Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Blogu

Na. Timothy Mwakyenda – MAELEZO Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amesema hali ya amani na usalama katika Jiji la Dar es Salaam ni shwari, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere. Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho hayo leo Julai 7, 2026, Chalamila aliwapongeza wakazi wa Dar es Salaam kwa mwitikio mkubwa wa kushiriki maonesho hayo, akisema ushiriki huo unaonesha wananchi wanatumia vyema fursa ya kujifunza, kufanya biashara na kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na washiriki. Alisema Serikali inaendelea kuhakikisha mazingira ya amani na utulivu yanatawala ili wananchi waweze kushiriki shughuli zao bila hofu, huku akiwataka kupuuza taarifa za upotoshaji zinazolenga kuwakatisha tamaa kushiriki maonesho hayo. Pokeeni salamu za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anawapongeza kwa kazi nzuri mnazozifanya na sisi tunaendelea kuhamasisha Watanzania kutumia fursa hii muhimu ya kuona teknolojia mpya, kununua bidhaa kwa bei nafuu na kujifunza ubunifu mbalimbali unaooneshwa na washiriki kutoka ndani na nje ya nchi,” alisema Chalamila. Alibainisha kuwa maonesho ya mwaka huu yanayoadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake yamewakutanisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 25, jambo linaloendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara, uwekezaji na ubunifu katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP. Jumanne Muliro alisema hali ya usalama katika jiji hilo inaendelea kuwa tulivu, huku akieleza kuwa tathmini ya maeneo mbalimbali, ikiwemo Kibamba, Kimara, Ubungo, Manzese, Tegeta, Bunju na Kigamboni, inaonesha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku kwa amani. Aliwahakikishia wananchi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama unaendelea kuimarika katika kipindi chote cha maonesho hayo, na kuwataka waendelee kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa za viashiria vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama. Muliro alisisitiza kuwa amani na utulivu ni msingi wa maendeleo ya taifa, akiwahimiza Watanzania kuendelea kuwa mabalozi wa amani kwa kushiriki shughuli za kijamii na kiuchumi kwa utulivu na uzalendo.

Na Mwandishi Wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), kwa kushirikiana na Balozi za Tanzania duniani, kuimarisha ufundishaji wa lugha ya Kiswahili na kuanzisha vituo vya utamaduni wa Kiswahili katika mataifa mbalimbali, ikiwemo Ufaransa. Maelekezo hayo yamewasilishwa leo, Julai 7, 2026, na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati wa kufunga Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani (MASKIDU 2026) yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), jijini Paris, Ufaransa. Kwa mujibu wa maelekezo ya Rais Samia, vituo hivyo vitakuwa kitovu cha kufundisha na kueneza lugha ya Kiswahili, kutangaza utamaduni wa Kitanzania na Afrika kwa ujumla, pamoja na kuimarisha diplomasia ya utamaduni. Vilevile, vitafungua fursa mpya za biashara, uwekezaji, utalii na ushirikiano wa kimataifa kupitia matumizi ya Kiswahili. Aidha, vituo hivyo vinatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuwawezesha wananchi wa mataifa mbalimbali kujifunza historia, urithi, mila, desturi na ustaarabu wa Afrika kupitia lugha ya Kiswahili, ambayo inaendelea kupata hadhi na kutambuliwa katika majukwaa ya kimataifa. Katika hatua nyingine, Rais Samia amewahimiza Watanzania wanaoishi ughaibuni (Diaspora) kuhakikisha wanawarithisha watoto wao lugha ya Kiswahili ili kudumisha utambulisho wa Taifa, kuimarisha mshikamano wa kizazi hadi kizazi na kuhifadhi urithi wa kitamaduni wa Tanzania. Amesisitiza kuwa kadri Kiswahili kinavyoendelea kupanua wigo wake duniani, ndivyo kinavyozidi kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha ushawishi wa Tanzania kimataifa, kukuza utamaduni wa Kiafrika na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Na Baraka Messa- MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam ( Sabasaba) yameendelea kuwa daraja muhimu linalowaunganisha wazalishaji, wanunuzi, wafanyabiashara, masoko na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa maonesho hayo ya 50 Julai 3,2026 jijini Dares Salaam amesema maonesho hayo yamekuwa sehemu ya maisha ya Watanzania wengi, huku yakitoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo kukua na kuwa wawekezaji wakubwa kupitia upatikanaji wa masoko na mitaji. “Kwa karibu miaka 50, maonesho ya Sabasaba yamekuwa daraja la kuwaunganisha wazalishaji, wanunuzi, wafanyabiashara, masoko na wawekezaji, huku yakiiunganisha Tanzania na dunia katika biashara na uwekezaji.” amesema. Amesema maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, huku mafanikio hayo yakichangiwa na maboresho makubwa ya miundombinu na matumizi ya teknolojia yaliyofanywa na Serikali. Aidha, Rais Samia amesema diplomasia ya uchumi imeendelea kuzaa matunda ambapo katika mwaka uliopita mauzo ya bidhaa na huduma za Tanzania nje ya nchi yalifikia takribani dola za Marekani bilioni 17, sawa na ongezeko la asilimia 15 ikilinganishwa na kipindi kilichopita. Pia, mauzo ya dhahabu yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia 35, yakionesha ukuaji wa sekta ya madini. Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo, amesema Tanzania na Msumbiji zinapaswa kutumia historia yao ya ushirikiano kuimarisha uchumi wa kikanda kwa kubadilisha mipaka ya nchi hizo kuwa korido za maendeleo, biashara na uwekezaji badala ya kuwa vikwazo Amesema uchumi wa Tanzania na Msumbiji unakamilishana na una fursa kubwa ya kukuza minyororo ya thamani, biashara ya kikanda na uwekezaji kutokana na rasilimali nyingi, nguvu kazi ya vijana na nafasi ya kimkakati inayounganisha Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kupitia Bahari ya Hindi. Aidha, Rais Chapo amewataka wawekezaji wa ndani na nje ya Afrika waitazame Tanzania na Msumbiji kama washirika wa kuaminika wenye mazingira rafiki ya biashara, huku akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika viwanda, sayansi, ubunifu, uchumi wa kidijitali na akili Unde (AI).

Na Baraka Messa – MAELEZO Serikali imesema Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili litakalofanyika jijini Paris, Ufaransa, kuanzia Julai 4 hadi 7, 2026, litakuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania na Afrika kwa ujumla kupitia lugha ya Kiswahili, huku likitarajiwa kufungua fursa mpya za biashara, utalii na uwekezaji. Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza kuhusu maandalizi ya kongamano hilo, akieleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha Kiswahili kinatumika kama lugha ya kimkakati katika kuchochea maendeleo ya uchumi. Jitihada za Serikali ni kuhakikisha Kiswahili kinatumika kama lugha ya kimkakati ili kiwe chachu ya kukuza biashara, kutangaza utalii na kuvutia wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani,” amesema Msigwa. Amesema Kiswahili kwa sasa si lugha ya mawasiliano pekee, bali ni rasilimali yenye fursa nyingi za kiuchumi, kielimu na kidiplomasia ambazo zinaendelea kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha maendeleo ya lugha hiyo duniani. Msigwa amesema mafanikio yaliyopatikana kupitia Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililofanyika Cuba yameongeza hadhi ya Kiswahili kimataifa, ambapo kwa sasa baadhi ya taasisi za elimu nchini Urusi na Ufaransa zimeanza kufundisha lugha hiyo. Pia amesema Kiswahili kimeanza kuingizwa katika mifumo ya kidijitali ikiwemo mitandao ya Kijamii, jambo linaloonyesha namna lugha hiyo inavyozidi kupata nafasi katika maendeleo ya teknolojia na ubunifu duniani. Kwa mujibu wa Msigwa, kongamano la Paris litahusisha tamasha kubwa la maonyesho ya Kiswahili, midahalo kuhusu tafiti na makala mbalimbali zinazohusu lugha hiyo pamoja na shughuli za kubadilishana uzoefu kati ya wadau kutoka mataifa mbalimbali. Takribani washiriki 1,000 wanatarajiwa kushiriki kongamano hilo, wakiwemo mabalozi, wawakilishi wa UNESCO, wataalamu kutoka vyuo vikuu, wafanyabiashara pamoja na taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa. Amesema Serikali inaamini kuwa kupitia kongamano hilo, Kiswahili kitaendelea kujijengea heshima duniani na kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kukuza biashara, utalii na uwekezaji kwa manufaa ya Tanzania na Afrika kwa ujumla. Mwisho

Na Josephina Lupasha – MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania inaendelea kupiga hatua kuelekea kujitegemea katika kugharamia shughuli za maendeleo kutokana na kuongezeka kwa mapato ya ndani huku akieleza kuwa mchango wa makampuni, mashirika na taasisi za umma unaendelea kuwa nguzo muhimu katika safari hiyo. Rais Samia amesema hayo Juni 30, 2026, wakati wa hafla ya kupokea gawio kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma, Ikulu jijini Dar Es Salaam. Rais Samia ameeleza kuwa mafanikio hayo yatachangia kupunguza pengo la kujitegemea katika bajeti ya mwaka huu na kwa miaka miwili ijayo jambo linaloonyesha kuwa mikakati ya kuongeza mapato ya ndani imeanza kuzaa matunda. “Gawio na mchango uliotolewa na makampuni, taasisi na mashirika yetu ni sehemu ya lengo letu la kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi katika kugharamia shughuli za maendeleo” amesema Rais Samia Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa matumaini yataongezeka endapo kasi ya ukusanyaji wa mapato na ufanisi wa taasisi utaendelea kuimarika ndani ya miaka miwili ijayo, Tanzania itakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kugharamia maendeleo yake kwa kutegemea vyanzo vya ndani pekee. Pamoja na mafanikio hayo, Rais Samia amewaelekeza viongozi na watendaji wote kutoridhika na pongezi wanazopata, bali amewasisitiza kuwa, pongezi hizo zinapaswa kuwa chachu ya kuongeza bidii, ubunifu na maarifa ili kufikia matokeo makubwa zaidi katika utoaji wa huduma na uzalishaji wa mapato. Kadhalika, ameeleza kuwa maendeleo ya uchumi wa Taifa yanahitaji uwajibikaji, usimamizi madhubuti wa rasilimali na juhudi endelevu kutoka kwa taasisi zote za umma ili kuhakikisha mchango wao unaendelea kuimarisha uwezo wa Serikali kugharamia miradi ya maendeleo.

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amevigiza vituo vya utafiti wa afya nchini kushirikiana na wabobezi wa tafitri duniani, kutafuta sababu za ongezeko la saratani na moyo kwa watoto wadogo ili kupata sababu zinazosababisha ongezeko la maradhi hayo na kutoa elimu kwa Watanzania ili kuepuka mambo yanayosababisha saratani kwa watoto. Rais Samia ametoa maagizo hayo Juni 24, 2026 wakati wa uzinduzi wa huduma za tiba mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC mjini Moshi,  na kueleza kuwa uwepo wa tiba mionzi katika Kanda ya Kaskazini, utasaidia kupunguza changamoto kwa wagonjwa wa saratani ambao awali walilazimika kwenda maeneo mengine yakiwemo Dar es Salaam kupata matibabu. Hili ni suala la kuangalia kwa kina hasa watafiti wetu. Vituo vyetu vya watafiti wa afya kwa kushirikiana na waliotuzidi ujuzi duniani, tuzame kutafuta sababu zinazoleta ongezeko la maradhi hayo kwa watoto wetu na kutoa elimu ya kutosha kwa jamii ya Watanzania ili kuepuka yale yote yanayofanya tulete watoto wenye maradhi hayo duniani”, ameelekeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Amesema ili kuimarisha huduma za afya nchini zikiwemo kinga, uchunguzi, na matibabu, Serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika huduma hizo, ambapo imetoa shilingi bilioni 5.5 kusaidia kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi. “Hospitali ya rufaa ya KCMC ina heshima kubwa hapa nchini na hata jirani kwa huduma bobezi na za kibingwa zinazotolewa hapa. Uzinduzi wa jengo hili la tiba mionzi ni hatua nyingine muhimu katika kusogeza huduma hizo karibu na wananchi”, ameeleza Rais Samia. Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusogeza huduma kubwa za afya ikiwemo matibabu ya saratani na magonjwa ya moyo katika maeneo mbalimbali ili wananchi wapate huduma karibu na wanapoishi na kwamba uwepo wa hospitali hiyo ya rufaa KCMC ni faraja kubwa kwa familia nyingi zilizokuwa zikibeba gharama na usumbufu wa kusafiri kwenda mikoa mingine kufuata matibabu. Rais Samia amewashukuru wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za afya, taasisi za dini na mashirika ya maendeleo yaliyoshiriki katika kufanikisha mradi huo, akisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuboresha huduma za afya nchini. Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema kituo hicho kwa sasa kina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 1,100 kwa mwaka na kikikamilika kitaweza kuhudumia zaidi ya wagonjwa 3,900 kwa mwaka. Mhe. Mchengerwa amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kupunguza gharama kwa familia, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini umeendelea kuwa nguzo muhimu katika utoaji wa huduma bora za afya. Mwisho

Na Baraka Messa – MAELEZO Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha kwa kishindo Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027, baada ya Wabunge wengi kuunga mkono mapendekezo ya matumizi na makusanyo ya Serikali yaliyowasilishwa bungeni. Akitoa matokeo ya kura zilizopigwa Juni 23, 2026, Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amesema jumla ya wabunge 395 walihudhuria kikao hicho huku wabunge wanane wakikosekana. Mhe. Zungu amesema kati ya wabunge waliohudhuria, wabunge 385 walipiga kura za ndiyo, sawa na asilimia 97.26 ya kura zote zilizopigwa, huku wabunge wanane wakipiga kura za hapana. Matokeo hayo yamedhihirisha uungwaji mkono mkubwa wa bajeti hiyo kutoka kwa wajumbe wa Bunge. Kupitishwa kwa bajeti hiyo kunatoa idhini kwa Serikali kuendelea kutekeleza mipango yake ya maendeleo pamoja na shughuli za kawaida za kiutawala katika mwaka mpya wa fedha. Bajeti hiyo imelenga kuimarisha uchumi wa taifa, kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali, kuboresha utoaji wa huduma za jamii na kuendeleza miradi ya kimkakati inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema Serikali imejipanga kikamilifu kutekeleza mipango ya maendeleo yenye lengo la kuimarisha uchumi wa taifa na kuongeza ustawi wa wananchi. Amesema bajeti ya mwaka 2026/2027 imeandaliwa kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya taifa sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Prof. Mkumbo amesisitiza umuhimu wa uwekezaji katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, hususan vijana huku akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hatua itakayochangia kuongezeka kwa uzalishaji na mapato ya taifa. Aidha, ametoa wito kwa wananchi, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango na miradi iliyopangwa, ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya Watanzania katika miaka ijayo.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika, Prof. Mohamed Janabi, ametoa rai kwa nchi za Afrika kuwekeza zaidi kwenye afya hasa upande wa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kwani afya haijawahi kuwa gharama na ni uwekezaji ambao nchi inaweza kuona faida yake. Ametoa rai hiyo Juni 23, 2026 wakati akizungumza katika Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Mkakati wa Kikanda wa PEN-Plus wa kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika (ICPPA) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam. Prof. Janabi amesema kuwa nchi inaweza kufanya magonjwa yasiyoambukiza kuwa kipaumbele cha maendeleo ya kitaifa kwa kutumia sera za kifedha zinazoweza kuokoa maisha ikiwa ni pamoja na kodi kwenye tumbaku, pombe na bidhaa zote zenye sukari, kupanua ulinzi wa kifedha ili ugonjwa usimaanishe umaskini, kuongeza kiwango cha mpango wa Pen na Pen-Plus kitaifa pamoja na kuwalinda watoto kwa kutengeneza mazingira yenye afya bora. Tunaweza kuwa na vipaumbele vingi lakini tunasahau kuwa vipaumbele vinahitaji vitendo. Magonjwa yasiyoambukiza si tishio la baadaye tena katika bara letu bali ni ukweli wa sasa kwani yanasababisha asilimia 37 ya vifo. Magonjwa kamwe hayapaswi kuamua hatma ya mtu kwa sababu kila maisha ya Mwafrika yana thamani na utu sawa”, amesema Prof. Janabi. Akizungumzia kuhusu Pen-Plus, amesema kuwa inafanya kazi katika nchi zaidi ya 20 na imeweza kuokoa maisha ya watu zaidi ya 100,000 huku akisisitiza kuwa si miradi ya majaribio tu bali ina ushahidi kwani kupitia kuimarisha afya, watoto wanarudi shuleni, vijana wanaishi maisha marefu na akina mama wanajifungua salama na kuishi.  Akizungumza kwa niaba ya Washirika wa Maendeleo, Bw. James Reid kutoka Mfuko wa Hisani wa Helmsley Charitable Trust ameeleza kuwa, kwa muda mrefu wananchi wenye magonjwa yasiyoambukiza hasa wanaoishi katika maeneo ya vijijini kwenye ukanda wa Afrika, wanakabiliwa na changamoto zikiwemo za huduma za afya zisizofikika, kukosa wafanyakazi wa afya waliofunzwa na mifumo michache ya kuwahudumia wagonjwa hao pamoja na ukosefu wa vifaa vya uchunguzi, dawa au huduma za ufuatiliaji. “Tunahitaji kuendelea kupanua idadi ya nchi zinazohusika katika mtandao huu ili kufikia malengo ya kikanda ya nchi wanachama wa WHO. Tunahitaji kuendelea kujenga na kuimarisha nguvu kazi inayofanya huduma hii iwezekane, tunahitaji kufanya kazi pamoja na nchi husika ili kuhakikisha kuwa kuna ufadhili endelevu na kuhakikisha kuwa mfumo huu unaweza kuendelea kupanuka”, amemalizia Bw. Reid. PEN-Plus ni mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mtandao wa NCDI Poverty unaolenga kupanua huduma za afya kwa ajili ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) yaliyo sugu na makali. Mpango huu unapanua wigo wa huduma kutoka ngazi za chini ili wagonjwa wapate matibabu katika hospitali za wilaya au rufaa za ngazi ya kwanza bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Na Baraka Messa- MAELEZO  Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, amesema Tanzania itaendelea kuwa sehemu muhimu katika historia ya Namibia kutokana na mchango wake mkubwa wa kuhifadhi na kusaidia wapigania uhuru waliowezesha taifa hilo kupata uhuru, akieleza kuwa Kongwa ni moja ya maeneo yenye thamani kubwa katika historia ya ukombozi wa Afrika. Dkt. Nandi-Ndaitwah ametoa kauli hiyo Juni 21, 2026 alipotembelea eneo la kihistoria la Kambi ya Wapigania Uhuru wa Namibia wilayani Kongwa mkoani Dodoma, katika ziara yake ya kwanza ya Kiserikali nchini Tanzania tangu aingie madarakani. Amesema ziara hiyo imekuwa ya kipekee kwake na kwa wananchi wa Namibia kwa kuwa imewapa fursa ya kushuhudia kwa macho yao sehemu ambayo mashujaa wa taifa hilo waliwahi kuishi, kupata mafunzo na kujiandaa kwa ajili ya mapambano ya ukombozi dhidi ya ukoloni. Kongwa ni mahali Patakatifu pa ukombozi kwa sababu nchi nyingi zilizopigania uhuru zilipata hifadhi na mafunzo hapa. Mashujaa wetu wamelala mahali hapa na damu yao ilimwagilia uhuru wetu,”amesema. Amewataka Watanzania na Wanamibia kuendeleza ushirikiano uliowekwa na waasisi wa mataifa hayo kwa kushirikiana katika kukamilisha ukombozi wa kiuchumi wa nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla ili kuleta maendeleo na ustawi wa wananchi. Akizungumzia umuhimu wa kuhifadhi historia hiyo, Rais Netumbo amesema ni wajibu wa kizazi cha sasa kuhakikisha mchango wa mashujaa wa ukombozi unaenziwa na kulindwa ili maadili, misingi na malengo waliyozipigania visiweze kupotea kwa vizazi vijavyo. Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Tanzania na Namibia zina historia moja ya ukombozi na zinaendelea kushirikiana katika kutimiza azma ya kukamilisha ukombozi wa Afrika kupitia maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Prof. Kabudi amesema Serikali ya Tanzania imejipanga kuhifadhi maeneo yote ya kihistoria yaliyotumiwa na wapigania uhuru kwa kuyaacha katika hali yake ya asili ili kulinda uhalisia wa historia hiyo, huku ikiendelea kuboresha miundombinu katika maeneo jirani kwa ajili ya matumizi ya sasa na ya baadaye.  

Na Baraka Messa – MAELEZO Serikali imekamilisha hatua muhimu za kisheria zitakazowezesha kuanza kwa malipo ya kifuta jasho kwa askari waliojitolea kushiriki Vita ya Kagera dhidi ya utawala wa Idd Amin mwaka 1978/79 ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika kulinda uhuru na usalama wa Taifa. Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akijibu maswali ya papo kwa papo Juni, 18, 2026, bungeni Dodoma, amesema kuwa vikwazo vya kisheria vilivyokuwa vinazuia utekelezaji wa malipo hayo vimeondolewa kufuatia maelekezo ya Rais, hivyo kufungua njia kwa askari hao kupata stahiki zao baada ya kusubiri kwa muda mrefu. Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Njombe, Mhe. Deo Mwanyika, Mhe. Waziri Mkuu, amesema kuwa Serikali inaendelea na zoezi la utambuzi na uhakiki wa askari hao, ambapo takribani askari 7,200 wanatarajiwa kunufaika na mpango huo mara baada ya taratibu husika kukamilika. Hatua hii ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuthamini na kutambua mchango wa wananchi walioweka maisha yao rehani katika nyakati muhimu za historia ya Taifa. Mwaka 2025 Serikali ilikamilisha zoezi la kuwatambua baadhi ya washiriki wa vita hii kutoka Uganda waliokuwa na mchango katika harakati za kuikomboa nchi wakati wa Vita vya Kagera, hatua iliyoweka msingi wa kuendelea kuwathamini wote walioshiriki katika mapambano hayo,” amesema Mhe. Waziri Mkuu. Vita ya Kagera ya mwaka 1978/79 inabaki kuwa moja ya matukio muhimu katika historia ya Tanzania na Afrika Mashariki, ambapo majeshi ya Tanzania kwa kushirikiana na wapigania uhuru wa Uganda yaliweza kuondoa utawala wa Idd Amin na kurejesha usalama katika eneo hilo.