Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Serengeti Kuwa Mwenyeji wa Tuzo za Dunia za Utalii (World Travel Awards)

November 5, 2026

Na Mwandishi Wetu London, Uingereza

Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake katika ramani ya utalii duniani baada ya kutangazwa kuwa mwenyeji wa hafla ya utoaji wa Tuzo za Dunia za Utalii (World Travel Awards – WTA) kwa mwaka 2026, zitakazofanyika Desemba 12, 2026 katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Tangazo hilo limetolewa Novemba 5, 2026 na Mwanzilishi na Rais wa World Travel Awards, Bw. Graham Cooke, wakati wa hafla maalumu iliyofanyika katika kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya World Travel Market (WTM) jijini London, Uingereza.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Cooke amesema Tanzania imechaguliwa kutokana na upekee wake katika sekta ya utalii, akibainisha kuwa Serengeti ni moja ya majina makubwa yanayotambulika barani Afrika na duniani kutokana na utajiri wake wa wanyamapori na vivutio vya kipekee.

Ameongeza kuwa uwepo wa Mlima Kilimanjaro, ambao ni mlima mrefu zaidi barani Afrika, pamoja na uzuri wa vivutio vya asili na ukarimu wa Watanzania, ni miongoni mwa sababu zilizoifanya Tanzania kuwa chaguo sahihi la kuandaa tukio hilo la kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amemshukuru Bw. Cooke na taasisi ya World Travel Awards kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa hafla hiyo muhimu, akieleza kuwa nchi ipo tayari kuhakikisha wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani wanapata uzoefu wa kipekee wa utalii wa Tanzania.

Amesema Serengeti nayo ipo tayari kupokea wageni zaidi ya 500 wanaotarajiwa kuhudhuria hafla hiyo kutoka mataifa mbalimbali duniani, huku akisisitiza kuwa tukio hilo ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania, kuongeza muonekano
wake kimataifa na kuimarisha nafasi yake katika soko la utalii duniani.

Aidha, Dkt. Kijaji ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi na uongozi wake katika kuifungua Tanzania na kuimarisha diplomasia, akisema kazi kubwa inayofanyika chini ya uongozi wake imechangia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Tanzania na kuiweka katika nafasi nzuri zaidi katika jukwaa la kimataifa la utalii.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Dkt. Thereza Mugobi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *