Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Mwandishi Wetu – Geneva, Uswisi Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza na kulinda utu na haki za binadamu kwa watu wote, huku ikiendelea kuweka upatikanaji wa haki na huduma muhimu kwa wananchi kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Serikali. Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Ulega, amesema hayo Novemba 5, 2026, wakati akiwasilisha hotuba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika awamu ya nne ya Mapitio ya Kimataifa ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR), mbele ya Kikundi Kazi cha UPR katika kikao chake cha 53 kinachoendelea jijini Geneva, Uswisi, kuanzia Novemba 2 hadi 13, 2026. Mhe. Ulega amesema Tanzania inajivunia kushiriki katika awamu hiyo ya mapitio, huku akieleza hatua zilizopigwa katika kuimarisha haki za kiraia na kisiasa, ushiriki wa kidemokrasia, uhuru wa msingi na upatikanaji wa haki. Ameeleza kuwa, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, juhudi za kuimarisha haki za binadamu zimeongozwa na falsafa ya Misingi Minne ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Upya. Tunatambua umuhimu wa kuendelea kufanya mageuzi, kuimarisha taasisi na kuhakikisha uwajibikaji katika maeneo yote huku tukiongozwa na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 na misingi ya kutomwacha mtu yeyote nyuma. Hivyo, tunakaribisha mapendekezo yenye kujenga pamoja na ushirikiano unaozingatia kuheshimiana. Tuko tayari kusikiliza, kubadilishana uzoefu na kushirikiana na nchi wanachama katika misingi ya mazungumzo yenye kujenga na kuheshimiana. Aidha, amezitaka nchi washirika wa kimataifa kuheshimu mamlaka ya Tanzania na taratibu zake za kisheria, akisisitiza kuwa ushirikiano katika masuala ya haki za binadamu unapaswa kuzingatia mazungumzo yenye kujenga, kuheshimiana na wajibu wa pamoja wa kulinda na kuendeleza haki hizo. Akieleza hatua zilizopigwa katika kutekeleza haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, Waziri Ulega amesema Tanzania imeendelea kuwekeza katika miundombinu na huduma muhimu zinazoboresha maisha ya wananchi na kupanua fursa za maendeleo. Ametaja uwekezaji huo kuwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa ya SGR yenye urefu wa zaidi ya kilomita 700 na Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme. Ameongeza kuwa vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vimefikiwa na huduma ya umeme, huku kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini kikifikia takribani asilimia 79.5. Vilevile, uwekezaji katika sekta mbalimbali za uzalishaji umewezesha kupatikana kwa fursa za ajira zaidi ya milioni 4.2. Katika sekta ya elimu, amesema bajeti imeongezeka kutoka takribani shilingi trilioni 5.6 katika mwaka wa fedha 2022/2023 hadi shilingi trilioni 6.3 katika mwaka wa fedha 2025/2026. Ameeleza pia kuwa Serikali inaendelea kutoa elimu ya msingi bila ada na kuweka utaratibu unaowawezesha wanafunzi waliokatisha masomo kurejea shuleni, wakiwemo wasichana walioacha masomo kutokana na ujauzito. Katika sekta ya afya, idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya Tanzania Bara imeongezeka kutoka 8,458 mwaka 2022 hadi zaidi ya 10,000 mwaka 2026. Huduma za kliniki kwa wajawazito zimefikia asilimia 98, huku kiwango cha wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya kikiongezeka kutoka asilimia 83 hadi asilimia 98. Aidha, kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi kimepungua kutoka 197 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, huku vifo vya watoto wachanga vikishuka kutoka 25 hadi 19 kwa kila vizazi hai 1,000. Hatua hizo zinaonesha juhudi za Serikali katika kupanua upatikanaji wa huduma za afya, hususan kwa akina mama na watoto. Kuhusu uwezeshaji wa wanawake na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, Waziri Ulega amesema Tanzania imepiga hatua katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na umiliki wa rasilimali. Uwakilishi wa wanawake katika Bunge ulifikia asilimia 39.3 mwaka 2025, huku uwakilishi wao katika Mahakama ukifikia asilimia 36.5. Aidha, uwiano wa wanawake wenye haki za umiliki wa ardhi uliongezeka kutoka asilimia 28.5 mwaka 2020 hadi asilimia 35 mwaka 2025. Akizungumzia utekelezaji wa mapendekezo ya mapitio yaliyotangulia, amesema katika awamu ya tatu iliyofanyika mwaka 2021, Tanzania ilipokea jumla ya mapendekezo 252, ikakubali mapendekezo 187, yakiwemo 20 yaliyokubaliwa kwa sehemu, huku mapendekezo 65 yakikosa ridhaa ya Serikali. Amesema mapendekezo yaliyokubaliwa yamekuwa mwongozo katika kutekeleza mageuzi mbalimbali katika kipindi chote kilichopita, hatua inayoonesha dhamira ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kuimarisha na kulinda haki za binadamu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuimarisha usimamizi wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini kwa kuongeza ufuatiliaji wa masuala yanayohusu haki za wananchi badala ya kutegemea malalamiko pekee. Akizungumza Novemba 2, 2026, alipokuwa akiwaapisha viongozi wateule katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Mhe. Rais amesema Tume hiyo inapaswa kuwa na utaratibu wa kubaini na kufuatilia changamoto za ukiukwaji wa haki za binadamu katika taasisi na sekta mbalimbali na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa. Amesema Tume hiyo pia inapaswa kufuatilia tuhuma na shutuma zinazoikabili Tanzania kuhusu haki za binadamu katika majukwaa ya kimataifa na kutoa majibu kwa kuzingatia ukweli na hali halisi ya ndani ya nchi. Nawaambieni sana ninyi vijana, mna uwezo wa kuperuzi mitandao yote na kuona yanayotokea duniani, mkaona shutuma tunazopewa na mkaweza kuzijibu. Ameongeza kuwa jukumu la Tume hiyo halipaswi kuishia katika kupokea malalamiko ya wananchi, bali pia kufuatilia maeneo ambayo kuna viashiria vya ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili kuhakikisha haki zinalindwa. Katika hatua nyingine, Mhe. Rais amewataka viongozi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Migogoro ya Wafanyakazi kusimamia haki za wafanyakazi na waajiri kwa kuzingatia sheria, akisisitiza kuwa maamuzi yao yanapaswa kutolewa bila chuki, hila wala upendeleo. Amesema ukuaji wa uwekezaji na shughuli za sekta binafsi unaweza kuongeza migogoro ya kikazi, hivyo wanapaswa kujiandaa kukabiliana nayo kwa weledi. Miongoni mwa viongozi walioapishwa ni Bw. Dunford George Mpelumbe, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; Bw. Omar Ali Omar, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo; Bi. Angeline Lubala Mabula, Mkuu wa Mkoa wa Tabora; pamoja na Jaji Mstaafu Wilfred Peter Dyansobera, Mwenyekiti wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Migogoro ya Wafanyakazi, na makamishna wa Tume hiyo. Mhe. Rais amewapongeza viongozi wote walioapishwa na kuwatakia mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa Serikali ina matarajio makubwa ya kuona wanatekeleza dhamana walizopewa kwa uadilifu na kuzingatia maslahi ya wananchi.

Na Baraka Messa – MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kusogeza huduma karibu na wananchi, kurahisisha upatikanaji wake na kuhakikisha huduma za umma zinapatikana kwa ufanisi na usawa katika maeneo mbalimbali ya nchi. Amesema hatua hiyo inaendeleza maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyetangaza mwaka 1973 uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma, kwa lengo la kuimarisha uwiano wa maendeleo na kusogeza shughuli za Serikali karibu zaidi na wananchi. Rais Samia ameyasema hayo Oktoba 30, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo ya wizara na taasisi za Serikali pamoja na barabara zilizojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, iliyohudhuriwa pia na Rais wa Jamhuri ya Angola, João Lourenço. Amesisitiza kuwa ujenzi wa majengo ya kisasa pekee hautoshi kutimiza azma ya Serikali, bali unapaswa kwenda sambamba na utoaji wa huduma bora, kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili taasisi za Serikali ziwasiliane kwa ufanisi, kupunguza urasimu na kurahisisha huduma kwa wananchi. Aidha, amewataka watumishi wa umma kutunza majengo na miundombinu iliyojengwa, kuyatumia kwa ufanisi na kuhakikisha yanakuwa mazingira bora ya kufanyia kazi na kuhudumia wananchi. Ameeleza pia kuwa ukuaji wa Dodoma unahitaji mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi na maendeleo ya mji ili kuendana na hadhi yake kama makao makuu ya nchi. Katika hatua nyingine, Rais Samia ameeleza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Angola, akibainisha kuwa uamuzi wa kuipa barabara moja ya Mji wa Serikali jina la Rais wa kwanza wa Angola, Agostinho Neto, ni ishara ya kuthamini mchango wa viongozi wa mataifa hayo katika historia ya ukombozi wa Afrika. Kwa upande wake, Rais wa Angola, João Lourenço, ameishukuru Tanzania kwa mchango wake katika harakati za ukombozi wa Angola na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo, hususan katika sekta za usafiri wa anga na reli. Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema utekelezaji wa mradi wa Mji wa Serikali ulianza mwaka 2016 katika Awamu ya Tano ya Serikali na kugharamiwa kwa kutumia fedha za ndani, hatua inayoonesha dhamira ya nchi katika kuwekeza kwenye miundombinu ya umma na maendeleo ya taifa. Kwa ujumla, Mji wa Serikali Mtumba ni zaidi ya mkusanyiko wa majengo ya wizara na taasisi za umma; ni hatua muhimu katika kutekeleza azma ya kuifanya Serikali iwe karibu zaidi na wananchi. Mafanikio yake yatapimwa kwa namna miundombinu hiyo itakavyotumika kuboresha huduma, kupunguza gharama na muda wa kuzifikia, pamoja na kuongeza ufanisi wa utendaji wa Serikali.

Na Timothy Mwakyenda – MAELEZO Safari iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço, kwa kutumia treni ya kisasa inayotumia nishati ya umeme kupitia reli ya SGR kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma, Oktoba 30, 2026, ni hatua yenye ujumbe mpana kuhusu maendeleo ya sekta ya usafirishaji nchini Tanzania. Mbali na kuonesha kuimarika kwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, safari hiyo imeonesha uwezo wa Tanzania kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya reli na kutoa huduma za usafiri zinazokidhi mahitaji ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Viongozi hao walianza safari yao katika Stesheni ya Magufuli jijini Dar es Salaam kuelekea Dodoma kushiriki hafla ya uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba pamoja na barabara zake za lami. Matumizi ya SGR katika safari hiyo yanaonesha namna reli ya kisasa inavyoweza kuwa kiungo muhimu katika kurahisisha usafiri wa watu na usafirishaji wa bidhaa, huku ikitoa fursa kwa viongozi na wageni wa kimataifa kujionea maendeleo ya miundombinu ya usafiri nchini. Hatua hiyo pia ni kielelezo cha ukuaji na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya usafirishaji Tanzania, hususan katika kuimarisha usalama, ufanisi na ubora wa huduma za reli. Reli ya SGR ina nafasi muhimu katika kupunguza muda wa safari, kurahisisha usafiri wa wananchi na kutoa huduma inayoweza kukidhi mahitaji ya makundi mbalimbali, yakiwemo wafanyabiashara, watalii na wasafiri wengine. Hivyo, uwekezaji huo una mchango katika kukuza shughuli za kiuchumi na kuimarisha ushindani wa Tanzania kama kitovu cha usafirishaji katika ukanda huu wa Afrika. Akizungumza kabla ya safari hiyo, Rais Samia alisema matumizi ya SGR yanaonesha dhamira ya Tanzania na Angola ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafirishaji, hususan reli, kwa lengo la kurahisisha usafiri wa watu na usafirishaji wa bidhaa kati ya nchi hizo na maeneo mengine ya Afrika. Alisema Tanzania inaendelea na ukarabati wa reli ya TAZARA inayounganisha nchi hiyo na Zambia kupitia Kapiri Mposhi, huku Angola nayo ikiendelea na ukarabati wa reli ya Benguela. Hatua hizo zinatarajiwa kuimarisha muunganiko wa reli na kurahisisha biashara katika ukanda huo. Katika mazungumzo yetu tumekubaliana tuunganishe korido zetu kati ya Benguela na korido ya ukanda wa Kati ya Tanzania ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa. Ndiyo maana tumeamua kutumia usafiri huu kuonesha kwamba inawezekana Kwa mtazamo mpana, matumizi ya SGR kwa viongozi hao ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania katika medani za kimataifa kama nchi inayopiga hatua katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya usafiri. Reli hiyo inatoa taswira ya Tanzania inayowekeza katika teknolojia na huduma zinazokidhi mahitaji ya sasa na zijazo, huku ikiimarisha uwezo wa nchi kuwahudumia wananchi na wageni wanaoitembelea. Aidha, kuunganisha korido za reli za Tanzania na Angola kunaweza kufungua fursa kubwa zaidi za biashara, utalii, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika. Kwa ujumla, safari hiyo imebeba ujumbe kwamba SGR si mradi wa usafiri pekee, bali ni sehemu ya mkakati mpana wa maendeleo ya taifa. Ni miundombinu inayopaswa kuendelea kutunzwa, kuboreshwa na kutumiwa ipasavyo ili kuimarisha usalama, kuongeza ufanisi wa usafirishaji na kuchochea uchumi. Hatua hiyo inaweka msingi wa Tanzania kuendelea kujijengea nafasi kama kitovu muhimu cha usafiri na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Na Neema Kaniki– MAELEZO Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kukuza uchumi na kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050. Amesema hayo Oktoba 25, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa jengo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo jijini Dodoma, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo na ustawi wa wananchi. Msigwa amesema Serikali inaendelea kutekeleza majukumu yake chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ukiwa umeanza kupitia bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa ulioanza Julai Mosi, 2026. Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 imeweka lengo la kujenga uchumi wenye thamani ya Dola za Marekani trilioni moja kutoka takribani Dola bilioni 90 za Marekani, hatua inayohitaji ushiriki na uwajibikaji wa pamoja kutoka kwa Serikali, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo. Mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 yanahitaji uwajibikaji wa pamoja kwa wadau wote, Serikali inatarajiwa kuchangia asilimia 30 ya uchumi huo, huku sekta binafsi ikitarajiwa kuchangia asilimia 70. Amesisitiza kuwa kufikiwa kwa malengo hayo kunategemea uwepo wa mazingira ya amani na utulivu yatakayowawezesha wananchi kujikita katika shughuli za uzalishaji mali, biashara, hususan biashara ya nje, pamoja na kuboresha maisha yao na ustawi wa jamii kwa ujumla. Amesema vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani vinaweza kukwamisha shughuli za kiuchumi, kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi, hivyo kuwataka Watanzania kutokubali kushawishiwa kushiriki matukio yanayoweza kuhatarisha utulivu wa nchi. Natoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kujiepusha na matukio yenye viashiria vya vurugu na uvunjifu wa amani, Watanzania wakatae watu wanaodhani wanaweza kufanikisha ajenda zao kwa kuwahamasisha kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria, pakichafuka hapa, hakuna mjomba wa kutusaidia zaidi ya sisi wenyewe. Aidha, Msigwa amewahakikishia wananchi kuwa Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kusimamia amani na usalama wa watu na mali zao, pamoja na kulinda mipaka ya nchi, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria kwa sababu ya kauli au msimamo wake.

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi majengo na miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Oktoba 30, 2026, katika hatua inayolenga kuimarisha ufanisi wa utendaji wa Serikali na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Akizungumza na waandishi wa habari, katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO jijini Dodoma, Oktoba 25, 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali imewekeza takribani shilingi bilioni 700 katika ujenzi wa mji huo. Msigwa amesema ujenzi wa majengo ya kisasa ya wizara na taasisi za Serikali ulianza mwaka 2021, chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, ukiwa ni sehemu ya utekelezaji wa uamuzi wa kuhamishia shughuli za Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, uliotangazwa mwaka 2016 na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Ameeleza kuwa Mji wa Serikali Mtumba umejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya kiutendaji, ukiwa na takribani kilomita 59 za barabara pamoja na mifumo ya kisasa ya mawasiliano inayowezesha taasisi za Serikali kuwasiliana na kutekeleza majukumu yake kwa njia ya mtandao. Amesema mifumo hiyo itapunguza urasimu na muda wa kushughulikia nyaraka, hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji wa Serikali na kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Faili likifika asubuhi linajibiwa mchana kwa sababu hakuna sababu ya kutuma watu na magari na bodaboda kwenda kusambaza barua. Barua zinatembea kwa mtandao. Aidha, amesema Tanzania imepokea ujumbe kutoka nchi zaidi ya 10 zilizofika kujifunza kuhusu ujenzi na uendeshaji wa Mji wa Serikali Mtumba, akibainisha kuwa miundombinu hiyo ina fursa ya kuwa kivutio cha utalii jijini Dodoma. Msigwa amewahimiza Watanzania kufuatilia uzinduzi huo, akieleza kuwa ni tukio muhimu katika historia ya maendeleo ya Dodoma na utekelezaji wa uamuzi wa kuifanya kuwa makao makuu ya Serikali.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Tanzania imeweka lengo la kuwa miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza duniani kwa uzalishaji wa chakula, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uchumi, kuongeza ajira na kuhakikisha usalama wa chakula kwa wananchi, kupitia uwekezaji katika sekta ya kilimo. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema azma hiyo imeainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050, inayolenga pia kuifanya nchi kuwa mzalishaji mkuu wa chakula barani Afrika. Akizungumza Oktoba 22, 2026, jijini Des Moines, Iowa, Marekani, wakati akiwasilisha mada kuu kuhusu mustakabali wa kilimo barani Afrika katika Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue), Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea kukipa kilimo kipaumbele kutokana na mchango wake katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa. Amesema chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi shilingi trilioni 1.241 mwaka 2025/2026, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kukifanya kilimo kuwa injini ya mageuzi ya kiuchumi, uzalishaji wa ajira, ukuaji wa viwanda na upanuzi wa masoko ya nje. Matokeo ya uwekezaji huo yanaonekana katika kiwango cha utoshelevu wa chakula nchini, ambacho kimefikia asilimia 130, hali inayoiwezesha Tanzania kukidhi mahitaji yake na kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya kikanda na kimataifa. Aidha, mauzo ya nje ya mazao ya kilimo yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 2.1 mwaka 2021/2022 hadi dola bilioni 3.7 mwaka 2024/2025, hatua inayoonesha nafasi inayozidi kuimarika ya kilimo katika kukuza biashara na mapato ya taifa. Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba anaeleza kuwa kilimo ni moja ya nguzo kuu za uchumi wa Tanzania, kikichangia asilimia 24.6 ya Pato la Taifa, kuajiri asilimia 65 ya nguvu kazi na kuzalisha takriban asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje, huku kikiendelea kutoa malighafi muhimu kwa viwanda vya ndani. Pamoja na mafanikio hayo, anasema Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza kilimo kinachozingatia usalama na ubora wa chakula. Katika mkutano huo, Dkt. Mwigulu amempongeza Prof. Huub Lelieveld, mshindi wa Tuzo ya Chakula Duniani ya mwaka 2026, kwa mchango wake katika masuala ya usalama wa chakula. Amesisitiza kuwa usalama wa chakula haupimwi kwa upatikanaji pekee, bali chakula kinapaswa kuwa salama kwa matumizi, kuwa na virutubisho vinavyohitajika na kupatikana kwa bei nafuu ili wananchi waweze kumudu mahitaji yao ya lishe. Akizungumzia kaulimbiu ya mjadala huo, “Kabla Njaa Haijatushinda,” Waziri Mkuu amesema Afrika ina uwezo mkubwa wa kuwa mchangiaji muhimu wa usalama wa chakula duniani, badala ya kuendelea kuonekana kama bara linalokabiliwa na changamoto za upatikanaji wa chakula. Amesema kufikia azma hiyo kunahitaji uwekezaji zaidi kwa wakulima, vijana na wanawake, pamoja na kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na mifumo imara ya uzalishaji na usambazaji wa chakula. Waziri Mkuu amehimiza mataifa ya Afrika kuchukua hatua za pamoja, kuendeleza ubunifu na kujenga mifumo endelevu ya chakula inayoweza kukidhi mahitaji ya vizazi vya sasa na vijavyo. Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mhariri Mkuu wa Jarida la Afrika la Chakula, Kilimo, Lishe na Maendeleo, Prof. Ruth Oniang’o, amesema anaamini Tanzania inaweza kuwa mfano kwa mataifa mengine kutokana na hatua inazopiga katika sekta ya kilimo. Prof. Oniang’o amesifu jitihada za Serikali, hususan uwekezaji katika miundombinu, utekelezaji wa programu ya Jenga Kesho Bora (BBT) na matumizi ya maafisa ugani kuwasaidia wakulima kuboresha uzalishaji. Kwa ujumla, lengo la Tanzania kuingia katika orodha ya nchi 10 bora duniani kwa uzalishaji wa chakula linaweka msisitizo katika kuendeleza uwekezaji, kuongeza tija na kutumia fursa za masoko ya kimataifa. Utekelezaji wake utahitaji kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao, kupanua fursa kwa wakulima na kuhakikisha chakula kinachozalishwa kinakidhi viwango vya ubora na usalama. Dkt. Mwigulu amehudhuria mkutano huo akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe; Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde; Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie Kanza, pamoja na watendaji wengine wa Serikali.

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO Ujenzi wa miundombinu ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma umefikia asilimia 89.02, huku ujenzi wa majengo ukifikia asilimia 78.37 na kazi mbalimbali za ukamilishaji zikiendelea kwa kasi. Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema hayo Septemba 24, 2026, jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka 2026/27. Kwa mujibu wa taarifa ya mradi, ujenzi wa jengo la abiria umefikia asilimia 81, mnara wa kuongozea ndege asilimia 74, Kituo cha Huduma za Zimamoto asilimia 88, jengo la kituo kikuu cha umeme asilimia 71 na jengo la huduma za hali ya hewa (MTO) asilimia 87. Mhandisi Besta amesema kazi zinazoendelea ni pamoja na kukamilisha majengo, kufunga mifumo ya mitambo ya uendeshaji wa uwanja, umeme na mabomba, mifumo ya mawasiliano na ukaguzi wa mizigo, pamoja na kufunga madaraja ya kupita abiria, mifumo ya hali ya hewa na magari ya zimamoto. Mradi huo pia umeendelea kutoa ajira kwa Watanzania. Mhandisi Besta amesema hadi sasa jumla ya ajira 9,059 zimezalishwa katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi. Amefafanua kuwa kati ya ajira hizo, 3,571 zimehusisha ujenzi wa miundombinu na 5,488 ujenzi wa majengo, huku wafanyakazi wa kigeni wakiwa 47. Kwa mujibu wa Mhandisi Besta, ujenzi wa miundombinu ya mradi unatarajiwa kukamilika Novemba 27, 2026, wakati ujenzi wa majengo ukitarajiwa kukamilika Desemba 30, 2026. Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria na mizigo, na kuimarisha nafasi ya Dodoma katika shughuli za kitaifa na kimataifa.

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Tanzania imeweka wazi azma yake ya kuwania nafasi ya uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029–2030, ikiwa na dhamira ya kupeleka katika chombo hicho sauti ya Afrika na kusukuma mbele ajenda ya amani, maendeleo na mageuzi ya mfumo wa kimataifa. Azma hiyo imetangazwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mjadala wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika jijini New York, Marekani. Mhe. Ndejembi amesema endapo Tanzania itachaguliwa, itatoa kipaumbele kwa diplomasia ya kuzuia migogoro kabla haijageuka kuwa vita, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani, kuimarisha nafasi ya wanawake katika ulinzi na ujenzi wa amani, kuongeza ushiriki wa vijana katika ajenda za amani na usalama, pamoja na kusukuma mbele mageuzi ya operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani. Dhamira hiyo imepata uungwaji mkono wa Umoja wa Afrika (AU), huku uchaguzi wa nafasi hiyo ukitarajiwa kufanyika Juni 2028. Kwa Tanzania, safari ya kuwania nafasi hiyo inakwenda sambamba na hoja pana ya kutaka mfumo wa kimataifa uwe na uwakilishi wenye uwiano zaidi na kutoa nafasi kubwa kwa nchi zinazoendelea kushiriki katika maamuzi yanayogusa mustakabali wa dunia. Katika hotuba yake, Mhe. Ndejembi amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kuendelea kufanyiwa mageuzi ili kuimarisha misingi ya haki, usawa na uwakilishi, hususan wakati dunia ikikabiliwa na changamoto zinazovuka mipaka ya nchi moja. Migogoro na vita, mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa, kasi ya maendeleo ya akili mnemba (AI) na changamoto za usalama wa nishati ni miongoni mwa masuala ambayo Tanzania imesema yanahitaji ushirikiano wa kimataifa na taasisi zenye uwezo wa kuitikia mahitaji ya dunia ya sasa. Katika kueleza msingi wa msimamo wake, Tanzania imeonyesha pia uzoefu wake katika kushughulikia changamoto za maendeleo na ustawi wa jamii. Mhe. Ndejembi amesema Tanzania imepiga hatua katika kuboresha afya ya mama na mtoto, ambapo kiwango cha uzazi unaofanyika katika vituo vya afya kiliongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2015 hadi asilimia 81 mwaka 2022. Tanzania pia imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama kwa asilimia 80 ndani ya kipindi cha miaka saba, hatua ambayo imehusishwa na uwekezaji katika huduma za afya na kuweka ustawi wa wananchi kuwa sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo. Uzoefu huo umeendelea kupewa nafasi katika ajenda ya afya ya mama na mtoto barani Afrika, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amekubali jukumu la kuwa kinara wa masuala hayo kwa niaba ya Umoja wa Afrika. Chini ya ajenda ya “Sifuri Tatu” (Three Zeros), Tanzania inalenga kufikia kutokuwepo kwa vifo vya mama na mtoto vinavyoweza kuzuilika, kutokuwepo kwa uzazi unaofanyika majumbani na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo. Mhe. Ndejembi amesema kufikia malengo hayo kunawezekana, lakini kunahitaji uongozi thabiti wa kisiasa, rasilimali za kutosha na ushirikiano imara wa kimataifa. Pamoja na afya, Tanzania imeunganisha azma yake ya kidiplomasia na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi jumuishi, shindani na wenye uwezo wa kustahimili misukosuko kupitia uwekezaji katika watu, miundombinu, teknolojia, ubunifu, wanawake na vijana. Hata hivyo, Tanzania imesema utekelezaji wa malengo ya maendeleo katika nchi zinazoendelea unaendelea kukabiliwa na changamoto za upatikanaji wa fedha, gharama za mikopo na mazingira ya mfumo wa fedha wa kimataifa huku ikitoa wito wa kuongezwa kwa mikopo yenye masharti nafuu, kuhamasishwa kwa uwekezaji wa sekta binafsi, kurahisishwa kwa upatikanaji wa fedha za maendeleo na tabianchi, pamoja na nchi zinazoendelea kupewa sauti kubwa zaidi katika maamuzi ya kifedha duniani. Mabadiliko ya tabianchi nayo yamepewa nafasi katika ujumbe wa Tanzania, huku nchi ikieleza wasiwasi kuhusu pengo lililopo kati ya kiwango cha uzalishaji wa gesi chafuzi duniani na fedha zinazotolewa kusaidia nchi zinazoathirika kukabiliana na madhara yake. Tanzania imesisitiza kuwa nchi zinazochangia kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa gesi chafuzi zinapaswa kubeba wajibu mkubwa zaidi katika kugharamia hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Katika kueleza hatua zake za mpito kuelekea nishati safi, Tanzania imetaja Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, miradi ya nishati ya jua na upepo yenye jumla ya megawati 650, pamoja na mipango ya kuzalisha megawati 130 za nishati ya jotoardhi. Tanzania pia imeeleza uwekezaji katika reli ya umeme na lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia hadi kufikia asilimia 80 ya kaya ifikapo mwaka 2034. Katika masuala ya diplomasia na mahusiano ya kimataifa, Tanzania imeeleza msimamo wake dhidi ya matumizi ya vikwazo vya upande mmoja vinavyowekwa na baadhi ya mataifa dhidi ya mengine. Kwa mujibu wa Tanzania, hatua hizo zinaweza kuathiri maendeleo, mamlaka ya nchi na uwezo wa wananchi kunufaika kikamilifu na haki zao. Nchi hiyo imetaja mshikamano wake na Cuba, Zimbabwe na mataifa mengine yanayokabiliwa na vikwazo hivyo, huku ikitoa wito wa hatua za makusudi kuelekea kuondolewa kwa vikwazo bila masharti. Kuhusu migogoro inayoendelea ukanda wa Gaza na Mashariki ya Kati, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kulindwa kwa raia, misaada ya kibinadamu kuwafikia wanaohitaji bila vikwazo na diplomasia kurejeshwa kuwa njia kuu ya kutafuta amani ya kudumu. Kwa ujumla, ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeunganisha masuala ya amani na usalama na ajenda ya maendeleo ya nchi zinazoendelea. Azma ya kuwania nafasi katika Baraza la Usalama imekuja ikiwa imejengwa juu ya hoja za kuimarisha diplomasia ya kuzuia migogoro, kutafuta suluhu za amani, kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika amani na usalama, pamoja na kusukuma mageuzi ya mfumo wa kimataifa. Kwa Tanzania, mjadala wa nafasi ya Afrika katika mfumo wa kimataifa hauishii kwenye uwakilishi pekee. Unaenda sambamba na masuala ya maendeleo, fedha, tabianchi, afya, nishati na amani ambayo yanaathiri moja kwa moja maisha ya watu.

Na Baraka Messa – Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewataka Maafisa Habari wa Serikali na Taasisi za Umma kuongeza ubunifu na weledi katika utoaji wa taarifa kwa umma kwa kuangazia zaidi uwekezaji unaofanywa na Serikali na matokeo yake katika kuboresha maisha ya wananchi. Msigwa ametoa wito huo Septemba 9, 2026, jijini Dodoma, wakati akiwakaribisha na kuwapa maelekezo Maafisa Habari wapya walioajiriwa katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, katika Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali, Mtumba. Amesema wajibu wa Maafisa Habari ni kuhakikisha wananchi wanafahamu kwa wakati hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuleta maendeleo, ikiwemo uwekezaji katika miundombinu, elimu, afya, maji, nishati, usafiri, teknolojia na sekta nyingine zinazogusa maisha yao. Kazi yetu ni kuhabarisha wananchi. Tueleze Serikali imefanya nini, inafanya nini na inatarajia kufanya nini, kwa sababu hayo ndiyo mambo yanayowagusa wananchi. Amesema katika kutekeleza wajibu huo, Maafisa Habari wanapaswa kuwasilisha taarifa zinazoonesha kwa uwazi uwekezaji uliofanyika, miradi inayotekelezwa, thamani ya uwekezaji huo, hatua iliyofikiwa na matokeo yanayopatikana, ili wananchi waweze kutambua namna rasilimali za Serikali zinavyotumika katika kuleta maendeleo. Msigwa amesema taarifa za utekelezaji wa Serikali zinapaswa kwenda zaidi ya kueleza tukio, badala yake zioneshe maana ya mradi kwa mwananchi, ikiwemo huduma zitakazopatikana, fursa zitakazozalishwa, ajira zitakazoongezeka na mchango wake katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Amesema Maafisa Habari wana nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanaelewa mipango na vipaumbele vya Serikali, pamoja na kutambua hatua zinazochukuliwa katika kutatua changamoto zinazowakabili. Taarifa nzuri si ile inayosema tu mradi umejengwa, bali ieleze mradi huo umejengwa kwa gharama gani, unahudumia wananchi wangapi na umeleta mabadiliko gani katika maisha yao. Aidha, amewataka Maafisa Habari kutumia ipasavyo teknolojia za kisasa na majukwaa ya kidijitali, hususan mitandao ya kijamii, katika kufikisha taarifa za maendeleo kwa wananchi kwa lugha rahisi, yenye mvuto na inayoeleweka kwa makundi mbalimbali. Amesema matumizi ya teknolojia yanatoa fursa ya Serikali kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja, hivyo Maafisa Habari wanapaswa kutumia ubunifu katika kuandaa maudhui yanayowapa wananchi uelewa wa shughuli, miradi na uwekezaji unaofanywa na Serikali. Vilevile, Msigwa amewataka Maafisa Habari hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wakizingatia misingi ya uadilifu, weledi, uwajibikaji na maslahi mapana ya umma. Amesema Maafisa Habari ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi, hivyo wanapaswa kuhakikisha taarifa wanazozitoa zinajenga uelewa kuhusu maendeleo yanayotekelezwa na Serikali na kuwasaidia wananchi kutambua fursa na manufaa yanayotokana na uwekezaji huo. Msigwa amesisitiza kuwa, kupitia taarifa sahihi, zenye ushahidi na zinazoonesha matokeo, Maafisa Habari wanaweza kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya rasilimali za Taifa na mchango wa uwekezaji wa Serikali katika kuboresha huduma na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.