Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Blogu

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Katika miji inayokua kwa kasi, biashara ndogo ndogo zimekuwa sehemu muhimu ya maisha ya wananchi. Kwa maelfu ya Watanzania, biashara hizo ni chanzo cha ajira, kipato na mahitaji ya kila siku ya familia. Hata hivyo, ukuaji wa shughuli hizo unahitaji usimamizi wenye mipango unaozingatia maslahi ya wafanyabiashara, wananchi na ustawi wa miji. Ni kwa kuzingatia umuhimu huo ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Wakuu wa Mikoa kusimamia kwa umakini suala la wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga, akieleza kuwa wameanza kurejea kwa kasi katika maeneo yaliyotengwa kwa wafanyabiashara wakubwa. Rais Samia ametoa kauli hiyo Septemba 2, 2026, katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa. Amesema suala la wafanyabiashara wadogo lilikuwa likisimamiwa vizuri, lakini kwa sasa kumekuwa na kulegalega katika utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao katika maeneo yaliyopangwa. Suala la wafanyabiashara wadogo wadogo, tulikuwa tunalisimamia vizuri, lakini kwa sasa tumepunguza usimamizi hasa katika Majiji ya Mwanza, Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Dodoma, amesema Rais Samia. Kwa Rais Samia, changamoto ya Machinga kurejea katika maeneo ya wafanyabiashara wakubwa haiwezi kutatuliwa kwa kutumia nguvu au kuwaondoa bila kuwa na mpango mbadala. Amesisitiza umuhimu wa viongozi kuweka mipango mizuri itakayowawezesha wafanyabiashara hao kuendelea na shughuli zao katika maeneo salama na yaliyopangwa. Si kwa kuwapiga fimbo au kuwapeleka Askari Mgambo kwenda kuwanyang’anya vitu vyao na kuwapiga mateke, tuwapangie mipango mizuri, watoke walipo na warudi kwenye masoko, ameagiza. Kauli hiyo inaweka msisitizo kwenye matumizi ya mipango badala ya nguvu, ili kutatua changamoto ya wafanyabiashara wadogo kwa njia inayolinda utu wao na wakati huo huo kuhakikisha miji inakuwa na mpangilio unaokubalika. Biashara za Machinga zina nafasi kubwa katika uchumi wa wananchi kwa kuwa zinawawezesha watu wengi kujiajiri na kupata kipato bila kutegemea ajira rasmi. Kwa baadhi ya wananchi, biashara hizi ni hatua ya kwanza ya kujenga mtaji, kukuza biashara na hatimaye kuingia katika shughuli kubwa zaidi za kiuchumi. Hivyo, usimamizi wa wafanyabiashara hao unahitaji kuangalia zaidi namna ya kuwawezesha kukua kuliko kuwaona kama tatizo linalopaswa kuondolewa katika maeneo ya mijini. Mipango mizuri ya upangaji wa maeneo ya biashara inaweza kuwasaidia Machinga kupata maeneo yenye wateja, mazingira salama na huduma muhimu, huku ikisaidia pia kupunguza msongamano na migongano kati ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa. Maelekezo ya Rais Samia kwa viongozi ya kuwarudisha wafanyabiashara wadogo katika masoko yanapaswa kutafsiriwa kama wito wa kuhakikisha maeneo hayo yana mazingira yanayoweza kuwawezesha kufanya biashara kwa tija. Soko lenye mpangilio mzuri, usalama, usafi na mazingira rafiki kwa biashara linaweza kuwa zaidi ya sehemu ya kuuza bidhaa; linaweza kuwa kichocheo cha maendeleo ya wafanyabiashara na wananchi wanaotegemea huduma zao. Kwa mtazamo huo, kuwaondoa Machinga katika maeneo yasiyofaa kunapaswa kuambatana na kuwaandalia maeneo mbadala yenye uwezo wa kuwasaidia kuendelea kujipatia kipato. Ujumbe wa Rais Samia pia unawakumbusha viongozi kuwa utekelezaji wa sheria na mipango ya miji unapaswa kwenda sambamba na kuheshimu utu wa wananchi. Wafanyabiashara wadogo wanapaswa kupewa maelekezo yanayoeleweka, kushirikishwa katika mipango inayowahusu na kupewa muda na mazingira yanayowawezesha kuhamia katika maeneo yaliyopangwa. Kwa kufanya hivyo, Serikali inaweza kufikia malengo mawili kwa wakati mmoja: kuweka miji katika mpangilio unaotakiwa na kulinda fursa za kiuchumi za wananchi. Maelekezo ya Rais Samia yanaibua umuhimu wa kutafuta uwiano kati ya maendeleo ya miji na mahitaji ya wananchi wanaotegemea biashara ndogo ndogo. Miji inahitaji kuwa na maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya biashara mbalimbali, huku wafanyabiashara nao wakihitaji mazingira yatakayowawezesha kufanya biashara bila kuvunja taratibu zilizowekwa. Hivyo, suluhisho la changamoto ya Machinga si kuwafukuza kutoka eneo moja kwenda jingine, bali ni kuwa na mpango endelevu wa upangaji, ugawaji wa maeneo na usimamizi wa biashara ndogo ndogo. Kwa kufanya hivyo, biashara ndogo zinaweza kuendelea kuwa chanzo muhimu cha ajira na kipato kwa wananchi, huku miji ikiendelea kuwa safi, salama na yenye mpangilio. Hatua hiyo pia itaimarisha uhusiano kati ya Serikali na wafanyabiashara wadogo kwa kujenga mazingira ambayo wananchi wanaona kuwa mipango ya Serikali inalenga kuwawezesha, badala ya kuwazuia kujitafutia maisha. Ujumbe wa Rais Samia ni kwamba Machinga wanahitaji kupangwa na kuwezeshwa, si kubughudhiwa Wanahitaji maeneo yanayofaa kwa biashara, viongozi wenye mipango na utekelezaji unaozingatia utu.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi aliowateua hivi karibuni, wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, kutanguliza maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha wanawasikiliza, wanatatua kero zao na kutoa huduma bora kwa ufanisi. Rais Samia ametoa wito huo Septemba 2, 2026, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni, Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, akisisitiza kuwa nafasi walizopewa si fursa ya kujinufaisha, bali ni dhamana ya kuwatumikia wananchi na kulinda maslahi ya Taifa. Amewakumbusha viongozi hao kuwa wao ni watumishi wa wananchi, hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo, uadilifu na uwajibikaji, huku wakitanguliza maslahi ya Taifa mbele ya maslahi binafsi. Rais Samia amewasisitiza viongozi hao kuwa utumishi wa umma ni kuwa tayari kuwatumikia wananchi waliokupa dhamana hiyo, kwa kuweka mbele uzalendo na maslahi mapana ya nchi. Amesema viongozi wanapaswa kuwa karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuhakikisha kero zinazoweza kutatuliwa katika ngazi za mikoa na wilaya zinapatiwa majibu na hatua stahiki kwa wakati. Amesema uongozi wa aina hiyo utasaidia kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali na kuhakikisha huduma za umma zinawafikia walengwa kwa wakati na kwa ufanisi. Aidha, amesisitiza kuwa wananchi hawahitaji viongozi wanaosubiri kero zifikishwe ofisini pekee bali wanahitaji viongozi wanaokwenda kwao, kusikiliza changamoto zao, kutafuta suluhisho na kusimamia utekelezaji ili matokeo yaonekane.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imefanikiwa kuokoa fedha za Serikali takribani Shilingi bilioni 121.99 ambazo zingetumika kwa matibabu nje ya nchi, baada ya kuwapatia wagonjwa 2,282 huduma za ubingwa na ubingwa bobezi katika mwaka wa fedha 2025/26.   Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, Taasisi hiyo ilihudumia jumla ya wagonjwa 211,359, wakiwemo wagonjwa 202,000 wa nje na 9,359 waliolazwa. Amesema kuimarishwa kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa, kumeiwezesha MOI kupunguza rufaa za wagonjwa wa mifupa kwa asilimia 98 na wagonjwa wa ubongo kwa asilimia 97. Huduma zilizoboreshwa ni pamoja na upasuaji wa ubongo kwa teknolojia za kisasa, upasuaji kupitia matundu, tiba ya maumivu, upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu, huduma za kiharusi, pamoja na upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo kupitia tundu la pua. Katika huduma za ubingwa bobezi, wagonjwa 2,282 walipatiwa matibabu yakiwemo upasuaji wa nyonga, upandikizaji wa goti bandia, upasuaji wa hydrocephalus na scoliosis, hatua iliyosaidia kupunguza utegemezi wa matibabu nje ya nchi na kuokoa fedha za Serikali. Aidha, amesema MOI imeendelea kuchangia ukuaji wa tiba utalii nchini, ambapo katika mwaka huo ilihudumia wagonjwa 270 kutoka Comoro, Msumbiji, Malawi, Zambia, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda, Burundi, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Balozi Dkt. Ulisubisya amesema uwepo wa wataalamu wenye uzoefu, vifaa tiba vya kisasa na mifumo bora ya utoaji huduma umeifanya MOI kuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa kutoka ndani na nje ya Tanzania. Katika kuimarisha ubora wa huduma, asilimia 87.5 ya wagonjwa waliridhishwa na huduma walizopata, huku kiwango cha kuridhika kwa watumishi kikifikia asilimia 82 na ushughulikiaji wa malalamiko kufikia asilimia 90. Aidha, katika kipindi hicho MOI ilifanya vipimo 83,847 vya radiolojia, ikiwemo MRI 11,533, CT Scan 6,796 na X-Ray 53,384, huku wagonjwa 71,819 wakipatiwa huduma za tiba kwa mazoezi (fiziotherapia). Taasisi hiyo pia imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia huduma mkoba, zilizowafikia wagonjwa 18,455, ambapo 4,310 walifanyiwa upasuaji. Mafanikio hayo yamekwenda sambamba na utekelezaji wa miradi ya kuboresha miundombinu, ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la OPD lenye thamani ya Shilingi bilioni 13.8, ukarabati wa MOI Annex, maboresho ya vyumba 25 vya kisasa vya kulaza wagonjwa, ukarabati wa ICU ya watoto pamoja na ujenzi wa tenki la Hewa Tiba ya Oksijeni lenye ujazo wa tani 10. Kuhusu mipango ya baadaye ya taasisi hiyo, Dkt. Ulisubisya amesema MOI itaendelea kuboresha huduma kwa viwango vya kimataifa, kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kuanzisha huduma mpya za kibingwa na ubingwa bobezi kwa kutumia teknolojia za kisasa. Amesema pia Taasisi hiyo inaendelea kujiandaa kutoa huduma za afya kwa wanamichezo na wadau wengine wakati wa michuano ya AFCON 2027.

Na. Baraka Messa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzania kuilinda na kuitunza miundombinu ya Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHP), akisema kuwa mradi huo ni mali ya Watanzania na urithi muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Rais Samia amesema hayo  Agosti 22, 2026, wilayani Rufiji mkoani Pwani, wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Uzalishaji wa Umeme cha Julius Nyerere chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115. Amesema kuwa Serikali imewekeza rasilimali kubwa katika utekelezaji wa mradi huo kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme na kuweka msingi wa maendeleo ya viwanda, uchumi na ustawi wa wananchi na kusisitiza kuwa jukumu la kulinda mradi huo si la Serikali pekee, bali ni la kila Mtanzania, kutokana na umuhimu wake katika maendeleo ya Taifa. Mradi huu ni wetu sote, Ni lazima tuulinde, tuutunze na tuhakikishe unaendelea kutoa manufaa kwa Watanzania wa leo na vizazi vijavyo,” amesema Rais Samia. Ameongeza kuwa Mradi wa JNHP ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya nishati nchini, hivyo akawataka wananchi kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika katika kulinda miundombinu ya mradi huo. Kituo cha Uzalishaji wa Umeme cha Julius Nyerere chenye uwezo wa megawati 2,115 kinatarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini na kuimarisha upatikanaji wa nishati kwa matumizi ya majumbani, viwandani na katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratus Ndejembi amebainisha kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Taifa. Aidha, uzinduzi  wa kituo hicho unafungua sura mpya katika safari ya Tanzania ya kuimarisha usalama wa nishati, huku Serikali ikiendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuwa washiriki wakuu katika kulinda na kunufaika na miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini.