Tanzania Yaweka Lengo la Kuingia Nchi 10 Bora kwa Uzalishaji wa Chakula Duniani
Na Mwandishi Wetu – MAELEZO
Tanzania imeweka lengo la kuwa miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza duniani kwa uzalishaji wa chakula, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uchumi, kuongeza ajira na kuhakikisha usalama wa chakula kwa wananchi, kupitia uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema azma hiyo imeainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050, inayolenga pia kuifanya nchi kuwa mzalishaji mkuu wa chakula barani Afrika.
Akizungumza Oktoba 22, 2026, jijini Des Moines, Iowa, Marekani, wakati akiwasilisha mada kuu kuhusu mustakabali wa kilimo barani Afrika katika Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue), Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea kukipa kilimo kipaumbele kutokana na mchango wake katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa.
Amesema chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi shilingi trilioni 1.241 mwaka 2025/2026, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kukifanya kilimo kuwa injini ya mageuzi ya kiuchumi, uzalishaji wa ajira, ukuaji wa viwanda na upanuzi wa masoko ya nje.
Matokeo ya uwekezaji huo yanaonekana katika kiwango cha utoshelevu wa chakula nchini, ambacho kimefikia asilimia 130, hali inayoiwezesha Tanzania kukidhi mahitaji yake na kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya kikanda na kimataifa.
Aidha, mauzo ya nje ya mazao ya kilimo yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 2.1 mwaka 2021/2022 hadi dola bilioni 3.7 mwaka 2024/2025, hatua inayoonesha nafasi inayozidi kuimarika ya kilimo katika kukuza biashara na mapato ya taifa.

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba anaeleza kuwa kilimo ni moja ya nguzo kuu za uchumi wa Tanzania, kikichangia asilimia 24.6 ya Pato la Taifa, kuajiri asilimia 65 ya nguvu kazi na kuzalisha takriban asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje, huku kikiendelea kutoa malighafi muhimu kwa viwanda vya ndani.
Pamoja na mafanikio hayo, anasema Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza kilimo kinachozingatia usalama na ubora wa chakula. Katika mkutano huo, Dkt. Mwigulu amempongeza Prof. Huub Lelieveld, mshindi wa Tuzo ya Chakula Duniani ya mwaka 2026, kwa mchango wake katika masuala ya usalama wa chakula.
Amesisitiza kuwa usalama wa chakula haupimwi kwa upatikanaji pekee, bali chakula kinapaswa kuwa salama kwa matumizi, kuwa na virutubisho vinavyohitajika na kupatikana kwa bei nafuu ili wananchi waweze kumudu mahitaji yao ya lishe.
Akizungumzia kaulimbiu ya mjadala huo, “Kabla Njaa Haijatushinda,” Waziri Mkuu amesema Afrika ina uwezo mkubwa wa kuwa mchangiaji muhimu wa usalama wa chakula duniani, badala ya kuendelea kuonekana kama bara linalokabiliwa na changamoto za upatikanaji wa chakula.
Amesema kufikia azma hiyo kunahitaji uwekezaji zaidi kwa wakulima, vijana na wanawake, pamoja na kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na mifumo imara ya uzalishaji na usambazaji wa chakula.
Waziri Mkuu amehimiza mataifa ya Afrika kuchukua hatua za pamoja, kuendeleza ubunifu na kujenga mifumo endelevu ya chakula inayoweza kukidhi mahitaji ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mhariri Mkuu wa Jarida la Afrika la Chakula, Kilimo, Lishe na Maendeleo, Prof. Ruth Oniang’o, amesema anaamini Tanzania inaweza kuwa mfano kwa mataifa mengine kutokana na hatua inazopiga katika sekta ya kilimo.
Prof. Oniang’o amesifu jitihada za Serikali, hususan uwekezaji katika miundombinu, utekelezaji wa programu ya Jenga Kesho Bora (BBT) na matumizi ya maafisa ugani kuwasaidia wakulima kuboresha uzalishaji.

Kwa ujumla, lengo la Tanzania kuingia katika orodha ya nchi 10 bora duniani kwa uzalishaji wa chakula linaweka msisitizo katika kuendeleza uwekezaji, kuongeza tija na kutumia fursa za masoko ya kimataifa. Utekelezaji wake utahitaji kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao, kupanua fursa kwa wakulima na kuhakikisha chakula kinachozalishwa kinakidhi viwango vya ubora na usalama.
Dkt. Mwigulu amehudhuria mkutano huo akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe; Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde; Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie Kanza, pamoja na watendaji wengine wa Serikali.