Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Rais Samia Azindua Ramani ya Bara la Afrika ya Kupunguza Vifo vya Mama na Watoto

November 23, 2026

Na Sidi Mgumia, MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua Ramani ya Utekelezaji ya Umoja wa Afrika (AU) ya mwaka 2026–2030, inayolenga kuimarisha afya ya uzazi, mama, watoto wachanga, watoto na vijana, huku akizitaka nchi za Afrika kuongeza uwekezaji, uwajibikaji na juhudi za pamoja katika kukabiliana na vifo vinavyoweza kuzuilika.

Akizungumza leo, Novemba 23, 2026, katika Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Afrika unaofanyika Addis Ababa, Ethiopia, Rais Samia amesema usalama na uhuru wa Afrika katika sekta ya afya unahitaji uongozi imara wa kisiasa, mifumo bora ya utawala, ufadhili endelevu na umiliki wa vipaumbele vya afya na nchi zenyewe.

Rais Samia amesema takwimu za mwaka 2023 zinaonesha kuwa takribani wanawake 180,000 walifariki kutokana na sababu zinazohusiana na uzazi barani Afrika, huku watoto wachanga milioni 1.18 wakipoteza maisha katika kipindi hicho.

Kwa wastani, Afrika inapoteza mwanamke mmoja kila baada ya dakika tatu kutokana na sababu zinazohusiana na uzazi, na watoto wachanga zaidi ya wawili kila dakika. Iwapo hali hiyo itaendelea, bara hili linaweza kuwa na vifo vya wajawazito 300 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030, kiwango ambacho ni cha juu ikilinganishwa na lengo la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) la kupunguza vifo hivyo hadi chini ya 70.

Amesema ramani hiyo imejengwa katika malengo makuu matatu yanayofahamika kama Three Zeros. Malengo hayo ni kuhakikisha hakuna mama anayejifungulia nyumbani kwa kuwezesha kila mama kupata huduma salama katika kituo cha afya chenye wataalamu; kutokuwepo kwa vifo vya mama na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika kupitia huduma bora za afya na mifumo ya uwajibikaji; pamoja na kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo muhimu zinazookoa maisha, hususan watoto wanaoishi katika maeneo ya pembezoni na yasiyofikika kwa urahisi.

Ameongeza kuwa malengo hayo yatawezesha nchi za Afrika kuratibu hatua za pamoja na kuimarisha mifumo iliyopo ya utoaji wa huduma za afya.

Akizungumzia maandalizi ya ramani hiyo, Rais Samia amesema imeandaliwa kupitia mashauriano na viongozi wa kisiasa pamoja na wataalamu katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa. Ameeleza kuwa katika Mkutano Maalumu wa Umoja wa Afrika kuhusu Afya uliofanyika Accra, Ghana, Julai mwaka huu, pamoja na mkutano wa pembeni wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika Septemba 2026, viongozi wa Afrika walisisitiza umuhimu wa ufadhili endelevu na uhuru wa bara katika sekta ya afya.

Aidha, ametaja Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) uliofanyika Arusha, Tanzania, Oktoba 2026, ambapo wabunge na wadau wapatao 300 walijadili masuala ya ufadhili, utungaji wa sheria na usimamizi wa huduma za afya ya mama na mtoto.

Tanzania imepiga hatua katika kupunguza vifo vya wajawazito kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2019 hadi 104 mwaka 2023, huku takwimu za utafiti wa hivi karibuni zikionesha kuwa vifo hivyo vimepungua zaidi hadi takribani 75 kwa kila vizazi hai 100,000.

Amesisitiza kuwa mafanikio hayo yaliifanya Tanzania kutambuliwa na taasisi ya Gates Foundation mwaka 2022 na 2023, jambo lililochochea juhudi zaidi za kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto. Pia ameeleza kuwa mafanikio hayo yataoneshwa kupitia filamu fupi inayoelezea safari ya Tanzania katika kuimarisha usalama na uhuru wa afya.

Aidha, Rais Samia ametangaza kutolewa kwa nafasi 60 za ufadhili wa masomo kwa nchi za Afrika kwa ajili ya mafunzo ya kitaalamu na ya juu katika fani za ukunga, usingizi wa kitabibu, uzazi na magonjwa ya wanawake, pamoja na huduma za watoto wachanga.

Amesema mafunzo hayo yataambatana na kozi fupi za kuongeza ujuzi na mafunzo kwa vitendo chini ya usimamizi wa wataalamu, kwa lengo la kuimarisha huduma za uzazi salama, kukabiliana na dharura za uzazi na kuboresha huduma muhimu kwa watoto wachanga. Amewahimiza nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kuteua waratibu wenye mamlaka na kujumuisha malengo matatu ya ramani hiyo katika mikakati yao ya kitaifa.

Rais Samia pia amewapongeza viongozi mbalimbali wa Afrika kwa juhudi zao katika kuimarisha afya, lishe na ustawi wa wananchi, akiwataja Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dkt. Abiy Ahmed Ali, kupitia mpango wa Yele Maternal na Azimio la Seqota, pamoja na viongozi wa Ghana, Afrika Kusini, Nigeria, Kenya, Sierra Leone na Burundi.

Aidha, ametoa shukrani kwa Umoja wa Afrika, Africa CDC, UNFPA, WHO, UNICEF, Gavi, Global Fund, Gates Foundation na wadau wengine kwa mchango wao katika kufanikisha maandalizi na utekelezaji wa ramani hiyo. Ameeleza kuwa ofisi yake, kwa kushirikiana na Africa CDC, itaendesha mazungumzo ya ngazi ya juu Novemba 24, 2026, jijini Addis Ababa, ili kuweka mikakati ya utekelezaji wa ramani hiyo.

Rais Samia amesema mafanikio ya ramani hiyo yatapimwa kwa maisha ya mama atakayeokolewa wakati wa kujifungua, mtoto mchanga atakayepata mwanzo salama wa maisha na kila mtoto atakayepata huduma muhimu za afya.

Ametoa wito kwa viongozi na wadau wa Afrika kuongeza juhudi za kuhakikisha kila mama anajifungua salama na watoto wanakuwa na afya bora. Akisisitiza ujumbe huo kwa kutumia kaulimbiu ya Kiswahili, “Jiongeze tuwavushe salama,” amesema Afrika inapaswa kuongeza juhudi katika kulinda afya ya mama na mtoto ili kujenga kizazi chenye afya na mustakabali bora wa bara hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *