Makamu wa Rais Asisitiza Uwekezaji Katika Miundombinu Bora Kupunguza Upotevu wa Mazao
Na Scolastica Sambi – MAELEZO
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu ya ukusanyaji, uhifadhi na usafirishaji wa mazao ili kupunguza upotevu baada ya mavuno na kuongeza kipato cha wakulima nchini.
Akizungumza Novemba 9, 2026, jijini Arusha, wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonyesho ya Kimataifa ya Horticultural Logistics Africa 2026, amesema wakulima wamekuwa wakifanya juhudi kubwa kuongeza uzalishaji, lakini sehemu ya mazao yao hupotea kutokana na uhaba wa miundombinu na mifumo bora ya kuyahifadhi na kuyasafirisha.
Ametoa mfano wa wakulima wa mananasi katika mikoa ya Tanga, Arusha na Morogoro, ambao baadhi yao hulazimika kuuza mazao yao kando ya barabara, huku mengine yakiharibika kwa kukosa mifumo madhubuti ya ukusanyaji na uhifadhi. Hali kama hiyo pia inawakabili wakulima wa parachichi katika mikoa ya Njombe, Mbeya na Manyara.
Tunazalisha sana, wakulima wetu wanajitoa sana, lakini tunapoteza zao lile ambalo tunazalisha,” amesema Makamu wa Rais, akisisitiza umuhimu wa kujenga vituo vya kisasa vya ukusanyaji wa mazao, maghala ya kuhifadhi, mifumo ya ubaridi na kuboresha usafirishaji.
Amesema uwekezaji katika maeneo hayo utapunguza hasara kwa wakulima, kuongeza thamani ya mazao na kuhakikisha bidhaa zinafika sokoni kwa wakati na katika ubora unaohitajika.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwaunganisha wakulima na wanunuzi kupitia mikataba ya uzalishaji na ununuzi wa mazao ili kuhakikisha shughuli za kilimo zinaendana na mahitaji halisi ya soko.
Makamu wa Rais, amebainisha kuwa uzalishaji wa mazao ya bustani nchini umeongezeka kutoka tani milioni 8.4 mwaka 2023 hadi tani milioni 9.7 mwaka 2025, sawa na ukuaji wa asilimia 15.9.
Hata hivyo, amesema ongezeko hilo la uzalishaji linapaswa kwenda sambamba na uwekezaji katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya bustani ili kuongeza kipato cha wakulima, kutengeneza ajira na kukuza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.