Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Tume ya Haki za Binadamu Kuimarisha Usimamizi wa Haki na Utawala Bora

November 2, 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuimarisha usimamizi wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini kwa kuongeza ufuatiliaji wa masuala yanayohusu haki za wananchi badala ya kutegemea malalamiko pekee.

Akizungumza Novemba 2, 2026, alipokuwa akiwaapisha viongozi wateule katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Mhe. Rais amesema Tume hiyo inapaswa kuwa na utaratibu wa kubaini na kufuatilia changamoto za ukiukwaji wa haki za binadamu katika taasisi na sekta mbalimbali na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa.

Amesema Tume hiyo pia inapaswa kufuatilia tuhuma na shutuma zinazoikabili Tanzania kuhusu haki za binadamu katika majukwaa ya kimataifa na kutoa majibu kwa kuzingatia ukweli na hali halisi ya ndani ya nchi.

Nawaambieni sana ninyi vijana, mna uwezo wa kuperuzi mitandao yote na kuona yanayotokea duniani, mkaona shutuma tunazopewa na mkaweza kuzijibu.

Ameongeza kuwa jukumu la Tume hiyo halipaswi kuishia katika kupokea malalamiko ya wananchi, bali pia kufuatilia maeneo ambayo kuna viashiria vya ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili kuhakikisha haki zinalindwa.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais amewataka viongozi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Migogoro ya Wafanyakazi kusimamia haki za wafanyakazi na waajiri kwa kuzingatia sheria, akisisitiza kuwa maamuzi yao yanapaswa kutolewa bila chuki, hila wala upendeleo. Amesema ukuaji wa uwekezaji na shughuli za sekta binafsi unaweza kuongeza migogoro ya kikazi, hivyo wanapaswa kujiandaa kukabiliana nayo kwa weledi.

Miongoni mwa viongozi walioapishwa ni Bw. Dunford George Mpelumbe, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; Bw. Omar Ali Omar, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo; Bi. Angeline Lubala Mabula, Mkuu wa Mkoa wa Tabora; pamoja na Jaji Mstaafu Wilfred Peter Dyansobera, Mwenyekiti wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Migogoro ya Wafanyakazi, na makamishna wa Tume hiyo.

Mhe. Rais amewapongeza viongozi wote walioapishwa na kuwatakia mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa Serikali ina matarajio makubwa ya kuona wanatekeleza dhamana walizopewa kwa uadilifu na kuzingatia maslahi ya wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *