Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Ndejembi Asimamia Kilio cha Maji Kilwa

November 15, 2026

Na Baraka Messa – MAELEZO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameitaka Wizara ya Maji kuharakisha usanifu wa upanuzi wa Mradi wa Maji wa Kilwa ili wananchi wa Kata ya Mandawa, Hoteli Tatu na maeneo jirani nao wanufaike na huduma ya maji safi na salama.

Ndejembi ametoa agizo hilo novemba 15,2026 wakati wa kukagua utekelezaji wa mradi huo katika eneo la Mavuji, Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, akisisitiza kuwa uwekezaji unaofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unapaswa kuwafikia wananchi wote, wakiwemo wale ambao bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji.

Ni muhimu kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya maji unawanufaisha wananchi wote. Hivyo, usanifu wa upanuzi wa mradi huu uharakishwe ili wananchi wa Mandawa, Hoteli Tatu na maeneo jirani nao wapate huduma ya maji safi na salama.

Amesema ni muhimu hatua za upanuzi wa mradi huo kuchukuliwa kwa haraka ili maeneo ambayo hayajanufaika na huduma hiyo ya msingi yaendelee kuingizwa katika mfumo wa usambazaji wa maji, hatua itakayosaidia kuboresha afya na maisha ya wananchi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi akikagua mradi wa Maji wa Miji 28 wa chanzo cha Mto Mavuji, Wilaya ya Kilwa, akiwa ziarani mkoani Lindi.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema mamlaka ya maji imeelekezwa kuanza usanifu wa upanuzi wa mradi huo ili kubaini gharama zinazohitajika, huku Wizara ya Maji ikiahidi kutoa fedha kwa ajili ya kufanikisha hatua hiyo.

Mradi huo ni sehemu ya Mradi wa Maji wa Miji 28, wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 44.25 na umefikia asilimia 97.4 ya utekelezaji. Tayari umeanza kutoa huduma na unatarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 59,983 wa Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje, Mavuji na Mchakama.

Muonekano wa Mradi wa Maji wa Miji 28 wa chanzo cha Mto Mavuji, Wilaya ya Kilwa, uliokaguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa ziarani mkoani Lindi.

Kwa mujibu wa taarifa za mradi huo, unatumia chanzo cha Mto Mavuji na una uwezo wa kuzalisha lita milioni tano za maji kwa siku, kiasi kinacholenga kukidhi mahitaji ya wananchi katika maeneo yanayohudumiwa.

Aidha, mradi huo unahudumia pia Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, ambayo inahitaji lita milioni moja za maji kwa siku wakati wa uendeshaji wake, hivyo kuwa na mchango muhimu katika kuimarisha huduma za kijamii na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *