Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Tumejenga Mji wa Serikali Dodoma Kusogeza Huduma Kwa Wananchi – Rais Samia

October 30, 2026

Na Baraka Messa – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kusogeza huduma karibu na wananchi, kurahisisha upatikanaji wake na kuhakikisha huduma za umma zinapatikana kwa ufanisi na usawa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Amesema hatua hiyo inaendeleza maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyetangaza mwaka 1973 uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma, kwa lengo la kuimarisha uwiano wa maendeleo na kusogeza shughuli za Serikali karibu zaidi na wananchi.

Rais Samia ameyasema hayo Oktoba 30, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo ya wizara na taasisi za Serikali pamoja na barabara zilizojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, iliyohudhuriwa pia na Rais wa Jamhuri ya Angola, João Lourenço.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akikata utepe pamoja na mgeni wake Mhe. João Manuel Conçalves Lourenço, Rais wa Jamhuri ya Angola kuashiria ufunguzi wa Majengo ya Ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Amesisitiza kuwa ujenzi wa majengo ya kisasa pekee hautoshi kutimiza azma ya Serikali, bali unapaswa kwenda sambamba na utoaji wa huduma bora, kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili taasisi za Serikali ziwasiliane kwa ufanisi, kupunguza urasimu na kurahisisha huduma kwa wananchi.

Aidha, amewataka watumishi wa umma kutunza majengo na miundombinu iliyojengwa, kuyatumia kwa ufanisi na kuhakikisha yanakuwa mazingira bora ya kufanyia kazi na kuhudumia wananchi. Ameeleza pia kuwa ukuaji wa Dodoma unahitaji mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi na maendeleo ya mji ili kuendana na hadhi yake kama makao makuu ya nchi.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameeleza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Angola, akibainisha kuwa uamuzi wa kuipa barabara moja ya Mji wa Serikali jina la Rais wa kwanza wa Angola, Agostinho Neto, ni ishara ya kuthamini mchango wa viongozi wa mataifa hayo katika historia ya ukombozi wa Afrika.

Muonekano wa baadhi ya majengo ya Ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na Barabara katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Kwa upande wake, Rais wa Angola, João Lourenço, ameishukuru Tanzania kwa mchango wake katika harakati za ukombozi wa Angola na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo, hususan katika sekta za usafiri wa anga na reli.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema utekelezaji wa mradi wa Mji wa Serikali ulianza mwaka 2016 katika Awamu ya Tano ya Serikali na kugharamiwa kwa kutumia fedha za ndani, hatua inayoonesha dhamira ya nchi katika kuwekeza kwenye miundombinu ya umma na maendeleo ya taifa.

Kwa ujumla, Mji wa Serikali Mtumba ni zaidi ya mkusanyiko wa majengo ya wizara na taasisi za umma; ni hatua muhimu katika kutekeleza azma ya kuifanya Serikali iwe karibu zaidi na wananchi. Mafanikio yake yatapimwa kwa namna miundombinu hiyo itakavyotumika kuboresha huduma, kupunguza gharama na muda wa kuzifikia, pamoja na kuongeza ufanisi wa utendaji wa Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *