Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Rais Samia Atoa Maagizo Kukomesha Migogoro ya Ardhi Nchini

November 27, 2026

Na Neema Kaniki – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaagiza viongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuchukua hatua za kukomesha migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, pamoja na kudhibiti vitendo vya baadhi ya maafisa wasio waaminifu wanaogawa kiwanja kimoja kwa watu zaidi ya mmoja.

Akizungumza leo Novemba 27, 2026, mara baada ya kuwaapisha viongozi wapya aliowateua Ikulu, Rais Dkt. Samia amemtaka Waziri wa wizara hiyo kuendeleza kampeni ya Kliniki za Ardhi kwa kasi ili kuwafikia wananchi na kutatua kero zao.

Nendeni kwa wananchi, sikilizeni matatizo yao myatatue. Msiwaache watu wauane kwa sababu ya ardhi.

Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza pia umuhimu wa kukamilisha miradi ya upimaji wa ardhi na kuhakikisha matumizi ya ardhi yanafuata mipango iliyowekwa.

Katika sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Rais Dkt. Samia amemtaka Waziri pamoja na viongozi wapya wa wizara hiyo kushirikiana na wataalamu katika kutekeleza majukumu yao. Aidha, ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutafuta vifaa na mifumo sahihi ya kuchuja maudhui yasiyofaa kwenye mitandao ya kijamii ili kulinda jamii, hususan watoto.

Nendeni mkatazame vifaa gani vinatakiwa, mfumo gani unahitajika na tufanye nini ili tuweze kuchuja maudhui hayo. Yale yasiyo na maadili tuyazuie, na yenye maadili yawafikie wananchi.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi kuunda timu ya wahandisi itakayochunguza makadirio ya gharama za ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, baada ya kueleza kuwa gharama zilizowasilishwa ni kubwa na kushindwa kuyaidhinisha.

Amesema mvutano kuhusu gharama hizo unasababisha kuchelewa kwa kazi za ukarabati, wakati Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) likisubiri kufanya ukaguzi wa uwanja huo kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Vilevile, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa amepandisha hadhi Idara ya Habari (MAELEZO) na kuifanya kuwa idara inayojitegemea, huku akimuagiza Mkurugenzi wa Idara hiyo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Ayub Rioba kuhakikisha mafanikio ya sekta mbalimbali yanawafikia wananchi kupitia taarifa sahihi, pamoja na kuhakikisha malalamiko na changamoto zinazowasilishwa na wananchi zinapatiwa majibu kwa wakati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts