Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Serikali Kuanzisha Mfuko wa Nishati Safi Kuwezesha Vijana na Wanawake Kiuchumi

November 15, 2026

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO

Serikali imepanga kuanzisha Mfuko Maalumu wa Nishati Safi ya Kupikia ili kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi kwa kuwapatia mitaji ya kuzalisha majiko banifu na nishati mbadala katika halmashauri zote nchini.

Akizungumza Novemba 15, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu manufaa ya ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), uliofanyika Antalya, Uturuki, Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Homera, amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Amesema kupitia mfuko huo, vikundi vya vijana na wanawake katika kila halmashauri vitawezeshwa kupata mitaji kwa ajili ya kutengeneza majiko banifu na kuzalisha mkaa mbadala, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za ajira na ujasiriamali pamoja na kuinua kipato cha wananchi.

Ameeleza kuwa mpango huo pia utachangia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida, hivyo kupunguza shinikizo la ukataji wa miti, kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, ameitaka sekta binafsi kutumia fursa zilizopo katika sekta ya nishati safi ya kupikia kwa kuwekeza katika uzalishaji na usambazaji wa teknolojia za nishati hiyo, akibainisha kuwa uwekezaji huo una uwezo mkubwa wa kuchochea ukuaji wa uchumi na kutengeneza ajira kwa Watanzania.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali inaendelea kupanua matumizi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi za umma, ambapo hadi sasa taasisi 2,745 zimeanza kutumia nishati hiyo. Kati ya hizo, magereza ni 129 huku taasisi nyingine za Serikali zikiwa 2,616.

Ameongeza kuwa wadau wa maendeleo wameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha sekta hiyo, ikiwemo kutekeleza mpango wa kuwafikia wananchi milioni moja kwa kuwapatia majiko ya umeme yatakayolipiwa kupitia mfumo wa LUKU.

Amesisitiza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, huku ikiendeleza fursa za kiuchumi kwa vijana na wanawake na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *