Rais Samia Kuzindua Mji wa Serikali Mtumba Oktoba 30
Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi majengo na miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Oktoba 30, 2026, katika hatua inayolenga kuimarisha ufanisi wa utendaji wa Serikali na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari, katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO jijini Dodoma, Oktoba 25, 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali imewekeza takribani shilingi bilioni 700 katika ujenzi wa mji huo.
Msigwa amesema ujenzi wa majengo ya kisasa ya wizara na taasisi za Serikali ulianza mwaka 2021, chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, ukiwa ni sehemu ya utekelezaji wa uamuzi wa kuhamishia shughuli za Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, uliotangazwa mwaka 2016 na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Ameeleza kuwa Mji wa Serikali Mtumba umejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya kiutendaji, ukiwa na takribani kilomita 59 za barabara pamoja na mifumo ya kisasa ya mawasiliano inayowezesha taasisi za Serikali kuwasiliana na kutekeleza majukumu yake kwa njia ya mtandao.
Amesema mifumo hiyo itapunguza urasimu na muda wa kushughulikia nyaraka, hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji wa Serikali na kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Faili likifika asubuhi linajibiwa mchana kwa sababu hakuna sababu ya kutuma watu na magari na bodaboda kwenda kusambaza barua. Barua zinatembea kwa mtandao.
Aidha, amesema Tanzania imepokea ujumbe kutoka nchi zaidi ya 10 zilizofika kujifunza kuhusu ujenzi na uendeshaji wa Mji wa Serikali Mtumba, akibainisha kuwa miundombinu hiyo ina fursa ya kuwa kivutio cha utalii jijini Dodoma.
Msigwa amewahimiza Watanzania kufuatilia uzinduzi huo, akieleza kuwa ni tukio muhimu katika historia ya maendeleo ya Dodoma na utekelezaji wa uamuzi wa kuifanya kuwa makao makuu ya Serikali.