Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Mhe. Ndejembi Aagiza Dampo la Pugu Liboreshwe, Kero za Wananchi Zitatuliwe

September 18, 2026

Na Mwandishi wetu

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Halmashauri zake kuhakikisha hali ya dampo la Pugu inaboreshwa, huku akielekeza maeneo ya makazi yanayozunguka dampo hilo kupuliziwa dawa ili kuwalinda wananchi dhidi ya wadudu na kupunguza hatari ya magonjwa, hususan katika kipindi cha mvua.

Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo Septemba 18, 2026, alipofanya ziara katika Dampo la Pugu linalotumika kukusanya taka za Mkoa wa Dar es Salaam ili kujionea hali halisi ya eneo hilo na kusikiliza kero za wananchi wanaoishi maeneo ya jirani.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Wananchi wa eneo la Pugu, mara baada ya kutembelea na kukagua Dampo la kukusanyia taka la mkoa wa Dar es Salaam, lililopo Pugu Kinyamwezi wakati wa ziara maalum aliyoifanya leo tarehe 18 Septemba 2026.

Aidha, ameelekeza kuandaliwa kwa mpango kazi wa pamoja utakaoainisha hatua za haraka na za muda mrefu za kukabiliana na changamoto za uendeshaji wa dampo la Pugu pamoja na kero zinazowakabili wananchi wanaoishi katika maeneo yanayolizunguka, ikiwemo kutopuliziwa dawa za kuua wadudu.

Akiwa katika dampo hilo, Mhe. Ndejembi ameonesha kutoridhishwa na kutofautiana kwa takwimu kuhusu kiasi cha taka zinazokusanywa na kupelekwa katika Dampo la Pugu kila siku kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Kutokana na hali hiyo, amezitaka mamlaka zote zinazohusika kukaa pamoja, kuhakiki na kuweka takwimu sahihi zitakazokuwa msingi wa kupanga na kutekeleza hatua madhubuti za kuboresha usimamizi wa taka jijini Dar es Salaam.

Hatuwezi kutatua changamoto za eneo hili bila kuwa na taarifa na takwimu sahihi. Hawa wananchi mnaowaona wamechoka na stori; wanataka kuona kazi.

Amesema wananchi wanatarajia kuona matokeo ya moja kwa moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali, hivyo amewataka viongozi na taasisi husika kuharakisha utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha kero za wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Ndejembi ametoa siku saba kwa mawaziri wanaohusika na TAMISEMI, Maliasili na Utalii pamoja na Ardhi kufika katika maeneo husika na kutatua mgogoro wa muda mrefu unaohusu mipaka ya kiutawala na mpaka wa Msitu wa Kazimzumbwi, ambao umekuwa ukiwaathiri wananchi wa Pugu na maeneo ya jirani.

Changamoto hiyo imesababisha baadhi ya wananchi kutokuwa na uhakika kuhusu maeneo yao ya makazi kutokana na kutofahamika kwa mipaka ya kiutawala pamoja na mpaka wa Msitu wa Kazimzumbwi.

Waheshimiwa Mawaziri, nataka mfike wenyewe kwenye eneo hili kutambua GN za mikoa na mipaka ya Msitu wa Kazimzumbwi, kwani hii imekuwa kero ya muda mrefu. Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka tutatue kero za wananchi; kwa hiyo naelekeza hili mkalifanyie kazi ndani ya siku saba liwe limeisha.

Awali, wananchi wa maeneo ya Mstafa, Viwege na Kinyamwezi walitumia fursa ya ziara hiyo kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, zikiwemo athari zinazotokana na uwepo wa dampo, kutopuliziwa dawa za kuua wadudu katika maeneo yao, ukosefu wa maji kwa muda mrefu pamoja na migogoro ya ardhi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ameahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Makamu wa Rais.

Miongoni mwa hatua zitakazotekelezwa ni kuboresha usimamizi wa dampo la Pugu, kuweka utaratibu wa kila halmashauri kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya uendeshaji wa dampo hilo, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa vifaa na kuboresha miundombinu muhimu ili shughuli za dampo ziendeshwe kwa kuzingatia matakwa ya kimazingira na kiafya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *