Watanzania Tuendelee Kulinda Amani-Msigwa
Na Neema Kaniki– MAELEZO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kukuza uchumi na kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Amesema hayo Oktoba 25, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa jengo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo jijini Dodoma, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo na ustawi wa wananchi.
Msigwa amesema Serikali inaendelea kutekeleza majukumu yake chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ukiwa umeanza kupitia bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa ulioanza Julai Mosi, 2026.
Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 imeweka lengo la kujenga uchumi wenye thamani ya Dola za Marekani trilioni moja kutoka takribani Dola bilioni 90 za Marekani, hatua inayohitaji ushiriki na uwajibikaji wa pamoja kutoka kwa Serikali, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo.
Mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 yanahitaji uwajibikaji wa pamoja kwa wadau wote, Serikali inatarajiwa kuchangia asilimia 30 ya uchumi huo, huku sekta binafsi ikitarajiwa kuchangia asilimia 70.
Amesisitiza kuwa kufikiwa kwa malengo hayo kunategemea uwepo wa mazingira ya amani na utulivu yatakayowawezesha wananchi kujikita katika shughuli za uzalishaji mali, biashara, hususan biashara ya nje, pamoja na kuboresha maisha yao na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Amesema vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani vinaweza kukwamisha shughuli za kiuchumi, kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi, hivyo kuwataka Watanzania kutokubali kushawishiwa kushiriki matukio yanayoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.
Natoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kujiepusha na matukio yenye viashiria vya vurugu na uvunjifu wa amani, Watanzania wakatae watu wanaodhani wanaweza kufanikisha ajenda zao kwa kuwahamasisha kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria, pakichafuka hapa, hakuna mjomba wa kutusaidia zaidi ya sisi wenyewe.
Aidha, Msigwa amewahakikishia wananchi kuwa Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kusimamia amani na usalama wa watu na mali zao, pamoja na kulinda mipaka ya nchi, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria kwa sababu ya kauli au msimamo wake.