Tanzania Yataja Mafanikio na Hatua za Kuimarisha Haki za Binadamu UN
Na Mwandishi Wetu – Geneva, Uswisi
Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza na kulinda utu na haki za binadamu kwa watu wote, huku ikiendelea kuweka upatikanaji wa haki na huduma muhimu kwa wananchi kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Serikali.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Ulega, amesema hayo Novemba 5, 2026, wakati akiwasilisha hotuba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika awamu ya nne ya Mapitio ya Kimataifa ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR), mbele ya Kikundi Kazi cha UPR katika kikao chake cha 53 kinachoendelea jijini Geneva, Uswisi, kuanzia Novemba 2 hadi 13, 2026.
Mhe. Ulega amesema Tanzania inajivunia kushiriki katika awamu hiyo ya mapitio, huku akieleza hatua zilizopigwa katika kuimarisha haki za kiraia na kisiasa, ushiriki wa kidemokrasia, uhuru wa msingi na upatikanaji wa haki.
Ameeleza kuwa, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, juhudi za kuimarisha haki za binadamu zimeongozwa na falsafa ya Misingi Minne ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Upya.
Tunatambua umuhimu wa kuendelea kufanya mageuzi, kuimarisha taasisi na kuhakikisha uwajibikaji katika maeneo yote huku tukiongozwa na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 na misingi ya kutomwacha mtu yeyote nyuma. Hivyo, tunakaribisha mapendekezo yenye kujenga pamoja na ushirikiano unaozingatia kuheshimiana. Tuko tayari kusikiliza, kubadilishana uzoefu na kushirikiana na nchi wanachama katika misingi ya mazungumzo yenye kujenga na kuheshimiana.
Aidha, amezitaka nchi washirika wa kimataifa kuheshimu mamlaka ya Tanzania na taratibu zake za kisheria, akisisitiza kuwa ushirikiano katika masuala ya haki za binadamu unapaswa kuzingatia mazungumzo yenye kujenga, kuheshimiana na wajibu wa pamoja wa kulinda na kuendeleza haki hizo.
Akieleza hatua zilizopigwa katika kutekeleza haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, Waziri Ulega amesema Tanzania imeendelea kuwekeza katika miundombinu na huduma muhimu zinazoboresha maisha ya wananchi na kupanua fursa za maendeleo.
Ametaja uwekezaji huo kuwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa ya SGR yenye urefu wa zaidi ya kilomita 700 na Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme.
Ameongeza kuwa vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vimefikiwa na huduma ya umeme, huku kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini kikifikia takribani asilimia 79.5. Vilevile, uwekezaji katika sekta mbalimbali za uzalishaji umewezesha kupatikana kwa fursa za ajira zaidi ya milioni 4.2.
Katika sekta ya elimu, amesema bajeti imeongezeka kutoka takribani shilingi trilioni 5.6 katika mwaka wa fedha 2022/2023 hadi shilingi trilioni 6.3 katika mwaka wa fedha 2025/2026. Ameeleza pia kuwa Serikali inaendelea kutoa elimu ya msingi bila ada na kuweka utaratibu unaowawezesha wanafunzi waliokatisha masomo kurejea shuleni, wakiwemo wasichana walioacha masomo kutokana na ujauzito.

Katika sekta ya afya, idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya Tanzania Bara imeongezeka kutoka 8,458 mwaka 2022 hadi zaidi ya 10,000 mwaka 2026. Huduma za kliniki kwa wajawazito zimefikia asilimia 98, huku kiwango cha wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya kikiongezeka kutoka asilimia 83 hadi asilimia 98.
Aidha, kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi kimepungua kutoka 197 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, huku vifo vya watoto wachanga vikishuka kutoka 25 hadi 19 kwa kila vizazi hai 1,000. Hatua hizo zinaonesha juhudi za Serikali katika kupanua upatikanaji wa huduma za afya, hususan kwa akina mama na watoto.
Kuhusu uwezeshaji wa wanawake na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, Waziri Ulega amesema Tanzania imepiga hatua katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na umiliki wa rasilimali. Uwakilishi wa wanawake katika Bunge ulifikia asilimia 39.3 mwaka 2025, huku uwakilishi wao katika Mahakama ukifikia asilimia 36.5. Aidha, uwiano wa wanawake wenye haki za umiliki wa ardhi uliongezeka kutoka asilimia 28.5 mwaka 2020 hadi asilimia 35 mwaka 2025.
Akizungumzia utekelezaji wa mapendekezo ya mapitio yaliyotangulia, amesema katika awamu ya tatu iliyofanyika mwaka 2021, Tanzania ilipokea jumla ya mapendekezo 252, ikakubali mapendekezo 187, yakiwemo 20 yaliyokubaliwa kwa sehemu, huku mapendekezo 65 yakikosa ridhaa ya Serikali.
Amesema mapendekezo yaliyokubaliwa yamekuwa mwongozo katika kutekeleza mageuzi mbalimbali katika kipindi chote kilichopita, hatua inayoonesha dhamira ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kuimarisha na kulinda haki za binadamu.