Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Blogu

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Sekta ya Kilimo kwa miaka mingi imeendelea kuwa mhimili wa uchumi wa Tanzania na inayotoa uhakika wa usalama wa chakula, kutoa ajira kwa mamilioni ya wananchi na kuchechemua biashara, viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji. Hivyo, kumuwezesha mkulima kuongeza tija katika kilimo na kuimarisha kipato si jukumu la sekta moja pekee, bali ni uwekezaji wa moja kwa moja katika uchumi na mustakabali wa Taifa. Katika miaka ya hivi karibuni, uwekezaji katika sekta ya kilimo umeongezeka. Mathalani Bajeti ya Wizara ya Kilimo imepanda kutoka Shilingi bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi Shilingi trilioni 1.19 mwaka 2025/2026. Ongezeko hilo linaonesha uzito wa sekta ya kilimo katika ajenda ya maendeleo na juhudi za kujenga mazingira yatakayomwezesha mkulima kuongeza uzalishaji. Miongoni mwa hatua zinazomgusa mkulima moja kwa moja ni mfumo wa ruzuku za pembejeo, hususan mbolea na mbegu bora. Lengo ni kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija shambani. Taarifa zinaonyesha kuwa matumizi ya mbolea yaliongezeka kutoka tani 360,000 kabla ya mfumo wa ruzuku hadi tani 840,000 katika msimu uliofuata, huku lengo likiwa kufikisha matumizi hadi tani milioni moja. Lakini kuongeza uzalishaji kunahitaji pia uhakika wa maji. Kutegemea mvua pekee kunaendelea kuwa changamoto katika uzalishaji wa kilimo, hivyo uwekezaji katika umwagiliaji ni hatua muhimu ya kumuwezesha mkulima kuzalisha kwa uhakika zaidi. Kufikia mwaka 2024/2025, Serikali ilikuwa ikitekeleza miradi 780 ya umwagiliaji yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 543,000, huku kukamilika kwa miradi hiyo kukitarajiwa kuongeza eneo la umwagiliaji hadi zaidi ya hekta milioni 1.27. Pamoja na miundombinu hiyo, ushiriki wa wakulima katika usimamizi wa umwagiliaji nao umeongezeka. Idadi ya Vyama vya Umwagiliaji vilivyosajiliwa imepanda kutoka 19 mwaka 2020/2021 hadi 912 mwaka 2024/2025. Hii inaashiria nafasi inayoongezeka ya wakulima katika kusimamia rasilimali muhimu kwa uzalishaji wao. Kilimo pia kinafungua ukurasa mpya kwa vijana. Kupitia programu kama Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), vijana wanahamasishwa kukiona kilimo kama biashara na fursa ya uwekezaji. Mtazamo huu ni muhimu kwa kizazi kinachoweza kutumia teknolojia, ubunifu na maarifa ya kisasa kubadilisha kilimo kutoka shughuli ya kutegemea nguvu kazi pekee na kuwa biashara yenye tija. Hata hivyo, kumuwezesha mkulima hakumaanishi kumuwezesha kuzalisha pekee. Mkulima anahitaji kuwezeshwa kuzalisha, kuhifadhi, kusindika na kuuza kwa thamani inayostahili. Bila soko la uhakika na uwezo wa kuongeza thamani, ongezeko la uzalishaji linaweza lisitafsiriwe moja kwa moja kuwa ongezeko la kipato. Hapa ndipo nafasi ya viwanda inakuwa muhimu. Mazao yanayotoka mashambani yanapaswa kuwa malighafi ya viwanda vya ndani. Alizeti inaweza kuzalisha mafuta, nafaka zikachakatwa kuwa bidhaa mbalimbali, maziwa yakaongezwa thamani na mazao mengine yakahifadhiwa na kusindikwa. Kwa kufanya hivyo, thamani inayotokana na kilimo hubaki zaidi ndani ya nchi, huku ikifungua nafasi za ajira na biashara. Kwa mtazamo huo, Agenda 10/30 inaleta umuhimu wa kuongeza tija, thamani ya mazao, mauzo ya nje, ushiriki wa vijana na upatikanaji wa malighafi kwa viwanda. Kilimo kinapounganishwa na viwanda na masoko, mkulima haonekani tena kama mzalishaji wa malighafi pekee, bali anakuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani unaozalisha utajiri. Hata hivyo, kipimo cha mwisho cha mafanikio ya uwezeshaji kinapaswa kuwa maisha ya mkulima. Bajeti inaweza kuongezeka na miradi inaweza kujengwa, lakini mafanikio halisi yataonekana pale mkulima atakapoweza kuzalisha kwa gharama nafuu, kupata mavuno bora, kuhifadhi mazao, kupata soko na kulipwa kwa thamani inayolingana na jasho lake. Tanzania ina ardhi, maji, nguvu kazi, masoko na malighafi nyingi zinazoweza kuifanya kilimo kuwa injini kubwa zaidi ya uchumi. Kinachohitajika ni kuendelea kujenga mazingira yatakayomwezesha mkulima kutumia fursa hizo kikamilifu na kuwahamasisha vijana, wafanyabiashara na wawekezaji kuingia katika kilimo kwa mtazamo wa biashara. Tanzania yenye mkulima mwenye uwezo wa kiuchumi ni Tanzania yenye msingi imara wa chakula, viwanda, ajira na uchumi shirikishi. Kumuwezesha mkulima si kumsaidia mkulima pekee ni kuijenga Tanzania yenye uwezo wa pato la Taifa lenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja na wastani wa pato la mtu mmoja lenye thamani ya dola za Marekani 7000 kwa mwaka.

Sekta ya Madini inapozidi kuwa muhimu katika uchumi wa dunia, ushindani wa kimataifa haupimwi tena kwa wingi wa rasilimali pekee, bali pia kwa namna zinavyosimamiwa, uwekezaji unaovutwa na manufaa yake kwa wananchi. Mabadiliko haya yanaifanya Sekta ya Madini ya Tanzania kuzidi kujijengea nafasi katika mjadala wa kimataifa, kupitia maboresho ya sekta, ukuaji wa uwekezaji na ushirikiano wa kikanda na kimataifa. Kwa mujibu wa Tathmini ya Taasisi ya Fraser ya Canada ya mwaka 2025, Tanzania imeendelea kuimarika katika Sekta ya Madini kwa kushika nafasi ya nne barani Afrika na ya 34 duniani katika Kiashiria cha Kuvutia Uwekezaji (Investment Attractiveness Index). Aidha, Tanzania imeorodheshwa nafasi ya 15 duniani katika kipengele cha upatikanaji wa rasilimali madini, ikiwa na alama 75, jambo linalothibitisha utajiri mkubwa wa rasilimali za madini zilizopo nchini. Hata hivyo, nafasi hizi hazielezi tu uwepo wa madini mengi nchini. Zinadhihirisha pia kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji, usimamizi wa sekta, uwazi wa sera na ongezeko la imani ya wawekezaji kwa Tanzania. Kwa maneno mengine, Tanzania haitajwi katika tathmini hizi kwa sababu ya utajiri wa madini pekee, bali kwa jinsi inavyoendelea kujenga mazingira yanayowezesha rasilimali hizo kuchangia maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi. Mwelekeo huo unaonekana pia katika upande wa uwekezaji. Kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 2025, Sekta ya Madini imeendelea kuongoza kwa kuvutia Uwekezaji wa Mtaji wa Nje, ambapo mtaji uliongezeka kutoka dola bilioni 8.64 mwaka 2022 hadi dola bilioni 9.15 mwaka 2023 na kufikia dola bilioni 9.79 mwaka 2024. Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, anasema kuwa mafanikio hayo yamechochewa na mageuzi yanayoendelea chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na usimamizi wa sekta ya madini. Ongezeko hili ni matunda ya uhamasishaji wa uwekezaji, mazingira wezeshi kwa wawekezaji, upanuzi wa miradi iliyopo, uwekezaji wa faida zinazozalishwa ndani ya sekta na uunganishaji wa mitaji. Katika miaka ya hivi karibuni, Sekta ya Madini Tanzania imeendelea kuvutia kampuni mbalimbali za ndani na nje ya nchi ambazo zimeingia katika ushirikiano na Serikali katika maeneo ya utafutaji, uchimbaji na uongezaji thamani wa madini. Mwelekeo huu unaonesha kuwa ukuaji wa sekta si wa bahati mbaya, bali ni matokeo ya sera zilizo wazi, mifumo iliyoboreshwa na imani inayoongezeka kwa mazingira ya uwekezaji nchini. Mbali na kuvutia uwekezaji, Tanzania pia imekuwa ni sehemu ya rejea katika mijadala ya maendeleo ya sekta ya madini barani Afrika. Nchi mbalimbali zikiwemo Zambia, Uganda, Kenya, Burkina Faso, Sudani ya Kusini, Malawi, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tayari zimefika nchini kujifunza uzoefu wa Tanzania katika maeneo ya usimamizi wa sekta, ushirikishwaji wa wananchi, uendeshaji wa masoko ya madini na namna ya kuongeza mchango wa Sekta katika uchumi wa taifa. Hali hiyo inaonesha kuwa Tanzania si mnufaika wa mageuzi ya sekta ya madini pekee, bali pia imeanza kuwa chanzo cha uzoefu na maarifa kwa nchi nyingine zinazotafuta namna bora ya kuendeleza rasilimali zao za madini kwa manufaa ya wananchi. Kupitia hotuba yake ya bajeti aliyoisoma bungeni, Waziri Mavunde anaeleza kuwa, mwelekeo wa siku zijazo utaendelea kujikita katika kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa madini, kuimarisha matumizi ya teknolojia katika uchimbaji na uchenjuaji, kuongeza shughuli za uongezaji thamani wa madini pamoja na kuhakikisha sekta inachangia zaidi katika ajira, mapato ya Serikali na ukuaji wa uchumi wa taifa. Fauka ya hayo, Tanzania inaendelea kutajwa katika tathmini mbalimbali za kimataifa si kwa sababu ya utajiri wa madini pekee, bali kutokana na mchanganyiko wa rasilimali, sera zinazoendelea kuimarishwa, ongezeko la uwekezaji, ushiriki wa wananchi na usimamizi unaojenga imani kwa wadau wa sekta. Huu ndio msingi unaoifanya Tanzania kuendelea kujijengea nafasi muhimu zaidi katika ramani ya madini duniani na kuifanya sekta ya madini kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa nchi.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Mwaka 2027, macho ya Afrika na dunia yataelekezwa Afrika Mashariki wakati Tanzania, Kenya na Uganda zitakapokuwa wenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). Kwa Tanzania, tukio hili ni zaidi ya dakika 90 za mchezo uwanjani; ni jukwaa kubwa la biashara, utalii, uwekezaji na kuitangaza nchi kwa mamilioni ya watu duniani. Kuanzia Dar es Salaam, Arusha hadi Zanzibar, ujio wa mashabiki, watalii na wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani ni wazi kwamba utaongeza mahitaji ya malazi, usafiri, chakula, burudani, bidhaa na huduma nyingine, na hapo ndipo fursa kwa Watanzania zinapojitokeza, na ukubwa wa manufaa ya fursa hizo utategemea namna wafanyabiashara na watoa huduma watakavyojiandaa mapema. AFCON 2027 inatoa nafasi ya Tanzania kutumia tukio la michezo kutengeneza shughuli za kiuchumi zinazoweza kuendelea hata baada ya mashindano kumalizika. Hoteli zinaweza kupanua huduma, sekta ya utalii inaweza kuongeza bidhaa na vifurushi vipya, huku wafanyabiashara wadogo na wakubwa wakitengeneza bidhaa na huduma zinazolenga mahitaji ya wageni. Kupitia Podcast ya Idara ya Habari-MAELEZO, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, anasisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kuanza maandalizi mapema ili fursa zitakazotokana na AFCON 2027 ziwafikie wazawa na kuchochea shughuli za kiuchumi. Msigwa anaeleza kuwa uzoefu wa nchi nyingine zilizowahi kuwa wenyeji wa AFCON unaonyesha ukubwa wa fursa zinazoweza kujitokeza. Anatoa mfano wa Morocco, iliyokuwa mwenyeji wa AFCON iliyofanyika Desemba 2025 hadi Januari 2026, ambapo zaidi ya wageni milioni 1.6 walifika nchini kutoka maeneo mbalimbali. Takwimu hiyo inaonyesha kwa nini maandalizi hayawezi kusubiri hadi mashabiki waanze kuwasili. Fursa inaanza kabla ya mpira kuanza. Mfanyabiashara anayejipanga leo ana nafasi ya kuwa tayari wakati mahitaji yatakapoongezeka. Kwa wafanyabiashara wa hoteli, utalii, usafiri na chakula, AFCON 2027 inaweza kuwa soko jipya lenye mahitaji makubwa. Msigwa anawataka watoa huduma kutumia muda uliopo kuboresha huduma zao na kujiandaa kukidhi mahitaji ya wageni. Kama wewe unafanya biashara ya utalii, jiandae kuwasafirisha wageni kuwapeleka maeneo mbalimbali. Kama wewe ni mfanyabiashara wa hoteli, jiandae kushawishi wageni wafikie kwenye hoteli yako, na kama wewe ni mfanyabiashara wa chakula, jiandae kuandaa chakula kizuri ili wageni wakija wajisikie kuweka kambi na kuja kula kwako. Ujumbe wa Msigwa unaweka jukumu kubwa kwa sekta binafsi: kutazama AFCON si kama tukio la kutazama mpira wa miguu pekee, bali kama soko la kutengenezwa na kutumiwa katika kukuza uchumi w mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Mbali na biashara za moja kwa moja wakati wa mashindano, AFCON 2027 inaweza kuwa kichocheo cha uwekezaji katika maeneo yenye mahitaji ya muda mrefu. Makazi, hoteli, usafirishaji, kilimo, teknolojia na huduma mbalimbali ni miongoni mwa maeneo yanayoweza kuhitaji uwekezaji zaidi. Msigwa anawataka Watanzania na sekta binafsi kuanza kuwasiliana na wadau ndani na nje ya nchi ili kuvutia uwekezaji na kutumia tukio hilo kama mlango wa kuonyesha fursa zilizopo Tanzania. Rais ametuletea tukio kubwa, sisi tulitumie kufanya uwekezaji mkubwa, mfano kwenye makazi. Kwenye kilimo tukaribishe wadau wazuri wenye teknolojia na mitambo ya kisasa kuja kuwekeza. Hii ina maana kwamba faida ya AFCON haipaswi kuishia katika mapato yatakayopatikana wakati wa mashindano. Tanzania inaweza kutumia wageni watakaofika kama daraja la kufungua masoko mapya, mitandao ya biashara na uwekezaji wa muda mrefu. AFCON 2027 pia ni fursa ya Tanzania kujitangaza kupitia michezo. Wageni watakapofika nchini watapata nafasi ya kuona zaidi ya viwanja vya soka. Wataona utamaduni, vivutio vya utalii, bidhaa na mazingira ya biashara na uwekezaji. Kwa mtazamo huo, mashindano yanaweza kuwa jukwaa la kuitambulisha Tanzania kama eneo la utalii, biashara na uwekezaji katika Afrika Mashariki, SADC na bara zima la Afrika. Wakati fursa hizo zikitarajiwa, maandalizi ya miundombinu ya michezo yanaendelea. Kwa mujibu wa Msigwa, viwanja vitakavyotumika katika mashindano pamoja na viwanja vya mazoezi vimekamilika kwa kiwango kikubwa. Tanzania pia inaendelea na maandalizi ya kuongeza hamasa kwa wananchi kushiriki katika mashindano hayo na kuunga mkono Taifa Stars, huku mikakati ya hamasa ikitarajiwa kulenga Dar es Salaam, Zanzibar na Arusha. Hatimaye, thamani ya AFCON 2027 kwa Tanzania haitapimwa kwa idadi ya mechi zitakazochezwa pekee, bali pia kwa fursa zitakazobaki baada ya mashindano.Tukio hilo linaweza kuwa kichocheo cha biashara mpya, uwekezaji, ajira, utalii na masoko mapya ikiwa maandalizi yatafanyika kwa wakati. Kwa Watanzania, ujumbe ni mmoja: AFCON 2027 isiwe mashindano ya kutazama mpira tu uwanjani au kupitia Televisheni; iwe fursa ya kufanya biashara, kuwekeza, kuzalisha na kujenga. Mpira utakapigwa uwanjani, fursa zitakuwa mitaani, kwenye hoteli, mashamba, viwanda, usafiri na biashara mbalimbali.

Na Mwandishi wetu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Halmashauri zake kuhakikisha hali ya dampo la Pugu inaboreshwa, huku akielekeza maeneo ya makazi yanayozunguka dampo hilo kupuliziwa dawa ili kuwalinda wananchi dhidi ya wadudu na kupunguza hatari ya magonjwa, hususan katika kipindi cha mvua. Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo Septemba 18, 2026, alipofanya ziara katika Dampo la Pugu linalotumika kukusanya taka za Mkoa wa Dar es Salaam ili kujionea hali halisi ya eneo hilo na kusikiliza kero za wananchi wanaoishi maeneo ya jirani. Aidha, ameelekeza kuandaliwa kwa mpango kazi wa pamoja utakaoainisha hatua za haraka na za muda mrefu za kukabiliana na changamoto za uendeshaji wa dampo la Pugu pamoja na kero zinazowakabili wananchi wanaoishi katika maeneo yanayolizunguka, ikiwemo kutopuliziwa dawa za kuua wadudu. Akiwa katika dampo hilo, Mhe. Ndejembi ameonesha kutoridhishwa na kutofautiana kwa takwimu kuhusu kiasi cha taka zinazokusanywa na kupelekwa katika Dampo la Pugu kila siku kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam. Kutokana na hali hiyo, amezitaka mamlaka zote zinazohusika kukaa pamoja, kuhakiki na kuweka takwimu sahihi zitakazokuwa msingi wa kupanga na kutekeleza hatua madhubuti za kuboresha usimamizi wa taka jijini Dar es Salaam. Hatuwezi kutatua changamoto za eneo hili bila kuwa na taarifa na takwimu sahihi. Hawa wananchi mnaowaona wamechoka na stori; wanataka kuona kazi. Amesema wananchi wanatarajia kuona matokeo ya moja kwa moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali, hivyo amewataka viongozi na taasisi husika kuharakisha utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha kero za wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu. Katika hatua nyingine, Mhe. Ndejembi ametoa siku saba kwa mawaziri wanaohusika na TAMISEMI, Maliasili na Utalii pamoja na Ardhi kufika katika maeneo husika na kutatua mgogoro wa muda mrefu unaohusu mipaka ya kiutawala na mpaka wa Msitu wa Kazimzumbwi, ambao umekuwa ukiwaathiri wananchi wa Pugu na maeneo ya jirani. Changamoto hiyo imesababisha baadhi ya wananchi kutokuwa na uhakika kuhusu maeneo yao ya makazi kutokana na kutofahamika kwa mipaka ya kiutawala pamoja na mpaka wa Msitu wa Kazimzumbwi. Waheshimiwa Mawaziri, nataka mfike wenyewe kwenye eneo hili kutambua GN za mikoa na mipaka ya Msitu wa Kazimzumbwi, kwani hii imekuwa kero ya muda mrefu. Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka tutatue kero za wananchi; kwa hiyo naelekeza hili mkalifanyie kazi ndani ya siku saba liwe limeisha. Awali, wananchi wa maeneo ya Mstafa, Viwege na Kinyamwezi walitumia fursa ya ziara hiyo kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, zikiwemo athari zinazotokana na uwepo wa dampo, kutopuliziwa dawa za kuua wadudu katika maeneo yao, ukosefu wa maji kwa muda mrefu pamoja na migogoro ya ardhi. Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ameahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Makamu wa Rais. Miongoni mwa hatua zitakazotekelezwa ni kuboresha usimamizi wa dampo la Pugu, kuweka utaratibu wa kila halmashauri kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya uendeshaji wa dampo hilo, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa vifaa na kuboresha miundombinu muhimu ili shughuli za dampo ziendeshwe kwa kuzingatia matakwa ya kimazingira na kiafya.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Upatikanaji wa umeme wa uhakika ni msingi wa kufungua fursa mpya za maendeleo kwa Taifa linalolenga kuongeza uzalishaji, kukuza viwanda na kujenga uchumi shindani. Tanzania inapofikisha ziada ya Megawati 2,000 za umeme, hatua hiyo inaashiria uwezo mkubwa wa nchi katika kuzalisha nishati ambayo inapaswa kugeuzwa kuwa kichocheo cha uzalishaji, uwekezaji, viwanda, kuzalisha ajira na kuongeza kipato kwa wananchi. Uwepo wa megawati 2000 za ziada ni habari njema kwa Watanzania kuichangamkia fursa hiyo na kutumia nguvu ya umeme kujenga uchumi wenye tija na kuongeza thamani ya rasilimali za Taifa. Akiongea hivi karibuni kwenye mkutano wa hadhara ulifanyika Bariadi mkoani Simiyu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Tanzania kwa sasa ina ziada ya MW 2,000 za umeme, hatua inayoiweka nchi katika nafasi nzuri ya uzalishaji wa nishati ikilinganishwa na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, SADC na maeneo mengine ya Afrika. Ziada hiyo ya umeme inapaswa kutazamwa kama fursa ya uzalishaji. Wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji wanapaswa kutumia mazingira hayo kuanzisha na kupanua viwanda, hasa viwanda vidogo na vya kati vinavyoweza kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo yao. Kilimo, mifugo, uvuvi na madini vinaweza kuongezewa thamani kupitia uchakataji unaotumia umeme, na hivyo kuongeza kipato na ajira. Mkulima, kwa mfano, hapaswi kuishia kuuza zao ghafi ikiwa anaweza kulichakata na kupata bidhaa yenye thamani zaidi. Alizeti inaweza kuzalisha mafuta, mazao ya nafaka yanaweza kuchakatwa, maziwa yanaweza kuongezwa thamani na mazao mengine yanaweza kuhifadhiwa au kusindikwa kwa kutumia teknolojia. Hapo ndipo umeme unapogeuka kuwa mtaji wa uzalishaji. Kwa wafanyabiashara na vijana, ongezeko la upatikanaji wa umeme linaweza kufungua milango ya shughuli mpya. Kuanzia karakana na mashine za uzalishaji hadi teknolojia, huduma za kidijitali na biashara zinazohitaji nishati ya uhakika. Fursa hiyo inahitaji ubunifu na hatua, si kusubiri. Serikali inaendelea kuweka mazingira ya kuifanya nguvu hiyo iwafikie wananchi. Kupitia Mradi wa Gridi Imara, unaotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Bariadi, uwezo wa gridi unaendelea kuimarishwa ili kuongeza uhakika wa usambazaji wa umeme. Aidha, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 302 kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini, hatua iliyowezesha mkoa wa Simiyu kufikisha huduma hiyo katika vijiji vyote 478. Hii ni nafasi ya wananchi wa mijini na vijijini kuangalia umeme kwa jicho jipya. Si huduma ya kutumia majumbani pekee, bali ni rasilimali ya kuzalisha utajiri. Kila eneo lenye umeme linaweza kuwa eneo la uzalishaji ikiwa wananchi watatumia fursa hiyo kuanzisha biashara, viwanda na shughuli zinazoongeza thamani. Tanzania pia ina rasilimali nyingi zinazoweza kuunganishwa na nguvu hii ya nishati. Ardhi, kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini vinaweza kutoa malighafi kwa viwanda vya ndani. Changamoto sasa ni kuongeza ubunifu, uwekezaji na uzalishaji ili nishati inayopatikana itumike kikamilifu katika kuongeza thamani ya rasilimali hizo. Kwa vijana, wajasiriamali na wawekezaji, ujumbe ni mmoja tu kwao: Fursa hii isitazamwe kama takwimu ya Serikali, bali kama nafasi ya kufanya biashara na kuzalisha. Badala ya kusubiri ajira, mazingira haya yanatoa nafasi ya kuanzisha shughuli zinazoweza kutengeneza ajira kwa wengine. Ziada ya Megawati 2,000 pia ina maana kwamba Tanzania ina nafasi ya kujiandaa kwa mahitaji makubwa zaidi ya nishati yatakayotokana na ukuaji wa viwanda, miji na shughuli za kiuchumi. Hivyo, hatua inayofuata ni kuhakikisha uwezo huo unabadilishwa kuwa uzalishaji halisi na thamani kwa wananchi. Nguvu ya umeme inakuwa nguvu ya uchumi pale inapogeuzwa kuwa uzalishaji. Na uzalishaji unaanza pale wananchi wanapochukua hatua. Megawati 2,000 za ziada ni mwaliko kwa Watanzania kuchangamkia fursa, kuanzisha viwanda, kuongeza thamani ya rasilimali, kukuza biashara na kujenga ajira. Tanzania ina umeme wa kuzalisha zaidi; sasa ni wakati wa wananchi kuzalisha zaidi.

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeendelea kuandika historia mpya katika sekta ya utalii duniani baada ya kujinyakulia jumla ya tuzo 54 katika World Travel Awards 2026, huku ikiibuka kinara wa vivutio vya utalii barani Afrika kwa mara ya nne. Mafanikio hayo ni uthibitisho wa nafasi inayozidi kuimarika ya Tanzania katika ramani ya utalii duniani na matokeo ya juhudi za pamoja za Serikali, sekta binafsi, jamii na wadau mbalimbali. World Travel Awards ni miongoni mwa majukwaa yanayotambulika kimataifa kwa kutambua ubora na ushindani katika sekta ya safari na utalii. Ushindi wa Tanzania katika tuzo hizo za mwaka 2026 umeongeza heshima ya nchi katika soko la utalii la Afrika na dunia, huku ukiendelea kujenga chapa ya Tanzania kama miongoni mwa maeneo bora ya utalii duniani. Hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika Agosti 28, 2026, Bwejuu, Zanzibar, iliifanya Tanzania kung’ara katika medani ya kimataifa baada ya kushinda tuzo katika maeneo mbalimbali yanayobeba sura na hadhi ya utalii wa nchi. Miongoni mwa tuzo kubwa zilizotwaa na Tanzania ni Eneo Bora la Utalii Afrika 2026, ushindi unaoendelea kuthibitisha uwezo wa nchi katika kutoa uzoefu wa kipekee wa utalii. Zanzibar nayo imeendelea kung’ara kwa kushinda tuzo ya Eneo Bora la Fukwe Afrika 2026, huku Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ikitwaa tuzo ya Bodi Bora ya Utalii Afrika 2026. Ushindi huo hauishii katika fukwe na mandhari ya kuvutia. Tanzania imeendelea kuthibitisha kuwa utajiri wake wa utalii unagusa maeneo mbalimbali, hususan uhifadhi wa wanyamapori na mazingira. Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeendelea kuonesha upekee wake baada ya kushinda tuzo mbili muhimu za Hifadhi Bora Afrika 2026 na Hifadhi Bora ya Big Five Afrika 2026. Mafanikio hayo yanaendelea kuimarisha hadhi ya Serengeti kama moja ya maeneo maarufu ya utalii barani Afrika na duniani. Kwa upande mwingine, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha imetwaa tuzo ya Hifadhi Bora ya Utalii wa Kiutamaduni Afrika 2026, huku Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ikishinda tuzo ya Hifadhi Bora ya Mandhari Afrika 2026. Hifadhi ya Taifa ya Tarangire nayo imeibuka mshindi wa tuzo ya Hifadhi Bora ya Paradiso ya Tembo Afrika 2026. Mafanikio hayo yanaonesha wazi kuwa Tanzania si nchi ya hifadhi na wanyamapori pekee, bali ina hazina pana ya vivutio vinavyoweza kuwavutia watalii kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Katika sekta ya usafiri wa anga, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) umeibuka mshindi wa tuzo ya Uwanja Bora wa Ndege Afrika 2026, hatua inayoongeza ushindani na hadhi ya Tanzania katika kurahisisha safari na kuwapa wageni huduma bora wanapoingia na kutoka nchini. Mafanikio haya si ya taasisi moja wala kundi moja. Ni matokeo ya ushirikiano wa Serikali, taasisi za utalii na uhifadhi, sekta binafsi, jamii zinazozunguka maeneo ya utalii na wadau wengine wanaoshiriki katika kulinda rasilimali, kuboresha huduma na kujenga uzoefu bora kwa wageni wanaotembelea Tanzania. Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amempongeza na kumshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wenye dira na dhamira ya kuitangaza Tanzania kimataifa na kuweka utalii miongoni mwa sekta muhimu katika kukuza uchumi wa nchi. Mafanikio haya yanatambua mchango wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Ngorongoro, pamoja na taasisi nyingine za uhifadhi na utalii zinazoendelea kulinda, kuendeleza na kutangaza rasilimali za kipekee za utalii za Tanzania. Kwa hakika, nyuma ya kila tuzo kuna kazi ya Watanzania wengi. Wapo waendesha safari za kitalii, kampuni za safari, hoteli na kambi, mashirika ya ndege, waongoza watalii, askari wa wanyamapori, wahifadhi, wawekezaji, vyama vya utalii, jamii zinazozunguka maeneo ya utalii, vyombo vya habari na maelfu ya Watanzania wanaoshiriki kila siku kuhakikisha wageni wanaotembelea Tanzania wanapata uzoefu wa kipekee. Akizungumzia mafanikio hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Masuala ya Utalii, Bw. Nkoba Mabula, amesema Tanzania inajivunia hatua kubwa iliyofikiwa katika sekta hiyo, ikiwemo kujinyakulia tuzo 54 na kutajwa kuwa kinara wa vivutio vya utalii barani Afrika kwa mara ya nne. Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya dira na juhudi endelevu za Serikali pamoja na ushirikiano mkubwa wa wadau katika kulinda, kuendeleza na kuitangaza rasilimali na vivutio vya Tanzania. Kwa mtazamo mpana, ushindi huo ni zaidi ya medali na tuzo. Ni fursa ya kuitangaza Tanzania, kuongeza idadi ya watalii, kukuza ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa Watanzania. Ni pia ujumbe kwa dunia kwamba Tanzania ina kila sababu ya kuwa miongoni mwa chaguo la kwanza kwa mtu anayetamani kuona wanyamapori wa aina yake, fukwe za kuvutia, mandhari ya kipekee, utamaduni na ukarimu wa watu wake. Hatua iliyofikiwa inapaswa kuwa chachu ya kuongeza juhudi za kutunza rasilimali za nchi, kuboresha huduma, kuimarisha miundombinu na kuendelea kuitangaza Tanzania kwa nguvu zaidi katika masoko ya ndani, Afrika na kimataifa. Kwa Watanzania, tuzo hizi ni fahari ya Taifa na ushahidi kwamba tukilinda tulichonacho, tukiboresha huduma na kushirikiana, Tanzania inaweza si tu kushindana, bali pia kushinda katika soko la utalii duniani. Ushindi huu ni mwanzo wa hatua nyingine muhimu—ya kuhakikisha jina la Tanzania linaendelea kung’ara, fursa za utalii zinaongezeka na matunda ya sekta hiyo yanazidi kuwafikia Watanzania wengi zaidi.