Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Rais Samia Ataja Vipaumbele Vitatu Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi

November 11, 2026

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametaja vipaumbele vitatu ambavyo Tanzania inavipa uzito katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku akisisitiza umuhimu wa upatikanaji wa fedha za kutosha, mpito wa haki wa matumizi ya nishati na kuimarisha maendeleo jumuishi yanayostahimili athari za tabianchi.

Rais Dkt. Samia ametaja vipaumbele hivyo Novemba 11, 2026, alipokuwa akihutubia Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) unaofanyika jijini Antalya, nchini Uturuki, ambapo amesema Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea, inaendelea kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi zikiwemo ukame wa muda mrefu, mabadiliko yasiyotabirika ya mvua na kupanda kwa kina cha bahari.

Rais Samia amesema nchi zinazoendelea zinahitaji fedha za kutosha, zinazotabirika na zinazopatikana kwa urahisi, hususan ruzuku na mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, sambamba na uhamishaji wa teknolojia na kujengewa uwezo.

Tanzania ina fursa nyingi za kuchangia katika kupunguza hewa ukaa kupitia sekta za usafiri, usimamizi wa taka, nishati jadidifu ikiwemo umeme wa maji, jotoardhi na upepo, pamoja na misitu inayokadiriwa kufunika takribani hekta milioni 48.1. Hivyo, nasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mifumo ya uwazi ya biashara ya hewa ukaa na utekelezaji wa Ibara ya Sita ya Mkataba wa Paris ili kuhakikisha manufaa yanagawanywa kwa haki na mazingira yanalindwa.

Akitaja kipaumbele cha pili, Mhe. Rais Samia amesema kuwa Tanzania inasisitiza umuhimu wa mpito wa haki wa matumizi ya nishati barani Afrika, unaozingatia upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na endelevu kwa wananchi wote huku akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Nishati kwa lengo la kupanua upatikanaji wa umeme nchini, hususan maeneo ya vijijini, huku akitoa wito wa kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi, mikopo yenye masharti nafuu na uhamishaji wa teknolojia.

Ameendelea kwa kusema kipaumbele cha tatu kuwa Tanzania inaendelea kuimarisha maendeleo jumuishi na yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi kupitia Dira ya Maendeleo ya miaka 25 ijayo, inayoweka mkazo katika ubunifu, ujenzi wa viwanda na mageuzi ya kiuchumi endelevu.

Aidha, ameeleza kuwa Dira hiyo inatambua umuhimu wa kuwaandaa vijana kwa kuwapatia ujuzi wa kijani na fursa za ajira zinazozingatia utunzaji wa mazingira, pamoja na kuendeleza kilimo endelevu, nishati jadidifu na viwanda vinavyohifadhi mazingira.

Tanzania ina dhamira thabiti ya kutekeleza malengo ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi na Mkataba wa Paris, ni matarajio yangu kuwa COP31 itaimarisha ushirikiano wa kimataifa katika upatikanaji wa fedha, uhamishaji wa teknolojia na kujenga uwezo ili kuwezesha utekelezaji wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *