Ufugaji wa samaki kwa kutumia teknolojia ya vizimba ndani ya Ziwa Tanganyika umeanza kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi mkoani Kigoma, kupitia juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya uvuvi na kuongeza uzalishaji wa samaki. Teknolojia hiyo inatoa fursa kwa wananchi kujishughulisha na ufugaji wa samaki kibiashara, kuongeza kipato, kujiajiri na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla. Kupitia ushirikiano wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Serikali imewezesha upatikanaji wa vizimba, vifaranga na chakula cha samaki vyenye thamani ya Shilingi milioni 602 kwa wanufaika wa mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi. Msaada huo umetolewa kwa mfumo wa mikopo isiyo na riba, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wajasiriamali kuwekeza katika ufugaji wa samaki kwa njia za kisasa. Katika utekelezaji wa mpango huo, Kigoma imekuwa miongoni mwa mikoa inayonufaika zaidi kutokana na uwepo wa Ziwa Tanganyika, ambalo lina mazingira na rasilimali muhimu kwa shughuli za ufugaji wa samaki. Jumla ya vizimba 29, pamoja na vifaranga na chakula cha samaki, vyenye thamani ya Sh milioni 602 vilitolewa kwa wanufaika wa mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi kwa mikopo isiyo na riba. Kati ya hivyo, Kigoma ilipangiwa vizimba 26, huku Rukwa na Katavi zikipata vizimba viwili kila mmoja. Aidha, Serikali imeendelea kutoa elimu na kujenga uwezo kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika, ambapo jumla ya wananchi 302 walikuwa wamepatiwa mafunzo kuhusu mbinu bora za ufugaji wa samaki kwa kutumia teknolojia ya vizimba. Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wafugaji katika usimamizi wa vizimba, utunzaji wa samaki na matumizi sahihi ya chakula ili kuongeza uzalishaji na tija.uj Katika kuhakikisha ufugaji huo unakuwa endelevu na unazingatia uhifadhi wa mazingira, Serikali kwa kushirikiana na taasisi ya The Nature Conservancy imeainisha maeneo matano yanayofaa kwa ufugaji wa samaki kwa vizimba ndani ya Ziwa Tanganyika. Maeneo hayo ni Katabe, Kalalangabo, Kirando, Kimbwela na Kigalye, huku hatua hiyo ikilenga kuhakikisha shughuli za ufugaji zinafanyika katika maeneo yanayokidhi vigezo vya kitaalamu na kisheria. Ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba unatarajiwa kuwa kichocheo cha shughuli nyingine za kiuchumi katika mkoa huo, ikiwemo biashara ya chakula cha samaki, usafirishaji, uuzaji wa samaki, huduma za vifaa vya uvuvi na uchakataji wa mazao ya baharini. Hali hiyo itatoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kushiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi na kuongeza ajira zisizo za moja kwa moja. Kwa ujumla, uwekezaji katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba unaonesha namna rasilimali za maji zinavyoweza kutumika kama nyenzo muhimu ya kuimarisha uchumi wa wananchi. Kupitia teknolojia hiyo, Ziwa Tanganyika linaendelea kuwa na nafasi kubwa katika kukuza uzalishaji wa samaki, kuongeza kipato, kutengeneza ajira na kufungua fursa mpya za uwekezaji kwa wananchi wa Kigoma na maeneo mengine nchini.