Na Bupe Mwaiseje – Dodoma Elimu ya juu ni moja ya nguzo muhimu katika kujenga Taifa lenye wataalamu, wabunifu na vijana wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uchumi. Kutambua umuhimu huo, Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kuongeza fursa za elimu na kuwaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na ujasiriamali. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imewekeza jumla ya Sh bilioni 67.9 katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), uwekezaji unaolenga kuongeza uwezo wa taasisi hiyo kutoa elimu bora na kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa na ujuzi wa kuajiriwa au kujiajiri. Uwekezaji huo umeleta mabadiliko yanayoonekana katika ukuaji wa TIA, kuanzia upanuzi wa kampasi, ongezeko la wanafunzi, maboresho ya programu za masomo, uimarishaji wa rasilimali watu na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za elimu. Akizungumza kuhusu utekelezaji wa shughuli za TIA kwa mwaka wa fedha 2026/27 katika Ukumbi wa Idara ya Habari–MAELEZO, Mtumba jijini Dodoma, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Amos Palangyo, amesema uwekezaji huo umeelekezwa katika kuboresha miundombinu kwenye kampasi za Mtwara, Mbeya, Singida, Kigoma, Mwanza na Zanzibar. Mbali na uwekezaji wa Sh bilioni 67.9, TIA imepata Sh bilioni 27.8 kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET). Fedha hizo zimeelekezwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo miundombinu, TEHAMA, samani, mafunzo ya wahadhiri, maboresho ya mitaala, tathmini na shughuli nyingine za mradi. Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 22.6 zimetumika moja kwa moja katika ujenzi wa miundombinu ya Kampasi za Singida na Mwanza. Matokeo ya uwekezaji huo yanaonekana katika upanuzi wa TIA kutoka kuwa na kampasi sita mwaka 2021/22 hadi kufikia kampasi nane mwaka 2025/26, baada ya kuongezwa kwa kampasi za Tanga na Zanzibar. Ukuaji huo umeenda sambamba na ongezeko la idadi ya wanafunzi. Kutoka wanafunzi 24,494 mwaka 2021/22, idadi hiyo imefikia 37,397 mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 52.7. Wakati huohuo, uwezo wa taasisi kuhudumia wanafunzi umeongezeka kwa asilimia 35. Haya si mabadiliko ya miundombinu pekee; ni upanuzi wa fursa kwa Watanzania wengi zaidi kupata elimu ya juu na ujuzi unaohitajika katika kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya Taifa. Katika kuhakikisha elimu inayotolewa inaendana na mahitaji ya uchumi wa sasa, TIA imeongeza programu za masomo kutoka 49 hadi 54. Miongoni mwa programu hizo ni Shahada ya Maendeleo ya Biashara na Ujasiriamali pamoja na Shahada ya Uchumi na Fedha, ambazo zinalenga kuwajengea vijana uwezo katika biashara, ujasiriamali, uchumi na usimamizi wa fedha. Kwa upande wa mikopo ya elimu ya juu, wanafunzi 19,342 katika kampasi za Tanga, Dar es Salaam, Mwanza, Singida, Mbeya, Kigoma na Mtwara wamenufaika na mikopo hiyo. Aidha, jumla ya wahitimu 62,680 wamehitimu na kuingia katika maeneo mbalimbali ya ajira, ujasiriamali na huduma za kitaaluma. Prof. Pallangyo anasema ubora wa elimu hauwezi kutenganishwa na ubora wa walimu na wahadhiri. Kwa kutambua hilo, Serikali imeiwezesha TIA kupata maprofesa tisa na kugharamia watumishi 78 kusoma Shahada za Uzamivu (PhD) ndani na nje ya nchi. Kati yao, watumishi 48 tayari wamehitimu, huku 30 wakiendelea na masomo. Hatua hiyo imeongeza uwezo wa TIA katika ufundishaji, utafiti, ubunifu na uzalishaji wa maarifa. Sambamba na hilo, taasisi imeanzisha programu za Shahada ya Uzamili katika kampasi za Zanzibar, Mbeya, Singida na Mwanza. Hivyo, uwekezaji katika rasilimali watu unaendelea kuifanya TIA kuwa taasisi inayozalisha wahitimu pekee wenye maarifa na ubunifu unaoweza kutumika katika kutatua changamoto za jamii. Moja ya mafanikio yanayoipa thamani zaidi elimu inayotolewa TIA ni juhudi za kuwaunganisha wanafunzi na fursa za ajira na ujasiriamali. Zaidi ya wanafunzi 5,000 wamefikiwa kupitia warsha zinazohusu ujasiriamali, ubunifu, ajira na fursa za kimataifa. Wakati huohuo, zaidi ya wanafunzi 500 wamepatiwa mafunzo mahsusi ya ujasiriamali na takribani 100 wamewezeshwa kuanzisha biashara ndogo ndogo. Anasema mfano wa matokeo ya juhudi hizo ni Nicolaus Carol Mboya, mmoja wa wahitimu wa TIA ambaye ameanzisha kampuni ya STEAMORA inayotoa mafunzo ya teknolojia ya elimu kwa watoto na vijana. Kupitia STEAMORA, vijana wanapata mafunzo katika teknolojia mbalimbali ikiwemo roboti, upangaji programu (coding), ubunifu wa miundo ya pande tatu (3D) na akili bandia (AI). Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2026, kampuni hiyo imewafikia zaidi ya wanafunzi 600 kupitia ushirikiano na shule nane za kimataifa na vituo viwili vya kujifunzia vya kijamii jijini Dar es Salaam. Aidha, ina watumishi wanane na imezalisha zaidi ya Shilingi milioni 15 katika mapato jambo linalotoa taswira ya elimu inayokwenda hatua moja zaidi—elimu inayompa kijana si cheti pekee, bali pia uwezo wa kutengeneza fursa. TIA pia imeendelea kukuza utamaduni wa ubunifu kupitia Shindano la Ubunifu linalowapa wanafunzi nafasi ya kubadilisha mawazo yao kuwa suluhisho na fursa za biashara. Mwaka 2025, jumla ya mawazo 376 yaliwasilishwa katika shindano hilo. Kati yake, washindi 57 walipatikana na mawazo 17 yalifikia hatua ya kuanzishwa kuwa biashara zinazofanya kazi. Katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA TIA imeendelea kuboresha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma. Taasisi imeanzisha mfumo wa kidijitali wa kukusanya na kusimamia taarifa za wanafunzi (SIMS), unaowawezesha wanafunzi kupata huduma mbalimbali kuanzia maombi ya kujiunga, udahili na usajili, malipo, matokeo, huduma za maktaba hadi kujifunza kwa njia ya mtandao. Maboresho hayo yanalenga kuongeza ufanisi, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuendana na mahitaji ya kizazi cha sasa kinachokua katika mazingira ya kidijitali. Uwekezaji wenye matokeo kwa Taifa Kwa ujumla, uwekezaji unaofanywa na Serikali katika TIA unaonesha namna fedha zinazowekezwa katika elimu zinavyoweza kubadilika na kuwa fursa kwa vijana na Taifa kwa ujumla. Kutoka kwenye majengo na miundombinu hadi kwenye taaluma, TEHAMA, utafiti, ubunifu na ujasiriamali, uwekezaji huo umeiwezesha TIA kupanua wigo wa elimu ya juu na kuongeza uwezo wa kuzalisha wahitimu wenye maarifa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya dunia ya sasa.
Na Jacqueline Mrisho MAELEZO. Hatimaye Tanzania imeshuhudia kutimia kwa maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ya kujenga bwawa katika eneo la Stiegler’s Gorge kwenye Mto Rufiji kwa ajili ya kuzalisha umeme wa uhakika na wa kutosha kwa maendeleo ya Taifa. Wazo hilo lililoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1976 liliendelea kuenziwa na viongozi waliomfuata, wakiwemo Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin William Mkapa na Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Licha ya kukabiliwa na changamoto na upinzani mbalimbali ndani na nje ya nchi, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ilichukua hatua ya kutafuta fedha, kutatua changamoto na kuanza utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati. Leo, Bwawa la Mwalimu Nyerere limekuwa sehemu muhimu ya jitihada za Tanzania kuhakikisha Taifa linakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wenye uwezo wa kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii. Mradi huo una uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, hatua inayoongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Taifa kuzalisha umeme na kusaidia kuondoa changamoto ya upungufu na mgao wa umeme uliokuwa ukiathiri uzalishaji viwandani, huduma za jamii, biashara na matumizi ya majumbani. Umeme huo umefungua nafasi kubwa kwa uwekezaji, viwanda, biashara, utalii, uzalishaji na ajira, huku ukitoa fursa ya kuongeza kipato cha wananchi na kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa. Akizindua mradi huo Agosti 22, 2026, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema kukamilika kwa mradi huo ni fundisho kwamba mafanikio ya miradi ya kimkakati yanahitaji uthubutu, uthabiti na ufuatiliaji wa karibu. Tunapofanya maamuzi yenye maslahi kwa Taifa, hatupaswi kukata tamaa kwa sababu njia ya kufanikisha ni ngumu bali tunapaswa kuwa na uthubutu na uthabiti wa kuyasimamia maono na maamuzi yetu ili kufikia malengo tuliyojiwekea na manufaa tunayoyatarajia, alisema Rais Samia. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhe. Felischem Mramba, amesema mahitaji ya umeme nchini yanaongezeka kwa kati ya asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka, hali inayoashiria pia ukuaji wa shughuli za kiuchumi. Amesema Bwawa la Mwalimu Nyerere limekuwa msingi muhimu wa kuondoa mgao wa umeme na kuwezesha Tanzania kuendelea na uwekezaji katika uchumi wa viwanda, kuvutia wawekezaji, kuimarisha utalii na kukuza shughuli nyingine za uzalishaji. Bwawa hili limetutoa kwenye mgawanyo wa umeme kama nchi, na linatuhakikishia sasa kwamba tunaweza kuendelea kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda, tunaweza kualika wawekezaji kutoka nje wakaja kuwekeza kwenye uchumi wetu, tunaweza kuboresha utalii na mambo mengine mbalimbali ambayo ndiyo hasa yanayokuza uchumi wetu, amesema. Kukamilika kwa bwawa hilo ni hatua moja katika kuhakikisha umeme unaowafikia wananchi wote. Serikali inaendelea kuimarisha Gridi ya Taifa, ikiwemo kukamilisha njia ya umeme ya kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 345, pamoja na upanuzi wa kituo cha kupokea na kupooza umeme cha Zuzu, Dodoma. Kupitia kituo hicho, umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere unasafirishwa kwenda Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kaskazini. Jitihada hizo zimepanua wigo wa upatikanaji wa umeme, ambapo hadi sasa vijiji vyote 12,318 na takribani asilimia 62.4 ya vitongoji Tanzania Bara vimefikiwa na huduma hiyo. Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha nchi nzima inapata umeme ifikapo mwaka 2030. Uwezo mkubwa wa uzalishaji umeifanya Tanzania kuwa na umeme wa ziada, unaoweza kutumika kwa mahitaji ya ndani na kuuzwa katika nchi jirani ili kuongeza mapato na upatikanaji wa fedha za kigeni. Tayari Tanzania imepokea maombi kutoka nchi mbalimbali. Zambia imeonesha hitaji la kati ya Megawati 500 na 600, Rwanda inahitaji Megawati 100, huku Kenya ikikubaliana na Tanzania kuhusu uwezekano wa kufanya mabadilishano ya umeme. Hii inaifanya Tanzania kuingia katika hatua mpya, ambapo umeme hauwi tu huduma muhimu kwa maendeleo ya ndani, bali pia bidhaa yenye uwezo wa kuzalisha mapato na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi jirani. Pamoja na Bwawa la Mwalimu Nyerere, Serikali inaendelea kuwekeza katika vyanzo vingine vya nishati, ikiwemo jua, upepo na nishati ya jotoardhi (thermal), ili kuongeza uwezo wa Taifa kuzalisha umeme kulingana na kasi ya ukuaji wa uchumi. Hatua hizi zinaifanya Tanzania kujenga msingi wa nishati unaoweza kuhimili mahitaji ya sasa na ya baadaye, huku ukifungua milango zaidi kwa viwanda, uwekezaji, biashara na ajira. Kukamilika kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa hatua mpya ya Tanzania yenye nishati ya kutosha, uchumi unaokua na fursa zinazoongezeka kwa wananchi.
Na Baraka Messa – MAELEZO Utambulisho ni msingi muhimu katika maisha ya kila mwananchi, kwani humwezesha mtu kutambulika kisheria, kupata huduma za kijamii na kiuchumi, kushiriki katika shughuli za maendeleo na kutekeleza haki na wajibu wake kwa urahisi. Kutokana na umuhimu huo, Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Utambulisho Duniani, Septemba 16, 2026, huku nchini maadhimisho hayo yakianza Septemba Mosi kupitia shughuli mbalimbali zinazofanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika wilaya mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar. Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, anasema maadhimisho hayo yanafanyika wakati dunia ikiendelea kutafuta suluhisho la changamoto ya mabilioni ya watu ambao hawana utambulisho rasmi, hali inayowakosesha fursa ya kupata baadhi ya huduma muhimu. Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho hayo katika Kituo cha Urithi wa Ukombozi jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Msigwa amesema tathmini mbalimbali zinaonesha kuwa Bara la Afrika lina idadi kubwa ya watu wasio na utambulisho wa kisheria. Anasema hali hiyo imechochea juhudi za pamoja za mataifa ya Afrika na wadau mbalimbali kuhakikisha kila mtu anapata utambulisho rasmi unaomwezesha kutambulika na kupata haki pamoja na huduma muhimu za kijamii na kiuchumi. Katika safari hiyo, Msigwa amesema Tanzania imejijengea nafasi muhimu kutokana na hatua ilizochukua mapema kuanzisha mfumo wa usajili na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa, hatua ambayo imeendelea kuimarisha mifumo ya utambulisho nchini. Anasema mchakato wa usajili na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa ulianza mwaka 2012 kwa majaribio katika Mkoa wa Dar es Salaam, kabla ya kupanuliwa katika maeneo mengine nchini kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Msigwa anasema, NIDA imepewa majukumu mbalimbali ya msingi, yakiwemo kuwatambua na kuwasajili watu wanaoishi nchini wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, kutoa Vitambulisho vya Taifa kwa raia na wageni wakazi, pamoja na kutunza takwimu za usajili na utambuzi wa watu na kushirikishana taarifa hizo na wadau kwa mujibu wa sheria. Tanzania imepiga hatua kubwa katika usajili. Kufikia Julai 2026, jumla ya watu 27,455,882 wamesajiliwa, sawa na asilimia 87.2 ya watu wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, ambao ni 31,477,938 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, anasema Msigwa. Anasema katika kipindi hicho, jumla ya Vitambulisho vya Taifa 21,526,585 vilizalishwa, sawa na asilimia 92.2 ya namba za utambulisho 23,344,265 zilizotolewa, huku vitambulisho 20,935,351 vikiwa vimegawiwa kwa wananchi, sawa na asilimia 97.2 ya vitambulisho vilivyozalishwa. Msigwa anasema mfumo wa utambulisho umeleta manufaa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kusaidia taasisi zinazohusika na usalama kudhibiti uhalifu, kupunguza udanganyifu, kudhibiti utakatishaji fedha na kufuatilia shughuli mbalimbali zinazohitaji uthibitisho wa utambulisho wa mtu. Anasema pia matumizi ya Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) yamewezesha usajili wa laini za simu 92,735,799, hatua inayosaidia kupunguza udanganyifu na kuimarisha usalama katika mfumo wa mawasiliano, huku mfumo huo ukiwezesha wananchi, wakiwemo wazee, wanawake na vijana, kufungua akaunti na kupata huduma za kifedha na mikopo. Utambulisho pia umewezesha wananchi kutambuliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na kupata huduma za matibabu kwa urahisi, wanafunzi wa elimu ya juu kupata mikopo na kuiwasilisha kwa urahisi, pamoja na TASAF kuhakiki walengwa na kufanya malipo kwa ufanisi zaidi, anasema. Aidha, Msigwa amesema Serikali inaendelea na mpango wa kufanya maboresho katika mfumo wa Vitambulisho vya Taifa, hususan katika teknolojia ya uzalishaji na uchapishaji wa vitambulisho, baada ya kupokea maoni kutoka kwa wadau na kubaini umuhimu wa kuendana na teknolojia za kisasa. Anasema miongoni mwa maboresho yanayotarajiwa ni kuhamia kutoka teknolojia inayotumika sasa kwenda teknolojia inayotumia mionzi katika uchapishaji wa Vitambulisho vya Taifa, hatua inayolenga kuongeza ubora na usalama wa vitambulisho hivyo. Pamoja na hayo Msigwa, amesema Serikali inalenga kufanya Kitambulisho cha Taifa kuwa nyenzo pana zaidi ya utambulisho kwa kuunganisha taarifa muhimu za huduma anazopata mwananchi. Kadi ya Kitambulisho cha Taifa itabeba taarifa za utambulisho wa mtu pamoja na taarifa muhimu za huduma, zikiwemo bima ya afya na leseni ya udereva, anasema Msigwa. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uzalishaji Vitambulisho wa NIDA, Edson Guyai, amefafanua matumizi ya Kitambulisho cha Taifa cha NIDA na Kitambulisho cha Mkazi Zanzibar (ZAN ID), akisema NIDA ni taasisi ya Muungano hivyo Kitambulisho cha Taifa hutumika kumtambua mwananchi akiwa Tanzania Bara au Zanzibar. NIDA ni taasisi ya Muungano, Kwa hiyo, huduma zote za Muungano Kitambulisho cha Taifa cha NIDA hutumika kumtambua mwananchi akiwa Zanzibar au Tanzania Bara, Hata hivyo, kuna huduma ambazo ni mahsusi kwa Zanzibar, hivyo katika huduma hizo hutumika Kitambulisho cha Mkazi Zanzibar, amesema Guyai. Guyai anawataka wananchi ambao Vitambulisho vyao vya Taifa vimekamilika, wanaokadiriwa kufikia milioni 1.5, kwenda kuvichukua katika vituo husika ili waanze kuvitumia kupata huduma mbalimbali, Anasema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wananufaika kikamilifu na mfumo wa utambulisho wa taifa. Kwa ujumla, Mfumo huu, ambao umeanza kama njia ya kumtambua mtu, sasa unaendelea kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo, usalama, uchumi na utoaji wa huduma, huku Serikali ikiendelea kuboresha teknolojia ili kuhakikisha kila mwananchi anatambulika na anapata huduma kwa ufanisi.
Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na wazalishaji wa saruji nchini kutafuta suluhu ya haraka ya kurejesha bei ya saruji katika viwango vinavyomudu wananchi. Makamu wa Rais ametoa agizo hilo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya 19 ya Tuzo za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani, iliyofanyika katika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam. Amesema maono ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa muhimu kwa gharama nafuu, hivyo ni muhimu kuoanisha uzalishaji na upatikanaji wa malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa saruji ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama. Aidha, Makamu wa Rais ameitaka Serikali kufanya tathmini ya ukuaji wa sekta ya viwanda nchini ili kubaini iwapo viwanda vilivyopo vina uwezo wa kushindana katika masoko ya kikanda, Afrika na kimataifa. Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wafanyabiashara wanaojihusisha na uingizaji wa bidhaa bandia na biashara haramu zinazokwepa kodi na tozo, akieleza kuwa vitendo hivyo vinaathiri viwanda vya ndani, mapato ya Serikali na ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini. Makamu wa Rais amewataka wazalishaji kuongeza uchakataji wa malighafi ndani ya nchi na kuongeza thamani ya bidhaa, hatua itakayoongeza ajira, mapato na kuchochea ukuaji wa uchumi. Pia ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakiki takwimu za idadi ya viwanda vilivyopo nchini ili kuweka mikakati ya kuimarisha uwakilishi wa wazalishaji kupitia Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI). Amesema sekta ya viwanda ni mhimili muhimu wa maendeleo kwa kuwa inaongeza thamani ya malighafi, inazalisha ajira, inaongeza mapato ya Serikali na fedha za kigeni, huku ikichochea sayansi, teknolojia, ubunifu na uvumbuzi. Kwa kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi ikiwemo misitu na madini, ni muhimu kuendelea kukuza sekta ya viwanda na kujenga uhusiano madhubuti kati ya viwanda na sekta nyingine ili kuongeza ufanisi na kipato cha Watanzania. Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema Wizara inaendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa. Amesema Wizara imekamilisha Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 pamoja na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Mwaka 2003, Toleo la 2025, zinazolenga kwenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Hussein Suphian Ally, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kiuchumi ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), bandari, barabara na nishati, akisema miradi hiyo imepunguza gharama za usafirishaji na kurahisisha biashara. Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitunukiwa Tuzo ya Heshima kwa kutambua mchango wake katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na maendeleo ya sekta ya viwanda nchini. Hafla hiyo imewakutanisha wazalishaji wakubwa, wa kati na wadogo, wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa sekta ya viwanda na biashara, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ubora, ubunifu, uwekezaji, matumizi ya teknolojia na uzalishaji endelevu nchini.
Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Katika miji inayokua kwa kasi, biashara ndogo ndogo zimekuwa sehemu muhimu ya maisha ya wananchi. Kwa maelfu ya Watanzania, biashara hizo ni chanzo cha ajira, kipato na mahitaji ya kila siku ya familia. Hata hivyo, ukuaji wa shughuli hizo unahitaji usimamizi wenye mipango unaozingatia maslahi ya wafanyabiashara, wananchi na ustawi wa miji. Ni kwa kuzingatia umuhimu huo ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Wakuu wa Mikoa kusimamia kwa umakini suala la wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga, akieleza kuwa wameanza kurejea kwa kasi katika maeneo yaliyotengwa kwa wafanyabiashara wakubwa. Rais Samia ametoa kauli hiyo Septemba 2, 2026, katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa. Amesema suala la wafanyabiashara wadogo lilikuwa likisimamiwa vizuri, lakini kwa sasa kumekuwa na kulegalega katika utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao katika maeneo yaliyopangwa. Suala la wafanyabiashara wadogo wadogo, tulikuwa tunalisimamia vizuri, lakini kwa sasa tumepunguza usimamizi hasa katika Majiji ya Mwanza, Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Dodoma, amesema Rais Samia. Kwa Rais Samia, changamoto ya Machinga kurejea katika maeneo ya wafanyabiashara wakubwa haiwezi kutatuliwa kwa kutumia nguvu au kuwaondoa bila kuwa na mpango mbadala. Amesisitiza umuhimu wa viongozi kuweka mipango mizuri itakayowawezesha wafanyabiashara hao kuendelea na shughuli zao katika maeneo salama na yaliyopangwa. Si kwa kuwapiga fimbo au kuwapeleka Askari Mgambo kwenda kuwanyang’anya vitu vyao na kuwapiga mateke, tuwapangie mipango mizuri, watoke walipo na warudi kwenye masoko, ameagiza. Kauli hiyo inaweka msisitizo kwenye matumizi ya mipango badala ya nguvu, ili kutatua changamoto ya wafanyabiashara wadogo kwa njia inayolinda utu wao na wakati huo huo kuhakikisha miji inakuwa na mpangilio unaokubalika. Biashara za Machinga zina nafasi kubwa katika uchumi wa wananchi kwa kuwa zinawawezesha watu wengi kujiajiri na kupata kipato bila kutegemea ajira rasmi. Kwa baadhi ya wananchi, biashara hizi ni hatua ya kwanza ya kujenga mtaji, kukuza biashara na hatimaye kuingia katika shughuli kubwa zaidi za kiuchumi. Hivyo, usimamizi wa wafanyabiashara hao unahitaji kuangalia zaidi namna ya kuwawezesha kukua kuliko kuwaona kama tatizo linalopaswa kuondolewa katika maeneo ya mijini. Mipango mizuri ya upangaji wa maeneo ya biashara inaweza kuwasaidia Machinga kupata maeneo yenye wateja, mazingira salama na huduma muhimu, huku ikisaidia pia kupunguza msongamano na migongano kati ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa. Maelekezo ya Rais Samia kwa viongozi ya kuwarudisha wafanyabiashara wadogo katika masoko yanapaswa kutafsiriwa kama wito wa kuhakikisha maeneo hayo yana mazingira yanayoweza kuwawezesha kufanya biashara kwa tija. Soko lenye mpangilio mzuri, usalama, usafi na mazingira rafiki kwa biashara linaweza kuwa zaidi ya sehemu ya kuuza bidhaa; linaweza kuwa kichocheo cha maendeleo ya wafanyabiashara na wananchi wanaotegemea huduma zao. Kwa mtazamo huo, kuwaondoa Machinga katika maeneo yasiyofaa kunapaswa kuambatana na kuwaandalia maeneo mbadala yenye uwezo wa kuwasaidia kuendelea kujipatia kipato. Ujumbe wa Rais Samia pia unawakumbusha viongozi kuwa utekelezaji wa sheria na mipango ya miji unapaswa kwenda sambamba na kuheshimu utu wa wananchi. Wafanyabiashara wadogo wanapaswa kupewa maelekezo yanayoeleweka, kushirikishwa katika mipango inayowahusu na kupewa muda na mazingira yanayowawezesha kuhamia katika maeneo yaliyopangwa. Kwa kufanya hivyo, Serikali inaweza kufikia malengo mawili kwa wakati mmoja: kuweka miji katika mpangilio unaotakiwa na kulinda fursa za kiuchumi za wananchi. Maelekezo ya Rais Samia yanaibua umuhimu wa kutafuta uwiano kati ya maendeleo ya miji na mahitaji ya wananchi wanaotegemea biashara ndogo ndogo. Miji inahitaji kuwa na maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya biashara mbalimbali, huku wafanyabiashara nao wakihitaji mazingira yatakayowawezesha kufanya biashara bila kuvunja taratibu zilizowekwa. Hivyo, suluhisho la changamoto ya Machinga si kuwafukuza kutoka eneo moja kwenda jingine, bali ni kuwa na mpango endelevu wa upangaji, ugawaji wa maeneo na usimamizi wa biashara ndogo ndogo. Kwa kufanya hivyo, biashara ndogo zinaweza kuendelea kuwa chanzo muhimu cha ajira na kipato kwa wananchi, huku miji ikiendelea kuwa safi, salama na yenye mpangilio. Hatua hiyo pia itaimarisha uhusiano kati ya Serikali na wafanyabiashara wadogo kwa kujenga mazingira ambayo wananchi wanaona kuwa mipango ya Serikali inalenga kuwawezesha, badala ya kuwazuia kujitafutia maisha. Ujumbe wa Rais Samia ni kwamba Machinga wanahitaji kupangwa na kuwezeshwa, si kubughudhiwa Wanahitaji maeneo yanayofaa kwa biashara, viongozi wenye mipango na utekelezaji unaozingatia utu.
Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi aliowateua hivi karibuni, wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, kutanguliza maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha wanawasikiliza, wanatatua kero zao na kutoa huduma bora kwa ufanisi. Rais Samia ametoa wito huo Septemba 2, 2026, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni, Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, akisisitiza kuwa nafasi walizopewa si fursa ya kujinufaisha, bali ni dhamana ya kuwatumikia wananchi na kulinda maslahi ya Taifa. Amewakumbusha viongozi hao kuwa wao ni watumishi wa wananchi, hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo, uadilifu na uwajibikaji, huku wakitanguliza maslahi ya Taifa mbele ya maslahi binafsi. Rais Samia amewasisitiza viongozi hao kuwa utumishi wa umma ni kuwa tayari kuwatumikia wananchi waliokupa dhamana hiyo, kwa kuweka mbele uzalendo na maslahi mapana ya nchi. Amesema viongozi wanapaswa kuwa karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuhakikisha kero zinazoweza kutatuliwa katika ngazi za mikoa na wilaya zinapatiwa majibu na hatua stahiki kwa wakati. Amesema uongozi wa aina hiyo utasaidia kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali na kuhakikisha huduma za umma zinawafikia walengwa kwa wakati na kwa ufanisi. Aidha, amesisitiza kuwa wananchi hawahitaji viongozi wanaosubiri kero zifikishwe ofisini pekee bali wanahitaji viongozi wanaokwenda kwao, kusikiliza changamoto zao, kutafuta suluhisho na kusimamia utekelezaji ili matokeo yaonekane.
Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imefanikiwa kuokoa fedha za Serikali takribani Shilingi bilioni 121.99 ambazo zingetumika kwa matibabu nje ya nchi, baada ya kuwapatia wagonjwa 2,282 huduma za ubingwa na ubingwa bobezi katika mwaka wa fedha 2025/26. Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, Taasisi hiyo ilihudumia jumla ya wagonjwa 211,359, wakiwemo wagonjwa 202,000 wa nje na 9,359 waliolazwa. Amesema kuimarishwa kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa, kumeiwezesha MOI kupunguza rufaa za wagonjwa wa mifupa kwa asilimia 98 na wagonjwa wa ubongo kwa asilimia 97. Huduma zilizoboreshwa ni pamoja na upasuaji wa ubongo kwa teknolojia za kisasa, upasuaji kupitia matundu, tiba ya maumivu, upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu, huduma za kiharusi, pamoja na upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo kupitia tundu la pua. Katika huduma za ubingwa bobezi, wagonjwa 2,282 walipatiwa matibabu yakiwemo upasuaji wa nyonga, upandikizaji wa goti bandia, upasuaji wa hydrocephalus na scoliosis, hatua iliyosaidia kupunguza utegemezi wa matibabu nje ya nchi na kuokoa fedha za Serikali. Aidha, amesema MOI imeendelea kuchangia ukuaji wa tiba utalii nchini, ambapo katika mwaka huo ilihudumia wagonjwa 270 kutoka Comoro, Msumbiji, Malawi, Zambia, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda, Burundi, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Balozi Dkt. Ulisubisya amesema uwepo wa wataalamu wenye uzoefu, vifaa tiba vya kisasa na mifumo bora ya utoaji huduma umeifanya MOI kuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa kutoka ndani na nje ya Tanzania. Katika kuimarisha ubora wa huduma, asilimia 87.5 ya wagonjwa waliridhishwa na huduma walizopata, huku kiwango cha kuridhika kwa watumishi kikifikia asilimia 82 na ushughulikiaji wa malalamiko kufikia asilimia 90. Aidha, katika kipindi hicho MOI ilifanya vipimo 83,847 vya radiolojia, ikiwemo MRI 11,533, CT Scan 6,796 na X-Ray 53,384, huku wagonjwa 71,819 wakipatiwa huduma za tiba kwa mazoezi (fiziotherapia). Taasisi hiyo pia imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia huduma mkoba, zilizowafikia wagonjwa 18,455, ambapo 4,310 walifanyiwa upasuaji. Mafanikio hayo yamekwenda sambamba na utekelezaji wa miradi ya kuboresha miundombinu, ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la OPD lenye thamani ya Shilingi bilioni 13.8, ukarabati wa MOI Annex, maboresho ya vyumba 25 vya kisasa vya kulaza wagonjwa, ukarabati wa ICU ya watoto pamoja na ujenzi wa tenki la Hewa Tiba ya Oksijeni lenye ujazo wa tani 10. Kuhusu mipango ya baadaye ya taasisi hiyo, Dkt. Ulisubisya amesema MOI itaendelea kuboresha huduma kwa viwango vya kimataifa, kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kuanzisha huduma mpya za kibingwa na ubingwa bobezi kwa kutumia teknolojia za kisasa. Amesema pia Taasisi hiyo inaendelea kujiandaa kutoa huduma za afya kwa wanamichezo na wadau wengine wakati wa michuano ya AFCON 2027.
Na. Baraka Messa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzania kuilinda na kuitunza miundombinu ya Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHP), akisema kuwa mradi huo ni mali ya Watanzania na urithi muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Rais Samia amesema hayo Agosti 22, 2026, wilayani Rufiji mkoani Pwani, wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Uzalishaji wa Umeme cha Julius Nyerere chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115. Amesema kuwa Serikali imewekeza rasilimali kubwa katika utekelezaji wa mradi huo kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme na kuweka msingi wa maendeleo ya viwanda, uchumi na ustawi wa wananchi na kusisitiza kuwa jukumu la kulinda mradi huo si la Serikali pekee, bali ni la kila Mtanzania, kutokana na umuhimu wake katika maendeleo ya Taifa. Mradi huu ni wetu sote, Ni lazima tuulinde, tuutunze na tuhakikishe unaendelea kutoa manufaa kwa Watanzania wa leo na vizazi vijavyo,” amesema Rais Samia. Ameongeza kuwa Mradi wa JNHP ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya nishati nchini, hivyo akawataka wananchi kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika katika kulinda miundombinu ya mradi huo. Kituo cha Uzalishaji wa Umeme cha Julius Nyerere chenye uwezo wa megawati 2,115 kinatarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini na kuimarisha upatikanaji wa nishati kwa matumizi ya majumbani, viwandani na katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratus Ndejembi amebainisha kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Taifa. Aidha, uzinduzi wa kituo hicho unafungua sura mpya katika safari ya Tanzania ya kuimarisha usalama wa nishati, huku Serikali ikiendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuwa washiriki wakuu katika kulinda na kunufaika na miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini.