Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Hadhi ya Mji Isiwe Kikwazo cha Umeme Shilingi 27,000

October 16, 2026

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendelea kuwaunganishia umeme kwa gharama ya Shilingi 27,000 wananchi wa maeneo yaliyopandishwa hadhi kuwa miji midogo lakini bado yana mazingira ya vijijini, ili waendelee kunufaika na huduma hiyo kwa gharama nafuu.

Akizungumza na wananchi mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, Oktoba 16, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja, Dkt. Mwigulu amesema kupandishwa kwa hadhi ya eneo kuwa mji mdogo hakumaanishi kuwa uwezo wa kiuchumi wa wananchi umeongezeka, hivyo gharama za kuunganishiwa umeme zinapaswa kuzingatia hali halisi ya maisha yao.

Wananchi hawa wanaoitwa mji mdogo, niwaelekeze watu wa TANESCO, umeme waendelee kuunganishiwa kwa 27,000 ile ile ya kijijini.

Kuhusu hadhi ya Bagamoyo, Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi kuwa hati ya kurasimisha hadhi hiyo itapatikana wiki ijayo, akieleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari amefanya uamuzi na kilichobaki ni kukamilisha taratibu.

Katika kushughulikia kero za ardhi, amemwagiza Kamishna wa Ardhi kuongoza mwenyewe kliniki maalumu ya kusikiliza na kutatua migogoro ya wananchi wa Bagamoyo kuanzia Jumatatu inayofuata, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka makao makuu, mkoa na ofisi husika za Serikali kwa muda wa wiki nzima.

Usitume mwakilishi, uje mwenyewe kusikiliza mtu mmoja mmoja wewe mwenyewe.

Amesema migogoro ya ardhi inaweza kuhatarisha undugu na mshikamano wa wananchi. Ameeleza kuwa tayari amewaelekeza Waziri wa Ardhi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri anayesimamia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia upya utaratibu wa kutatua migogoro hiyo. Pia, amesisitiza wananchi wanaopisha uwekezaji na miradi ya maendeleo kulipwa fidia stahiki bila kupunjwa.

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na Wananchi wa Bagamoyo katika Viwanja wa Shule ya Msingi Majengo vilivyopo mkoani Pwani.

Katika sekta ya afya, Waziri Mkuu amekataza kutozwa kwa wananchi gharama za mafuta ya magari ya kubebea wagonjwa wanaopelekwa hospitali za rufaa, akizitaka mamlaka husika kuhakikisha magari hayo yana mafuta ya kutosha na yanatoa huduma kwa wakati. Aidha, amesisitiza utekelezaji wa maelekezo ya Rais ya kutokuzuia miili ya marehemu hospitalini kwa sababu ya madai ya malipo.

Vilevile, ameelekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia ununuzi, usambazaji na matumizi ya dawa za Serikali ili kuhakikisha zinawafikia wananchi waliokusudiwa.

Akizungumzia uchumi na ajira, Dkt. Mwigulu amesema sekta binafsi imara na viwanda vya kuchakata mazao ni muhimu katika kuongeza ajira na kipato cha wananchi. Amewahimiza kutumia fursa za uwekezaji na uzalishaji, huku wakizingatia matumizi bora ya ardhi na sheria za nchi.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *