Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Blogu

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka nchi za Afrika kujenga uwezo wa ndani wa kugharamia, kusimamia na kuzalisha mahitaji muhimu ya huduma za afya, badala ya kuendelea kutegemea misaada na mifumo kutoka nje. Dkt. Mwigulu ameyasema hayo, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi unaofanyika jijini Arusha, ukishirikisha zaidi ya washiriki 2,700 kutoka mataifa 27. Amesema wakati umefika kwa Afrika kubadili namna inavyoelewa na kutekeleza dhana ya kujenga uwezo, akisisitiza kuwa dhana hiyo haipaswi kuishia katika miradi midogo isiyojenga uwezo wa kudumu, bali ielekezwe katika uwekezaji wa uzalishaji wa dawa, vifaa tiba, teknolojia na wataalamu. Enzi zile nikiwa Waziri wa Fedha nilikuwa nawaambia nchi za Afrika zimeshashuhudia muda mrefu sasa wa maisha ya misaada na misaada inayoelekezwa pengine katika maeneo ambayo yanatofautiana na malengo ya ndani ya nchi kwa jina la capacity building. Capacity building. Capacity building. Na ndio tunaishia chapati, mandazi, sambusa. Hatuwekezi kitu kitakachodumu na kikawa endelevu. Kwa mujibu wa Dkt. Mwigulu, malengo ya ndani ya nchi yanayokwenda sambamba na Malengo ya Maendeleo Endelevu yanapaswa kuheshimiwa na washirika wa maendeleo, ili misaada na uwekezaji katika sekta ya afya viweze kuacha matokeo ya kudumu kwa wananchi wa Afrika. Amesema Tanzania inaendelea kuweka nguvu katika kuimarisha huduma za afya kwa kuongeza miundombinu, rasilimali watu pamoja na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, ambayo Serikali imeanza kuitekeleza mwaka 2026. Tunapozungumza kuhusu afya ya msingi, tusizungumzie tu kujenga vituo vya afya. Tujenge pia uwezo wa nchi zetu kugharamia huduma hizo, kuzalisha mahitaji yake na kutumia teknolojia zetu wenyewe. Ameongeza kuwa Tanzania imeanza kuwekeza katika uwezo wa ndani wa uzalishaji wa dawa kwa lengo la kupunguza utegemezi wa misaada na kuhakikisha upatikanaji wa dawa unaendelea kuwa wa uhakika, hususan wakati dunia inapokumbwa na changamoto zinazoathiri minyororo ya usambazaji. Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya watumishi wa afya, ikiwemo ujenzi wa nyumba za watumishi na kuongeza ajira katika sekta hiyo, hatua ambazo zitasaidia kuimarisha upatikanaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Dkt. Mwigulu amesema mkutano huo unapaswa kuzaa hatua mahsusi zinazoweza kutekelezwa na kupimwa, badala ya kuishia katika mijadala na maazimio yasiyotekelezwa. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Dkt. Jean Kaseya, amesema Afrika ya mwaka 2026 si Afrika ya mwaka 1960 na kwamba wakati umefika kwa washirika wa maendeleo kubadili namna wanavyoshirikiana na Serikali za Afrika. Dkt. Kaseya amesema Serikali za Afrika zinapaswa kuwa na umiliki na uelewa wa rasilimali zinazotolewa kwa ajili ya afya, huku fedha za washirika wa maendeleo zikiendana na mipango na vipaumbele vya kitaifa. Naye Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Profesa Mohammed Janabi, amesema changamoto kubwa kwa Afrika si kukosa suluhisho katika sekta ya afya, bali ni kukosa ujasiri wa kuyafadhili, nidhamu ya kuyatekeleza na uwajibikaji wa kuyadumisha. Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, amesema Serikali itaendelea kuongeza uwekezaji katika afya ya msingi kwa kuwa ndiyo ngazi inayohudumia wananchi wengi zaidi nchini. Amesema asilimia 95.6 ya wajawazito wanaojifungua nchini wanapata huduma katika ngazi ya afya ya msingi, huku asilimia 86 ya mahudhurio ya wagonjwa wa nje katika vituo vya umma yakihudumiwa katika ngazi hiyo. Profesa Shemdoe amesema kati ya vituo 8,288 vya afya vinavyomilikiwa na Serikali, vituo 7,946 sawa na asilimia 95.8 ni vya ngazi ya afya ya msingi, hivyo kuongeza uwekezaji katika ngazi hiyo ni kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja kwa wananchi wengi nchini. Mkutano huo wa siku tatu unajadili namna ya kuimarisha huduma za afya ya msingi kuelekea upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, kupitia ufadhili endelevu, ufanisi, ubora wa huduma, ubunifu, ushirikiano wa kikanda na kujenga mifumo ya afya inayostahimili majanga. Kwa ujumla, mkutano huo unalenga kuhimiza Afrika kujenga mifumo ya afya inayojitegemea, yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za ndani na za kimataifa, huku ikiweka mkazo katika uwekezaji wa muda mrefu, uzalishaji wa ndani, rasilimali watu na matumizi ya teknolojia ili kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wananchi wote.

Na Baraka Messa – Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewataka Maafisa Habari wa Serikali na Taasisi za Umma kuongeza ubunifu na weledi katika utoaji wa taarifa kwa umma kwa kuangazia zaidi uwekezaji unaofanywa na Serikali na matokeo yake katika kuboresha maisha ya wananchi. Msigwa ametoa wito huo Septemba 9, 2026, jijini Dodoma, wakati akiwakaribisha na kuwapa maelekezo Maafisa Habari wapya walioajiriwa katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, katika Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali, Mtumba. Amesema wajibu wa Maafisa Habari ni kuhakikisha wananchi wanafahamu kwa wakati hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuleta maendeleo, ikiwemo uwekezaji katika miundombinu, elimu, afya, maji, nishati, usafiri, teknolojia na sekta nyingine zinazogusa maisha yao. Kazi yetu ni kuhabarisha wananchi. Tueleze Serikali imefanya nini, inafanya nini na inatarajia kufanya nini, kwa sababu hayo ndiyo mambo yanayowagusa wananchi. Amesema katika kutekeleza wajibu huo, Maafisa Habari wanapaswa kuwasilisha taarifa zinazoonesha kwa uwazi uwekezaji uliofanyika, miradi inayotekelezwa, thamani ya uwekezaji huo, hatua iliyofikiwa na matokeo yanayopatikana, ili wananchi waweze kutambua namna rasilimali za Serikali zinavyotumika katika kuleta maendeleo. Msigwa amesema taarifa za utekelezaji wa Serikali zinapaswa kwenda zaidi ya kueleza tukio, badala yake zioneshe maana ya mradi kwa mwananchi, ikiwemo huduma zitakazopatikana, fursa zitakazozalishwa, ajira zitakazoongezeka na mchango wake katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Amesema Maafisa Habari wana nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaelewa mipango na vipaumbele vya Serikali, pamoja na kutambua hatua zinazochukuliwa katika kutatua changamoto zinazowakabili. Taarifa nzuri si ile inayosema tu mradi umejengwa, bali ieleze mradi huo umejengwa kwa gharama gani, unahudumia wananchi wangapi na umeleta mabadiliko gani katika maisha yao. Aidha, amewataka Maafisa Habari kutumia ipasavyo teknolojia za kisasa na majukwaa ya kidijitali, hususan mitandao ya kijamii, katika kufikisha taarifa za maendeleo kwa wananchi kwa lugha rahisi, yenye mvuto na inayoeleweka kwa makundi mbalimbali. Amesema matumizi ya teknolojia yanatoa fursa ya Serikali kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja, hivyo Maafisa Habari wanapaswa kutumia ubunifu katika kuandaa maudhui yanayowapa wananchi uelewa wa shughuli, miradi na uwekezaji unaofanywa na Serikali. Vilevile, Msigwa amewataka Maafisa Habari hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wakizingatia misingi ya uadilifu, weledi, uwajibikaji na maslahi mapana ya umma. Amesema Maafisa Habari ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi, hivyo wanapaswa kuhakikisha taarifa wanazozitoa zinajenga uelewa kuhusu maendeleo yanayotekelezwa na Serikali na kuwasaidia wananchi kutambua fursa na manufaa yanayotokana na uwekezaji huo. Msigwa amesisitiza kuwa, kupitia taarifa sahihi, zenye ushahidi na zinazoonesha matokeo, Maafisa Habari wanaweza kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya rasilimali za Taifa na mchango wa uwekezaji wa Serikali katika kuboresha huduma na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Na Bupe Mwaiseje – Dodoma Elimu ya juu ni moja ya nguzo muhimu katika kujenga Taifa lenye wataalamu, wabunifu na vijana wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uchumi. Kutambua umuhimu huo, Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kuongeza fursa za elimu na kuwaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na ujasiriamali. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imewekeza jumla ya Sh bilioni 67.9 katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), uwekezaji unaolenga kuongeza uwezo wa taasisi hiyo kutoa elimu bora na kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa na ujuzi wa kuajiriwa au kujiajiri. Uwekezaji huo umeleta mabadiliko yanayoonekana katika ukuaji wa TIA, kuanzia upanuzi wa kampasi, ongezeko la wanafunzi, maboresho ya programu za masomo, uimarishaji wa rasilimali watu na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za elimu. Akizungumza kuhusu utekelezaji wa shughuli za TIA kwa mwaka wa fedha 2026/27 katika Ukumbi wa Idara ya Habari–MAELEZO, Mtumba jijini Dodoma, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Amos Palangyo, amesema uwekezaji huo umeelekezwa katika kuboresha miundombinu kwenye kampasi za Mtwara, Mbeya, Singida, Kigoma, Mwanza na Zanzibar. Mbali na uwekezaji wa Sh bilioni 67.9, TIA imepata Sh bilioni 27.8 kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET). Fedha hizo zimeelekezwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo miundombinu, TEHAMA, samani, mafunzo ya wahadhiri, maboresho ya mitaala, tathmini na shughuli nyingine za mradi. Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 22.6 zimetumika moja kwa moja katika ujenzi wa miundombinu ya Kampasi za Singida na Mwanza. Matokeo ya uwekezaji huo yanaonekana katika upanuzi wa TIA kutoka kuwa na kampasi sita mwaka 2021/22 hadi kufikia kampasi nane mwaka 2025/26, baada ya kuongezwa kwa kampasi za Tanga na Zanzibar. Ukuaji huo umeenda sambamba na ongezeko la idadi ya wanafunzi. Kutoka wanafunzi 24,494 mwaka 2021/22, idadi hiyo imefikia 37,397 mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 52.7. Wakati huohuo, uwezo wa taasisi kuhudumia wanafunzi umeongezeka kwa asilimia 35. Haya si mabadiliko ya miundombinu pekee; ni upanuzi wa fursa kwa Watanzania wengi zaidi kupata elimu ya juu na ujuzi unaohitajika katika kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya Taifa. Katika kuhakikisha elimu inayotolewa inaendana na mahitaji ya uchumi wa sasa, TIA imeongeza programu za masomo kutoka 49 hadi 54. Miongoni mwa programu hizo ni Shahada ya Maendeleo ya Biashara na Ujasiriamali pamoja na Shahada ya Uchumi na Fedha, ambazo zinalenga kuwajengea vijana uwezo katika biashara, ujasiriamali, uchumi na usimamizi wa fedha. Kwa upande wa mikopo ya elimu ya juu, wanafunzi 19,342 katika kampasi za Tanga, Dar es Salaam, Mwanza, Singida, Mbeya, Kigoma na Mtwara wamenufaika na mikopo hiyo. Aidha, jumla ya wahitimu 62,680 wamehitimu na kuingia katika maeneo mbalimbali ya ajira, ujasiriamali na huduma za kitaaluma. Prof. Pallangyo anasema ubora wa elimu hauwezi kutenganishwa na ubora wa walimu na wahadhiri. Kwa kutambua hilo, Serikali imeiwezesha TIA kupata maprofesa tisa na kugharamia watumishi 78 kusoma Shahada za Uzamivu (PhD) ndani na nje ya nchi. Kati yao, watumishi 48 tayari wamehitimu, huku 30 wakiendelea na masomo. Hatua hiyo imeongeza uwezo wa TIA katika ufundishaji, utafiti, ubunifu na uzalishaji wa maarifa. Sambamba na hilo, taasisi imeanzisha programu za Shahada ya Uzamili katika kampasi za Zanzibar, Mbeya, Singida na Mwanza. Hivyo, uwekezaji katika rasilimali watu unaendelea kuifanya TIA kuwa taasisi inayozalisha wahitimu pekee wenye maarifa na ubunifu unaoweza kutumika katika kutatua changamoto za jamii. Moja ya mafanikio yanayoipa thamani zaidi elimu inayotolewa TIA ni juhudi za kuwaunganisha wanafunzi na fursa za ajira na ujasiriamali. Zaidi ya wanafunzi 5,000 wamefikiwa kupitia warsha zinazohusu ujasiriamali, ubunifu, ajira na fursa za kimataifa. Wakati huohuo, zaidi ya wanafunzi 500 wamepatiwa mafunzo mahsusi ya ujasiriamali na takribani 100 wamewezeshwa kuanzisha biashara ndogo ndogo. Anasema mfano wa matokeo ya juhudi hizo ni Nicolaus Carol Mboya, mmoja wa wahitimu wa TIA ambaye ameanzisha kampuni ya STEAMORA inayotoa mafunzo ya teknolojia ya elimu kwa watoto na vijana. Kupitia STEAMORA, vijana wanapata mafunzo katika teknolojia mbalimbali ikiwemo roboti, upangaji programu (coding), ubunifu wa miundo ya pande tatu (3D) na akili bandia (AI). Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2026, kampuni hiyo imewafikia zaidi ya wanafunzi 600 kupitia ushirikiano na shule nane za kimataifa na vituo viwili vya kujifunzia vya kijamii jijini Dar es Salaam. Aidha, ina watumishi wanane na imezalisha zaidi ya Shilingi milioni 15 katika mapato jambo linalotoa taswira ya elimu inayokwenda hatua moja zaidi—elimu inayompa kijana si cheti pekee, bali pia uwezo wa kutengeneza fursa. TIA pia imeendelea kukuza utamaduni wa ubunifu kupitia Shindano la Ubunifu linalowapa wanafunzi nafasi ya kubadilisha mawazo yao kuwa suluhisho na fursa za biashara. Mwaka 2025, jumla ya mawazo 376 yaliwasilishwa katika shindano hilo. Kati yake, washindi 57 walipatikana na mawazo 17 yalifikia hatua ya kuanzishwa kuwa biashara zinazofanya kazi. Katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA TIA imeendelea kuboresha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma. Taasisi imeanzisha mfumo wa kidijitali wa kukusanya na kusimamia taarifa za wanafunzi (SIMS), unaowawezesha wanafunzi kupata huduma mbalimbali kuanzia maombi ya kujiunga, udahili na usajili, malipo, matokeo, huduma za maktaba hadi kujifunza kwa njia ya mtandao. Maboresho hayo yanalenga kuongeza ufanisi, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuendana na mahitaji ya kizazi cha sasa kinachokua katika mazingira ya kidijitali. Uwekezaji wenye matokeo kwa Taifa Kwa ujumla, uwekezaji unaofanywa na Serikali katika TIA unaonesha namna fedha zinazowekezwa katika elimu zinavyoweza kubadilika na kuwa fursa kwa vijana na Taifa kwa ujumla. Kutoka kwenye majengo na miundombinu hadi kwenye taaluma, TEHAMA, utafiti, ubunifu na ujasiriamali, uwekezaji huo umeiwezesha TIA kupanua wigo wa elimu ya juu na kuongeza uwezo wa kuzalisha wahitimu wenye maarifa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya dunia ya sasa.

Na Jacqueline Mrisho MAELEZO. Hatimaye Tanzania imeshuhudia kutimia kwa maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ya kujenga bwawa katika eneo la Stiegler’s Gorge kwenye Mto Rufiji kwa ajili ya kuzalisha umeme wa uhakika na wa kutosha kwa maendeleo ya Taifa. Wazo hilo lililoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1976 liliendelea kuenziwa na viongozi waliomfuata, wakiwemo Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin William Mkapa na Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Licha ya kukabiliwa na changamoto na upinzani mbalimbali ndani na nje ya nchi, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ilichukua hatua ya kutafuta fedha, kutatua changamoto na kuanza utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati. Leo, Bwawa la Mwalimu Nyerere limekuwa sehemu muhimu ya jitihada za Tanzania kuhakikisha Taifa linakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wenye uwezo wa kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii. Mradi huo una uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, hatua inayoongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Taifa kuzalisha umeme na kusaidia kuondoa changamoto ya upungufu na mgao wa umeme uliokuwa ukiathiri uzalishaji viwandani, huduma za jamii, biashara na matumizi ya majumbani. Umeme huo umefungua nafasi kubwa kwa uwekezaji, viwanda, biashara, utalii, uzalishaji na ajira, huku ukitoa fursa ya kuongeza kipato cha wananchi na kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa. Akizindua mradi huo Agosti 22, 2026, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema kukamilika kwa mradi huo ni fundisho kwamba mafanikio ya miradi ya kimkakati yanahitaji uthubutu, uthabiti na ufuatiliaji wa karibu. Tunapofanya maamuzi yenye maslahi kwa Taifa, hatupaswi kukata tamaa kwa sababu njia ya kufanikisha ni ngumu bali tunapaswa kuwa na uthubutu na uthabiti wa kuyasimamia maono na maamuzi yetu ili kufikia malengo tuliyojiwekea na manufaa tunayoyatarajia, alisema Rais Samia. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhe. Felischem Mramba, amesema mahitaji ya umeme nchini yanaongezeka kwa kati ya asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka, hali inayoashiria pia ukuaji wa shughuli za kiuchumi. Amesema Bwawa la Mwalimu Nyerere limekuwa msingi muhimu wa kuondoa mgao wa umeme na kuwezesha Tanzania kuendelea na uwekezaji katika uchumi wa viwanda, kuvutia wawekezaji, kuimarisha utalii na kukuza shughuli nyingine za uzalishaji. Bwawa hili limetutoa kwenye mgawanyo wa umeme kama nchi, na linatuhakikishia sasa kwamba tunaweza kuendelea kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda, tunaweza kualika wawekezaji kutoka nje wakaja kuwekeza kwenye uchumi wetu, tunaweza kuboresha utalii na mambo mengine mbalimbali ambayo ndiyo hasa yanayokuza uchumi wetu, amesema. Kukamilika kwa bwawa hilo ni hatua moja katika kuhakikisha umeme unaowafikia wananchi wote. Serikali inaendelea kuimarisha Gridi ya Taifa, ikiwemo kukamilisha njia ya umeme ya kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 345, pamoja na upanuzi wa kituo cha kupokea na kupooza umeme cha Zuzu, Dodoma. Kupitia kituo hicho, umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere unasafirishwa kwenda Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kaskazini. Jitihada hizo zimepanua wigo wa upatikanaji wa umeme, ambapo hadi sasa vijiji vyote 12,318 na takribani asilimia 62.4 ya vitongoji Tanzania Bara vimefikiwa na huduma hiyo. Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha nchi nzima inapata umeme ifikapo mwaka 2030. Uwezo mkubwa wa uzalishaji umeifanya Tanzania kuwa na umeme wa ziada, unaoweza kutumika kwa mahitaji ya ndani na kuuzwa katika nchi jirani ili kuongeza mapato na upatikanaji wa fedha za kigeni. Tayari Tanzania imepokea maombi kutoka nchi mbalimbali. Zambia imeonesha hitaji la kati ya Megawati 500 na 600, Rwanda inahitaji Megawati 100, huku Kenya ikikubaliana na Tanzania kuhusu uwezekano wa kufanya mabadilishano ya umeme. Hii inaifanya Tanzania kuingia katika hatua mpya, ambapo umeme hauwi tu huduma muhimu kwa maendeleo ya ndani, bali pia bidhaa yenye uwezo wa kuzalisha mapato na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi jirani. Pamoja na Bwawa la Mwalimu Nyerere, Serikali inaendelea kuwekeza katika vyanzo vingine vya nishati, ikiwemo jua, upepo na nishati ya jotoardhi (thermal), ili kuongeza uwezo wa Taifa kuzalisha umeme kulingana na kasi ya ukuaji wa uchumi. Hatua hizi zinaifanya Tanzania kujenga msingi wa nishati unaoweza kuhimili mahitaji ya sasa na ya baadaye, huku ukifungua milango zaidi kwa viwanda, uwekezaji, biashara na ajira. Kukamilika kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa hatua mpya ya Tanzania yenye nishati ya kutosha, uchumi unaokua na fursa zinazoongezeka kwa wananchi.

        Na Baraka Messa – MAELEZO Utambulisho ni msingi muhimu katika maisha ya kila mwananchi, kwani humwezesha mtu kutambulika kisheria, kupata huduma za kijamii na kiuchumi, kushiriki katika shughuli za maendeleo na kutekeleza haki na wajibu wake kwa urahisi. Kutokana na umuhimu huo, Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Utambulisho Duniani, Septemba 16, 2026, huku nchini maadhimisho hayo yakianza Septemba Mosi kupitia shughuli mbalimbali zinazofanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika wilaya mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar. Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, anasema maadhimisho hayo yanafanyika wakati dunia ikiendelea kutafuta suluhisho la changamoto ya mabilioni ya watu ambao hawana utambulisho rasmi, hali inayowakosesha fursa ya kupata baadhi ya huduma muhimu. Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho hayo katika Kituo cha Urithi wa Ukombozi jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Msigwa amesema tathmini mbalimbali zinaonesha kuwa Bara la Afrika lina idadi kubwa ya watu wasio na utambulisho wa kisheria. Anasema hali hiyo imechochea juhudi za pamoja za mataifa ya Afrika na wadau mbalimbali kuhakikisha kila mtu anapata utambulisho rasmi unaomwezesha kutambulika na kupata haki pamoja na huduma muhimu za kijamii na kiuchumi. Katika safari hiyo, Msigwa amesema Tanzania imejijengea nafasi muhimu kutokana na hatua ilizochukua mapema kuanzisha mfumo wa usajili na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa, hatua ambayo imeendelea kuimarisha mifumo ya utambulisho nchini. Anasema mchakato wa usajili na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa ulianza mwaka 2012 kwa majaribio katika Mkoa wa Dar es Salaam, kabla ya kupanuliwa katika maeneo mengine nchini kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Msigwa anasema, NIDA imepewa majukumu mbalimbali ya msingi, yakiwemo kuwatambua na kuwasajili watu wanaoishi nchini wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, kutoa Vitambulisho vya Taifa kwa raia na wageni wakazi, pamoja na kutunza takwimu za usajili na utambuzi wa watu na kushirikishana taarifa hizo na wadau kwa mujibu wa sheria. Tanzania imepiga hatua kubwa katika usajili. Kufikia Julai 2026, jumla ya watu 27,455,882 wamesajiliwa, sawa na asilimia 87.2 ya watu wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, ambao ni 31,477,938 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, anasema Msigwa. Anasema katika kipindi hicho, jumla ya Vitambulisho vya Taifa 21,526,585 vilizalishwa, sawa na asilimia 92.2 ya namba za utambulisho 23,344,265 zilizotolewa, huku vitambulisho 20,935,351 vikiwa vimegawiwa kwa wananchi, sawa na asilimia 97.2 ya vitambulisho vilivyozalishwa. Msigwa anasema mfumo wa utambulisho umeleta manufaa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kusaidia taasisi zinazohusika na usalama kudhibiti uhalifu, kupunguza udanganyifu, kudhibiti utakatishaji fedha na kufuatilia shughuli mbalimbali zinazohitaji uthibitisho wa utambulisho wa mtu. Anasema pia matumizi ya Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) yamewezesha usajili wa laini za simu 92,735,799, hatua inayosaidia kupunguza udanganyifu na kuimarisha usalama katika mfumo wa mawasiliano, huku mfumo huo ukiwezesha wananchi, wakiwemo wazee, wanawake na vijana, kufungua akaunti na kupata huduma za kifedha na mikopo. Utambulisho pia umewezesha wananchi kutambuliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na kupata huduma za matibabu kwa urahisi, wanafunzi wa elimu ya juu kupata mikopo na kuiwasilisha kwa urahisi, pamoja na TASAF kuhakiki walengwa na kufanya malipo kwa ufanisi zaidi, anasema. Aidha, Msigwa amesema Serikali inaendelea na mpango wa kufanya maboresho katika mfumo wa Vitambulisho vya Taifa, hususan katika teknolojia ya uzalishaji na uchapishaji wa vitambulisho, baada ya kupokea maoni kutoka kwa wadau na kubaini umuhimu wa kuendana na teknolojia za kisasa. Anasema miongoni mwa maboresho yanayotarajiwa ni kuhamia kutoka teknolojia inayotumika sasa kwenda teknolojia inayotumia mionzi katika uchapishaji wa Vitambulisho vya Taifa, hatua inayolenga kuongeza ubora na usalama wa vitambulisho hivyo. Pamoja na hayo Msigwa, amesema Serikali inalenga kufanya Kitambulisho cha Taifa kuwa nyenzo pana zaidi ya utambulisho kwa kuunganisha taarifa muhimu za huduma anazopata mwananchi. Kadi ya Kitambulisho cha Taifa itabeba taarifa za utambulisho wa mtu pamoja na taarifa muhimu za huduma, zikiwemo bima ya afya na leseni ya udereva, anasema Msigwa. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uzalishaji Vitambulisho wa NIDA, Edson Guyai, amefafanua matumizi ya Kitambulisho cha Taifa cha NIDA na Kitambulisho cha Mkazi Zanzibar (ZAN ID), akisema NIDA ni taasisi ya Muungano hivyo Kitambulisho cha Taifa hutumika kumtambua mwananchi akiwa Tanzania Bara au Zanzibar. NIDA ni taasisi ya Muungano, Kwa hiyo, huduma zote za Muungano Kitambulisho cha Taifa cha NIDA hutumika kumtambua mwananchi akiwa Zanzibar au Tanzania Bara, Hata hivyo, kuna huduma ambazo ni mahsusi kwa Zanzibar, hivyo katika huduma hizo hutumika Kitambulisho cha Mkazi Zanzibar, amesema Guyai. Guyai anawataka wananchi ambao Vitambulisho vyao vya Taifa vimekamilika, wanaokadiriwa kufikia milioni 1.5, kwenda kuvichukua katika vituo husika ili waanze kuvitumia kupata huduma mbalimbali, Anasema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wananufaika kikamilifu na mfumo wa utambulisho wa taifa. Kwa ujumla, Mfumo huu, ambao umeanza kama njia ya kumtambua mtu, sasa unaendelea kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo, usalama, uchumi na utoaji wa huduma, huku Serikali ikiendelea kuboresha teknolojia ili kuhakikisha kila mwananchi anatambulika na anapata huduma kwa ufanisi.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na wazalishaji wa saruji nchini kutafuta suluhu ya haraka ya kurejesha bei ya saruji katika viwango vinavyomudu wananchi. Makamu wa Rais ametoa agizo hilo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya 19 ya Tuzo za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani, iliyofanyika katika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam. Amesema maono ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa muhimu kwa gharama nafuu, hivyo ni muhimu kuoanisha uzalishaji na upatikanaji wa malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa saruji ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama. Aidha, Makamu wa Rais ameitaka Serikali kufanya tathmini ya ukuaji wa sekta ya viwanda nchini ili kubaini iwapo viwanda vilivyopo vina uwezo wa kushindana katika masoko ya kikanda, Afrika na kimataifa. Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wafanyabiashara wanaojihusisha na uingizaji wa bidhaa bandia na biashara haramu zinazokwepa kodi na tozo, akieleza kuwa vitendo hivyo vinaathiri viwanda vya ndani, mapato ya Serikali na ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini. Makamu wa Rais amewataka wazalishaji kuongeza uchakataji wa malighafi ndani ya nchi na kuongeza thamani ya bidhaa, hatua itakayoongeza ajira, mapato na kuchochea ukuaji wa uchumi. Pia ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakiki takwimu za idadi ya viwanda vilivyopo nchini ili kuweka mikakati ya kuimarisha uwakilishi wa wazalishaji kupitia Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI). Amesema sekta ya viwanda ni mhimili muhimu wa maendeleo kwa kuwa inaongeza thamani ya malighafi, inazalisha ajira, inaongeza mapato ya Serikali na fedha za kigeni, huku ikichochea sayansi, teknolojia, ubunifu na uvumbuzi. Kwa kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi ikiwemo misitu na madini, ni muhimu kuendelea kukuza sekta ya viwanda na kujenga uhusiano madhubuti kati ya viwanda na sekta nyingine ili kuongeza ufanisi na kipato cha Watanzania. Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema Wizara inaendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa. Amesema Wizara imekamilisha Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 pamoja na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Mwaka 2003, Toleo la 2025, zinazolenga kwenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Hussein Suphian Ally, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kiuchumi ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), bandari, barabara na nishati, akisema miradi hiyo imepunguza gharama za usafirishaji na kurahisisha biashara. Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitunukiwa Tuzo ya Heshima kwa kutambua mchango wake katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na maendeleo ya sekta ya viwanda nchini. Hafla hiyo imewakutanisha wazalishaji wakubwa, wa kati na wadogo, wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa sekta ya viwanda na biashara, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ubora, ubunifu, uwekezaji, matumizi ya teknolojia na uzalishaji endelevu nchini.