Rais Samia Atoa Wito COP31 Kubadilisha Ahadi kuwa Vitendo
Na Sidi Mgumia-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema
Tanzania inaendelea kupanua upatikanaji wa umeme kupitia Mpango wa Taifa wa Nishati (National Energy Compact), huku ikiimarisha maendeleo jumuishi na yanayohimili mabadiliko ya tabianchi kupitia Dira ya Maendeleo ya miaka 25 ijayo.
Mhe. Rais Samia ameyasema hayo Novemba 11, 2026, nchini Uturuki , wakati akihutubia ufunguzi wa Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaofanyika Antalya, ambapo amesema Tanzania inaendelea kukabiliwa na ukame wa muda mrefu, mabadiliko yasiyotabirika ya misimu ya mvua na kupanda kwa kina cha bahari, hali inayokadiriwa kuigharimu nchi kati ya asilimia mbili na tatu ya Pato la Taifa (GDP) kila mwaka.
Tanzania inaipa kipaumbele upatikanaji wa fedha za tabianchi za kutosha, zinazotabirika na zinazopatikana kwa urahisi, pamoja na kuimarisha fursa za masoko ya kaboni katika sekta za usafirishaji, usimamizi wa taka, nishati jadidifu na misitu inayokadiriwa kufunika hekta milioni 48.1.
Amesisitiza kuwa juhudi hizo zitaenda sambamba na kuwaandaa vijana kupata ujuzi na ajira katika nishati jadidifu, kilimo endelevu na viwanda rafiki kwa mazingira, pia ametoa wito kwa nchi kushirikiana ili kuhakikisha COP31 inabadilisha ahadi kuwa vitendo na matokeo yanayopimika.
Afafanua kuwa umuhimu wa mifumo ya biashara ya kaboni chini ya Kifungu cha Sita cha Mkataba wa Paris kuwa ya uwazi na kuhakikisha manufaa yanawafikia jamii zinazotekeleza miradi hiyo.
Kwa upande wake, Rais wa COP31, Mhe. Murat Kurum, amezitaka nchi kuingiza malengo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika mipango ya uwekezaji, bajeti za kitaifa na miradi ya maendeleo ili kuhakikisha ahadi zinazotolewa zinatafsiriwa katika matokeo halisi kwa wananchi.
Amesema mabadiliko ya tabianchi sasa yanahusisha masuala ya nishati, viwanda, kilimo, maendeleo na usalama, hivyo yanahitaji mipango inayozingatia mahitaji ya sasa na vizazi vijavyo.
Ametolea mfano historia ya Istanbul katika karne ya 16, ambapo Sultan Suleiman alimwelekeza mbunifu Mimar Sinan kutafuta vyanzo vya maji na kujenga mifumo ya kuyasafirisha hadi jijini, akisema hatua hiyo ilihakikisha upatikanaji wa maji kwa wakazi kwa karne nyingi. Amesema mfano huo unaonesha umuhimu wa viongozi kuwekeza katika suluhisho za muda mrefu badala ya kusubiri changamoto zijitokeze.
Uturuki inalenga kufikia uchumi usiozalisha hewa chafuzi ifikapo mwaka 2053, sambamba na kuendelea kuunga mkono juhudi za kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzi joto 1.5.
Ameeleza kuwa uwekezaji katika matumizi bora ya nishati unaimarisha usalama wa nishati, usimamizi wa maji unaimarisha usalama wa chakula, huku teknolojia safi zikichochea maendeleo ya viwanda na kutengeneza ajira.
Aidha, amesema Uturuki imeandaa mpango wa Climate Implementation Bridge unaolenga kuunganisha mipango ya kitaifa ya tabianchi na uwekezaji, ufadhili, teknolojia na utaalamu ili kuharakisha utekelezaji wa ahadi.
Ameongeza kuwa kupitia mpango wa 35 by 35 Global Electrification Pledge, nchi hiyo inalenga kuongeza mchango wa umeme katika matumizi ya mwisho ya nishati hadi asilimia 35 ifikapo mwaka 2035, sambamba na kuendeleza mpango wa Zero Waste unaohamasisha matumizi endelevu ya rasilimali.