Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Megawati 2,000 za Ziada ni Nguvu Mpya ya Tanzania Kiuchumi

September 15, 2026

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO

Upatikanaji wa umeme wa uhakika ni msingi wa kufungua fursa mpya za maendeleo kwa Taifa linalolenga kuongeza uzalishaji, kukuza viwanda na kujenga uchumi shindani.

Tanzania inapofikisha ziada ya Megawati 2,000 za umeme, hatua hiyo inaashiria uwezo mkubwa wa nchi katika kuzalisha nishati ambayo inapaswa kugeuzwa kuwa kichocheo cha uzalishaji, uwekezaji, viwanda, kuzalisha ajira na kuongeza kipato kwa wananchi. Uwepo wa megawati 2000 za ziada ni habari njema kwa Watanzania kuichangamkia fursa hiyo na kutumia nguvu ya umeme kujenga uchumi wenye tija na kuongeza thamani ya rasilimali za Taifa.

Akiongea hivi karibuni kwenye mkutano wa hadhara ulifanyika Bariadi mkoani Simiyu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Tanzania kwa sasa ina ziada ya MW 2,000 za umeme, hatua inayoiweka nchi katika nafasi nzuri ya uzalishaji wa nishati ikilinganishwa na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, SADC na maeneo mengine ya Afrika.

Ziada hiyo ya umeme inapaswa kutazamwa kama fursa ya uzalishaji. Wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji wanapaswa kutumia mazingira hayo kuanzisha na kupanua viwanda, hasa viwanda vidogo na vya kati vinavyoweza kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo yao. Kilimo, mifugo, uvuvi na madini vinaweza kuongezewa thamani kupitia uchakataji unaotumia umeme, na hivyo kuongeza kipato na ajira.

Mkulima, kwa mfano, hapaswi kuishia kuuza zao ghafi ikiwa anaweza kulichakata na kupata bidhaa yenye thamani zaidi. Alizeti inaweza kuzalisha mafuta, mazao ya nafaka yanaweza kuchakatwa, maziwa yanaweza kuongezwa thamani na mazao mengine yanaweza kuhifadhiwa au kusindikwa kwa kutumia teknolojia. Hapo ndipo umeme unapogeuka kuwa mtaji wa uzalishaji.

Kwa wafanyabiashara na vijana, ongezeko la upatikanaji wa umeme linaweza kufungua milango ya shughuli mpya. Kuanzia karakana na mashine za uzalishaji hadi teknolojia, huduma za kidijitali na biashara zinazohitaji nishati ya uhakika. Fursa hiyo inahitaji ubunifu na hatua, si kusubiri.

Serikali inaendelea kuweka mazingira ya kuifanya nguvu hiyo iwafikie wananchi. Kupitia Mradi wa Gridi Imara, unaotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Bariadi, uwezo wa gridi unaendelea kuimarishwa ili kuongeza uhakika wa usambazaji wa umeme.

Aidha, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 302 kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini, hatua iliyowezesha mkoa wa Simiyu kufikisha huduma hiyo katika vijiji vyote 478.

Hii ni nafasi ya wananchi wa mijini na vijijini kuangalia umeme kwa jicho jipya. Si huduma ya kutumia majumbani pekee, bali ni rasilimali ya kuzalisha utajiri. Kila eneo lenye umeme linaweza kuwa eneo la uzalishaji ikiwa wananchi watatumia fursa hiyo kuanzisha biashara, viwanda na shughuli zinazoongeza thamani.

Tanzania pia ina rasilimali nyingi zinazoweza kuunganishwa na nguvu hii ya nishati. Ardhi, kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini vinaweza kutoa malighafi kwa viwanda vya ndani. Changamoto sasa ni kuongeza ubunifu, uwekezaji na uzalishaji ili nishati inayopatikana itumike kikamilifu katika kuongeza thamani ya rasilimali hizo.

Kwa vijana, wajasiriamali na wawekezaji, ujumbe ni mmoja tu kwao: Fursa hii isitazamwe kama takwimu ya Serikali, bali kama nafasi ya kufanya biashara na kuzalisha. Badala ya kusubiri ajira, mazingira haya yanatoa nafasi ya kuanzisha shughuli zinazoweza kutengeneza ajira kwa wengine.

Ziada ya Megawati 2,000 pia ina maana kwamba Tanzania ina nafasi ya kujiandaa kwa mahitaji makubwa zaidi ya nishati yatakayotokana na ukuaji wa viwanda, miji na shughuli za kiuchumi. Hivyo, hatua inayofuata ni kuhakikisha uwezo huo unabadilishwa kuwa uzalishaji halisi na thamani kwa wananchi.

Nguvu ya umeme inakuwa nguvu ya uchumi pale inapogeuzwa kuwa uzalishaji. Na uzalishaji unaanza pale wananchi wanapochukua hatua. Megawati 2,000 za ziada ni mwaliko kwa Watanzania kuchangamkia fursa, kuanzisha viwanda, kuongeza thamani ya rasilimali, kukuza biashara na kujenga ajira. Tanzania ina umeme wa kuzalisha zaidi; sasa ni wakati wa wananchi kuzalisha zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *