Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Ujenzi Uwanja wa Ndege Msalato wafikia asilimia 89

September 24, 2026

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO

Ujenzi wa miundombinu ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma umefikia asilimia 89.02, huku ujenzi wa majengo ukifikia asilimia 78.37 na kazi mbalimbali za ukamilishaji zikiendelea kwa kasi.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema hayo Septemba 24, 2026, jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka 2026/27.

Kwa mujibu wa taarifa ya mradi, ujenzi wa jengo la abiria umefikia asilimia 81, mnara wa kuongozea ndege asilimia 74, Kituo cha Huduma za Zimamoto asilimia 88, jengo la kituo kikuu cha umeme asilimia 71 na jengo la huduma za hali ya hewa (MTO) asilimia 87.

Mhandisi Besta amesema kazi zinazoendelea ni pamoja na kukamilisha majengo, kufunga mifumo ya mitambo ya uendeshaji wa uwanja, umeme na mabomba, mifumo ya mawasiliano na ukaguzi wa mizigo, pamoja na kufunga madaraja ya kupita abiria, mifumo ya hali ya hewa na magari ya zimamoto.

Mradi huo pia umeendelea kutoa ajira kwa Watanzania. Mhandisi Besta amesema hadi sasa jumla ya ajira 9,059 zimezalishwa katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi.

Amefafanua kuwa kati ya ajira hizo, 3,571 zimehusisha ujenzi wa miundombinu na 5,488 ujenzi wa majengo, huku wafanyakazi wa kigeni wakiwa 47.

Kwa mujibu wa Mhandisi Besta, ujenzi wa miundombinu ya mradi unatarajiwa kukamilika Novemba 27, 2026, wakati ujenzi wa majengo ukitarajiwa kukamilika Desemba 30, 2026.

Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria na mizigo, na kuimarisha nafasi ya Dodoma katika shughuli za kitaifa na kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *