Makamu Wa Rais Awaonya Viongozi Songea, Aagiza TAKUKURU Kuchunguza Mradi wa Soko la Bilioni 3
Na Mwandishi Wetu – Songea, Ruvuma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka viongozi na watendaji wa Serikali wanaosimamia miradi ya maendeleo kuwajibika ipasavyo na kuchukua hatua dhidi ya wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba.
Ametoa agizo hilo kufuatia kuchelewa kwa ujenzi wa Soko la Manzese A na B katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, licha ya mkandarasi wa mradi huo kulipwa Shilingi bilioni tatu kama malipo ya awali.
Mradi huo ulioanza mwaka 2025 kwa muda wa utekelezaji wa miezi 18, ulitarajiwa kukamilika Septemba 2026, lakini haujakamilika kwa wakati kutokana na changamoto za usimamizi na upungufu wa vifaa vya ujenzi hali iliyosababisha mkandarasi kuongezewa muda wa utekelezaji hadi Machi 2027.

Akizungumza na wananchi wa Songea wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma, Makamu wa Rais amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Wakili Bashir Muhoja, kueleza sababu za kuendelea kumuongezea muda mkandarasi huyo licha ya kutoridhisha kwa kasi ya utekelezaji wa mradi.
Hebu tubadilike! Tuwajibike katika matumizi ya fedha za umma. Kikao cha ngazi ya juu kinakusaidia nini?
alihoji Makamu wa Rais, akisisitiza kuwa vikao vya mara kwa mara havipaswi kutumika kama mbadala wa hatua madhubuti za kuwawajibisha Wakandarasi wanaokiuka masharti ya mikataba.
Aidha, amemtaka Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuchukua hatua stahiki dhidi ya mapungufu yaliyojitokeza katika usimamizi wa mradi huo, ili kuhakikisha watendaji wanawajibika kwa majukumu waliyopewa.
Katika hatua nyingine, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza kampuni iliyokabidhiwa kazi hiyo, ikiwemo matumizi ya fedha za malipo ya awali, ili kubaini sababu za kushindwa kutekeleza mradi kwa kasi inayotakiwa.
Amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia uzembe katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, hasa pale unapochangia kuchelewesha huduma kwa wananchi na kusababisha fedha za umma kutotumika kwa tija iliyokusudiwa.
Makamu wa Rais anaendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Ruvuma, ambapo anatarajiwa kutembelea mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.