Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Serikali Yaahidi Kuendelea Kuwekeza Sekta ya Nishati Kukuza Uchumi

October 2, 2026

Na Scolastica Sambi – MAELEZO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Deogratius Ndejembi amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya nishati kwa kuongeza uzalishaji, kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kupanua usambazaji wa umeme, hatua inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi.

Akizungumza Oktoba 2, 2026, jijini Dar es Salaam, katika hafla ya utiaji saini mkataba na uzinduzi wa mpango wa uunganishaji wa umeme kwa wananchi kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya CRDB, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, , amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha umeme unawafikia wananchi kwa uhakika na kwa urahisi zaidi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi akihutubia wakati wa hafla ya utiaji Saini Mkataba wa Uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi, kati ya Benki ya CRDB na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Tarehe 02 Oktoba 2026.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji wa umeme ni kukamilika na kuanza kuzalisha kwa Bwawa la Julius Nyerere, lililopo katika Mto Rufiji, lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115. Amesema ongezeko la uzalishaji linaenda sambamba na uwekezaji katika miundombinu ya usafirishaji na usambazaji ili umeme uwafikie walaji wa mwisho.

Mhe. Ndejembi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya umeme nchini, ikiwemo jijini Dar es Salaam ambako zaidi ya Shilingi bilioni 231 zimetengwa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kuimarisha huduma hiyo.

Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa vituo vikubwa vya kusambaza umeme, ikiwemo Dege na Mabibo, pamoja na ujenzi wa njia mpya za kusafirisha umeme kutoka Kinyerezi, Kimara, Ilala, Ubungo na Ununio, hatua inayolenga kuongeza uwezo na uhakika wa huduma ya umeme jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kuhusu mwelekeo wa muda mrefu, Makamu wa Rais amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeipa sekta ya nishati nafasi muhimu katika kujenga uchumi wa kisasa unaozingatia tija, ushindani, ubunifu na matumizi ya teknolojia. Tanzania inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji hadi megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 na megawati 74,000 ifikapo mwaka 2050.

Viongozi, wadau na wananchi mbalimbali wakishiriki katika hafla ya utiaji Saini Mkataba wa Uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi, kati ya Benki ya CRDB na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere(JNICC) Jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi. Tarehe 02 Oktoba 2026.

Aidha, amesema Tanzania inaendelea kushiriki katika juhudi za kimataifa za kuongeza upatikanaji wa umeme barani Afrika kupitia ‘Mission 300’, unaolenga kuwaunganisha takribani watu milioni 300 barani Afrika na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030. Tanzania pia iliandaa Mkutano wa Africa Energy Summit – Mission 300 jijini Dar es Salaam mwaka 2025.

Mhe. Ndejembi ameipongeza TANESCO kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kuongeza upatikanaji na uhakika wa umeme, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi zake na sekta binafsi katika kuharakisha uwekezaji wa nishati.

Amesema umeme unaofikishwa kwa wananchi unapaswa kuwa kichocheo cha maendeleo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo elimu, uzalishaji, biashara, teknolojia na shughuli nyingine za kiuchumi, hivyo jitihada za kuongeza uzalishaji zinapaswa kwenda sambamba na kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi kwa ufanisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *