanzania, hususan katika kuimarisha usalama, ufanisi na ubora wa huduma za reli. Reli ya SGR ina nafasi muhimu katika kupunguza muda wa safari, kurahisisha usafiri wa wananchi na kutoa huduma inayoweza kukidhi mahitaji ya makundi mbalimbali, yakiwemo wafanyabiashara, watalii na wasafiri wengine. Hivyo, uwekezaji huo una mchango katika kukuza shughuli za kiuchumi na kuimarisha ushindani wa Tanzania kama kitovu cha usafirishaji katika ukanda huu wa Afrika.
Akizungumza kabla ya safari hiyo, Rais Samia alisema matumizi ya SGR yanaonesha dhamira ya Tanzania na Angola ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafirishaji, hususan reli, kwa lengo la kurahisisha usafiri wa watu na usafirishaji wa bidhaa kati ya nchi hizo na maeneo mengine ya Afrika.
Alisema Tanzania inaendelea na ukarabati wa reli ya TAZARA inayounganisha nchi hiyo na Zambia kupitia Kapiri Mposhi, huku Angola nayo ikiendelea na ukarabati wa reli ya Benguela. Hatua hizo zinatarajiwa kuimarisha muunganiko wa reli na kurahisisha biashara katika ukanda huo.
Katika mazungumzo yetu tumekubaliana tuunganishe korido zetu kati ya Benguela na korido ya ukanda wa Kati ya Tanzania ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa. Ndiyo maana tumeamua kutumia usafiri huu kuonesha kwamba inawezekana
Kwa mtazamo mpana, matumizi ya SGR kwa viongozi hao ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania katika medani za kimataifa kama nchi inayopiga hatua katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya usafiri. Reli hiyo inatoa taswira ya Tanzania inayowekeza katika teknolojia na huduma zinazokidhi mahitaji ya sasa na zijazo, huku ikiimarisha uwezo wa nchi kuwahudumia wananchi na wageni wanaoitembelea. Aidha, kuunganisha korido za reli za Tanzania na Angola kunaweza kufungua fursa kubwa zaidi za biashara, utalii, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika.
Kwa ujumla, safari hiyo imebeba ujumbe kwamba SGR si mradi wa usafiri pekee, bali ni sehemu ya mkakati mpana wa maendeleo ya taifa. Ni miundombinu inayopaswa kuendelea kutunzwa, kuboreshwa na kutumiwa ipasavyo ili kuimarisha usalama, kuongeza ufanisi wa usafirishaji na kuchochea uchumi. Hatua hiyo inaweka msingi wa Tanzania kuendelea kujijengea nafasi kama kitovu muhimu cha usafiri na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.