Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Ndejembi Ataka 10% ya Mapato ya Madini Kuelekezwa kwenye Utafiti

November 19, 2026

Na Scolastica Sambi – MAELEZO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya madini nchini kwa kuanzisha na kuendeleza viwanda vya kuchakata rasilimali hizo ili kuchochea ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa Taifa.

Akizungumza Novemba 19, 2026, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Saba wa Tanzania wa Madini na Uwekezaji wa mwaka 2026 uliofanyika jijini Dar es Salaam, wenye kaulimbiu isemayo “Madini Yaliyoongezwa Thamani, Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi,” Mhe. Ndejembi amesema kuwa Tanzania inapaswa kuhakikisha inapata manufaa makubwa kutokana na utajiri wa madini ilionao badala ya kutegemea mauzo ya madini ghafi.

Amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wanaotaka kuanzisha viwanda vya kuchakata madini nchini kupitia sera, sheria, kanuni na miongozo, huku akielekeza Wizara ya Madini kuhakikisha asilimia 10 ya mapato yatokanayo na sekta hiyo yanaelekezwa kwenye utafiti wa kina ili kubaini maeneo mapya yenye rasilimali za madini na kutoa taarifa za uhakika kwa wawekezaji.

Serikali inatambua umuhimu wa wawekezaji katika kuendeleza sekta ya madini. Hivyo, hatuna budi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuvutia wawekezaji zaidi na kuifanya sekta hii iendelee kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Aidha, amewataka vijana na wanawake kutumia fursa zilizopo katika mnyororo mzima wa thamani wa madini kuanzia utafiti, uchimbaji, uchakataji hadi biashara, akisisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo ili washiriki kikamilifu katika shughuli hizo.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema sekta ya madini imeendelea kuwa miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa Taifa, ikichangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa, huku mauzo ya madini nje ya nchi yakifikia dola za Marekani bilioni 5.4, sawa na zaidi ya shilingi trilioni 13.

Mhe. Mavunde amesema Serikali inaendelea kuimarisha uwekezaji katika uchakataji wa madini nchini, ambapo tayari kuna viwanda nane vya kusafisha dhahabu kwa kiwango cha ubora wa asilimia 99.99, pamoja na viwanda 16 vinavyojengwa kwa ajili ya kuchakata madini mbalimbali yakiwemo nikeli na shaba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *