Rais Samia Aipandisha Hadhi Idara ya Habari – MAELEZO
Na Baraka Messa – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali inaendelea na mwelekeo wa kuimarisha Idara ya Habari – MAELEZO na kuinua hadhi yake ili iweze kufanya kazi kama Idara inayojitegemea, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika uratibu, usimamizi na usambazaji wa taarifa za Serikali kwa wananchi.
Rais Samia amesema hayo Novemba 27, 2026, mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali katika hafla iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam, ambapo pia amemkaribisha Mkurugenzi mpya wa Idara ya Habari – MAELEZO ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Ayub Rioba Chacha, kuongoza idara hiyo kufuatia uteuzi wake wa hivi karibuni.
Rais Samia amesema Idara ya Habari – MAELEZO inapaswa kuwa taasisi yenye uwezo wa kusimamia na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, hususan kuhakikisha taarifa za shughuli na utekelezaji wa majukumu katika sekta mbalimbali za Serikali zinakusanywa, kuratibiwa na kufikishwa kwa wananchi kwa wakati.
Amesisitiza kuwa anatarajia kuona Idara hiyo ikifanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa kuhakikisha kila sekta ya Serikali inawasilisha taarifa za shughuli na mafanikio yake ili ziweze kuratibiwa na kutangazwa kwa umma.
Nimekupa uongozi wa Habari MAELEZO, wewe sasa ndiyo utakuwa na dhamana ya kuhakikisha sekta zote zinaleta waliyoyafanya yazungumzwe.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa MAELEZO kuwa na kasi ya kujibu hoja, changamoto na malalamiko ya wananchi kuhusu utendaji wa Serikali, akieleza kuwa mawasiliano yanapaswa kufanyika kwa haraka ili wananchi wapate ufafanuzi kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kutatua changamoto zao.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Dkt. Ayub Rioba Chacha ana uzoefu na uwezo mzuri wa kuwasilisha ujumbe, akibainisha kuwa ana namna ya kuzungumza kwa utulivu huku akihakikisha ujumbe unawafikia walengwa.