Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Nchi ya Tanzania na Uganda zimekubaliana kuharakisha utatuzi wa vikwazo vya biashara, kupanua masoko ya bidhaa zao na kuboresha usafirishaji ili kukuza biashara na uwekezaji kwa manufaa ya nchi zote mbili. Makubaliano hayo yamefikiwa Novemba 18, 2026 wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika ziara ya kitaifa ya siku mbili ya Rais wa Tanzania nchini Uganda. Rais Dkt. Samia amesema Tanzania na Uganda zimepiga hatua katika kutekeleza maamuzi ya awali kuhusu biashara, uwekezaji, nishati, usafiri na miundombinu. Ametaja changamoto za usafiri na usafirishaji kuwa miongoni mwa sababu zinazorudisha nyuma ukuaji wa biashara, na kueleza hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kuboresha miundombinu hiyo. Rais Dkt. Samia amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Uganda katika mradi wa reli ya kisasa utakaounganisha Isaka na maeneo ya mpakani na Uganda. Tanzania itaendelea kushirikiana na Uganda kwa moyo wa watu wamoja, hatima moja. Sasa ni wakati wa kuharakisha utekelezaji wa tuliyokubaliana,” Amesema Rais Dkt. Samia, akibainisha hatua za upanuzi na maboresho ya Bandari za Dar es Salaam na Tanga kuwa sehemu ya jitihada za kuboresha usafiri na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki. Pia, Rais Dkt. Samia ameipongeza Uganda kwa kuanza ujenzi wa ubalozi wake katika Mji wa Serikali Dodoma, ikiwa ni Taifa la kwanza kufanya hivyo tangu kuzinduliwa kwa mji huo. Kwa upande wake, Rais Museveni amesema biashara kati ya Tanzania na Uganda inapaswa kuzingatia mahitaji ya pamoja, akitolea mfano wa mchele wa Tanzania wenye uhitaji mkubwa nchini Uganda, na sukari inayozalishwa Uganda yenye soko kubwa nchini Tanzania. Ameongeza kuwa, Uganda ina ziada kubwa ya sukari, huku wananchi wake wakinunua mchele wa Tanzania kwa kuwa ni bora na wa bei nafuu. Rais Museveni pia ameonya dhidi ya hatari ya shinikizo la ndani la kuzuia bidhaa zinazotoka nchi moja kwenda nyingine, na namna linavyoweza kudhoofisha uzalishaji, na kushusha uhusiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Uganda. Tunahitaji maliasili, uzalishaji wa bidhaa, soko la kutosha na mawasiliano. Amesema Rais Museveni, akisisitiza kuwa nchi za Afrika zinahitaji kuunganisha nguvu katika usimamizi wa rasilimali kwa manufaa ya wananchi wao. Viongozi hao pia wamejadili ushirikiano katika sekta ya nishati, ikiwemo usafishaji wa mafuta na uratibu wa miradi ya viwanda katika nchi hizo, ambapo Rais Museveni amesema nchi yake inapanga kujenga kiwanda kidogo cha kusafisha mafuta Hoima na inaunga mkono ujenzi wa kiwanda kikubwa zaidi jijini Tanga, Tanzania. Kwa pamoja, wamehimiza utekelezaji wa haraka wa makubaliano.

Na Baraka Messa – MAELEZO Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameitaka Wizara ya Maji kuharakisha usanifu wa upanuzi wa Mradi wa Maji wa Kilwa ili wananchi wa Kata ya Mandawa, Hoteli Tatu na maeneo jirani nao wanufaike na huduma ya maji safi na salama. Ndejembi ametoa agizo hilo novemba 15,2026 wakati wa kukagua utekelezaji wa mradi huo katika eneo la Mavuji, Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, akisisitiza kuwa uwekezaji unaofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unapaswa kuwafikia wananchi wote, wakiwemo wale ambao bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji. Ni muhimu kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya maji unawanufaisha wananchi wote. Hivyo, usanifu wa upanuzi wa mradi huu uharakishwe ili wananchi wa Mandawa, Hoteli Tatu na maeneo jirani nao wapate huduma ya maji safi na salama. Amesema ni muhimu hatua za upanuzi wa mradi huo kuchukuliwa kwa haraka ili maeneo ambayo hayajanufaika na huduma hiyo ya msingi yaendelee kuingizwa katika mfumo wa usambazaji wa maji, hatua itakayosaidia kuboresha afya na maisha ya wananchi. Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema mamlaka ya maji imeelekezwa kuanza usanifu wa upanuzi wa mradi huo ili kubaini gharama zinazohitajika, huku Wizara ya Maji ikiahidi kutoa fedha kwa ajili ya kufanikisha hatua hiyo. Mradi huo ni sehemu ya Mradi wa Maji wa Miji 28, wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 44.25 na umefikia asilimia 97.4 ya utekelezaji. Tayari umeanza kutoa huduma na unatarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 59,983 wa Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje, Mavuji na Mchakama. Kwa mujibu wa taarifa za mradi huo, unatumia chanzo cha Mto Mavuji na una uwezo wa kuzalisha lita milioni tano za maji kwa siku, kiasi kinacholenga kukidhi mahitaji ya wananchi katika maeneo yanayohudumiwa. Aidha, mradi huo unahudumia pia Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, ambayo inahitaji lita milioni moja za maji kwa siku wakati wa uendeshaji wake, hivyo kuwa na mchango muhimu katika kuimarisha huduma za kijamii na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO Serikali imepanga kuanzisha Mfuko Maalumu wa Nishati Safi ya Kupikia ili kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi kwa kuwapatia mitaji ya kuzalisha majiko banifu na nishati mbadala katika halmashauri zote nchini. Akizungumza Novemba 15, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu manufaa ya ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), uliofanyika Antalya, Uturuki, Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Homera, amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini. Amesema kupitia mfuko huo, vikundi vya vijana na wanawake katika kila halmashauri vitawezeshwa kupata mitaji kwa ajili ya kutengeneza majiko banifu na kuzalisha mkaa mbadala, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za ajira na ujasiriamali pamoja na kuinua kipato cha wananchi. Ameeleza kuwa mpango huo pia utachangia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida, hivyo kupunguza shinikizo la ukataji wa miti, kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Aidha, ameitaka sekta binafsi kutumia fursa zilizopo katika sekta ya nishati safi ya kupikia kwa kuwekeza katika uzalishaji na usambazaji wa teknolojia za nishati hiyo, akibainisha kuwa uwekezaji huo una uwezo mkubwa wa kuchochea ukuaji wa uchumi na kutengeneza ajira kwa Watanzania. Katika hatua nyingine, amesema Serikali inaendelea kupanua matumizi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi za umma, ambapo hadi sasa taasisi 2,745 zimeanza kutumia nishati hiyo. Kati ya hizo, magereza ni 129 huku taasisi nyingine za Serikali zikiwa 2,616. Ameongeza kuwa wadau wa maendeleo wameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha sekta hiyo, ikiwemo kutekeleza mpango wa kuwafikia wananchi milioni moja kwa kuwapatia majiko ya umeme yatakayolipiwa kupitia mfumo wa LUKU. Amesisitiza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, huku ikiendeleza fursa za kiuchumi kwa vijana na wanawake na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Na Mwandishi Wetu – Geneva, Uswisi Tanzania imekubali mapendekezo 196 kati ya 280 yaliyotolewa na nchi mbalimbali katika Duru ya Nne ya Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR), hatua inayoonesha dhamira ya Serikali kuendelea kuimarisha ulinzi na utekelezaji wa haki za binadamu, utawala bora na maendeleo jumuishi, kwa kuzingatia Katiba, sheria na vipaumbele vya Taifa. Katika mapendekezo hayo yaliyotolewa katika Kikao cha 53 cha Kikundi Kazi cha Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, kilichofanyika Geneva, Uswisi, Tanzania haijaunga mkono mapendekezo 68, huku ikiahirisha kutoa msimamo kuhusu mapendekezo 16 ili kupata nafasi ya kuyafanyia uchambuzi na mashauriano zaidi kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho. Akitangaza matokeo hayo hivi karibuni jijini Geneva, Uswisi, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Ulega, amesema maamuzi yaliyofikiwa yanaonesha utayari wa Tanzania kuendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kukuza na kulinda haki za binadamu, huku ikiheshimu mamlaka yake ya kitaifa katika kuamua masuala yanayohusu mustakabali wa nchi. Amesema mapendekezo 196 yaliyokubaliwa yanaendana na Katiba, sheria, sera na mipango ya maendeleo ya Taifa, hususan Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030, ambayo inaweka mkazo katika maendeleo jumuishi, ulinzi wa haki na ustawi wa wananchi. Mapendekezo yaliyokubaliwa yanahusu kuimarisha utawala bora, utawala wa sheria, upatikanaji wa haki, mageuzi ya kikatiba na huduma za msaada wa kisheria; kulinda haki za wanawake, watoto, watu wenye ulemavu ikiwemo wenye ualbino; pamoja na kuboresha huduma za elimu, afya, maji safi na salama na hifadhi ya jamii. Ameongeza kuwa mapendekezo mengine yanahusu utunzaji wa mazingira, kuimarisha ushirikiano na mifumo ya kimataifa na kikanda ya haki za binadamu, pamoja na kuhakikisha maendeleo yanawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi wala kumwacha mtu nyuma. Akifafanua sababu za kutounga mkono mapendekezo 68, Waziri Ulega amesema baadhi ya mapendekezo hayo hayawiani na misimamo na vipaumbele vya kitaifa, hususan yanapogusa masuala yanayohusiana na mila, desturi, tamaduni na maadili ya jamii ya Kitanzania. Amesema pia yapo mapendekezo yanayohitaji kuzingatia mazingira ya kikatiba, kisheria, kijamii na kiuchumi ya nchi, huku mengine yakihitaji utafiti, tathmini na mashauriano zaidi kabla ya kufikiwa kwa maamuzi. Miongoni mwa maeneo ambayo Tanzania haikuunga mkono ni masuala ya mahusiano ya jinsia moja, kuondoa adhabu ya kifo, pamoja na mapendekezo yanayohitaji maamuzi kabla ya kukamilika kwa mashauriano ya kitaifa na mapendekezo ya kurekebisha matakwa ya kisheria ambayo kwa tathmini ya Serikali tayari yanaendana na viwango vya kimataifa. Katika hatua nyingine, Serikali imeahirisha kutoa msimamo kuhusu mapendekezo 16 ili kufanya uchambuzi na mashauriano zaidi kuhusu athari zake za kisheria, kisera na kiuchumi, pamoja na mahitaji ya rasilimali fedha na watu yatakayohitajika katika utekelezaji wake. Waziri Ulega, amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa maamuzi yatakayofikiwa yanazingatia uhalisia wa mazingira ya nchi, uwezo wa utekelezaji na kuepusha athari zisizotarajiwa. Mapendekezo hayo yanahusu taratibu za dhamana, muda wa kushikiliwa kwa watuhumiwa na mfumo wa elimu bila ada, ambao Serikali inaendelea kuutekeleza. Tanzania inatarajia kuwasilisha msimamo wake wa mwisho kuhusu mapendekezo hayo 16 katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachotarajiwa kufanyika Februari 2027, baada ya kukamilisha mashauriano na taasisi husika, zikiwemo Mahakama, Bunge, asasi za kiraia na wadau wengine, kwa kuzingatia mamlaka na majukumu yao ya kikatiba na kisheria.

Na Mwandishi wetu- Lindi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Jeshi la Polisi kuchunguza matumizi ya fedha za mradi wa kuboresha miundombinu ya Manispaa ya Lindi, baada ya taarifa kuonesha kuwa mkandarasi amelipwa shilingi bilioni 4.22, huku utekelezaji ukiwa asilimia 24 na muda mkataba uliotumika ukiwa asilimia 80. Akitoa maelekezo Novemba 14, 2026 wakati wa ziara yake mkoani Lindi, Makamu wa Rais ametaka kufahamishwa namna malipo yalivyofanyika, fedha zilivyotumika na sababu za kazi kutotekelezwa kwa kasi iliyotarajiwa ambapo pia ameagiza taarifa ya uchunguzi imfikie ili aiwasilishe kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mhe. Ndejembi amehoji sababu za mkandarasi kuendelea kulipwa fedha nyingine wakati Halmashauri yenyewe ilieleza kuwa hakuwa na nidhamu katika matumizi ya malipo ya awali. Aidha, ameonesha kutoridhishwa na maelezo ya halmashauri kwamba imemwandikia mkandarasi barua 16 kuhusu kusuasua kwa mradi huo akieleza kuwa Halmashauri hiyo ilipaswa kuchukua hatua badala ya kuendelea kuandikiana barua wakati fedha za umma zimeshalipwa. Taarifa ya utekelezaji iliyowasilishwa wakati wa ukaguzi wa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 19.06 imeeleza kuwa mradi unatekelezwa na kampuni ya Hamerkop International Limited JV KIKIM Contractor’s Limited ambapo mkandarasi amelipwa jumla ya shilingi bilioni 4.22, zinazojumuisha malipo ya awali ya shilingi bilioni 2.86 na malipo kupitia hati namba mbili ya shilingi bilioni 1.36. Mkataba wa mradi huo ulisainiwa Juni 25, 2025, mjini Dodoma, na kazi kuanza rasmi Novemba 7, 2025. Mradi unatakiwa kukamilika Februari 5, 2027. Kwa mujibu wa taarifa, utekelezaji ulitarajiwa kufikia asilimia 80 katika hatua hii, hivyo kiwango cha asilimia 24 kilichofikiwa kiko nyuma kwa pointi 56 za asilimia. Mradi huo, unatekelezwa kupitia mpango wa TACTIC, unajumuisha Soko Kuu la Matopeni, barabara za kilomita 5.3, Stendi ya Mabasi Mitwero na Ofisi ya Uratibu wa Mradi. Unafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Serikali chini ya TAMISEMI, huku usimamizi wa kitaalamu ukifanywa na Inter-Consult Limited kwa kushirikiana na Tanzo Vision Engineering Limited. Kusuasua kwa ujenzi wa mradi huo kulimfanya Waziri anayehusika na TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, kufanya ukaguzi Septemba 14, 2026. Aliagiza mkandarasi atafute wakandarasi wadogo wenye uwezo, pamoja na kuundwa kwa timu maalumu ya ufuatiliaji iliyobaini mkandarasi hana uwezo wa kukamilisha mradi kwa wakati uliopangwa na kupedekeza abaki na ujenzi wa soko, huku kazi nyingine tatu zikitekelezwa na wakandarasi wadogo.

Na Mwandishi Wetu- Mtwara Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi ameonya kuwa Serikali haitamvumilia afisa ugani, afisa kilimo au mfanyabiashara atakayebainika kuchakachua pembejeo na kuwanyonya wakulima wa korosho. Akizungumza Novemba 12, 2026 na wananchi wa Masasi mkoani Mtwara, Makamu wa Rais amesema ruzuku ya pembejeo inayotolewa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kuongeza uzalishaji na kuinua kipato cha wakulima, hivyo haitaruhusiwa kugeuzwa njia ya watu wachache kujitajirisha. Onyo hilo limetolewa kufuatia kushuka kwa uzalishaji wa korosho kutoka tani 600,000 hadi tani 400,000, huku wakulima wakilalamikia pembejeo kutotoa matokeo yaliyotarajiwa. Wakati Rais Samia anaingia madarakani, uzalishaji ulikuwa tani 180,000 kabla ya kuongezeka hadi tani 600,000 baada ya Serikali kuweka ruzuku ya pembejeo ya salfa. Ameitaka Wizara ya Kilimo kuchunguza malalamiko kuhusu ubora wa pembejeo, yakiwemo madai ya kuchakachuliwa au kupungua nguvu kutokana na kukaa muda mrefu, ili kubaini chanzo cha kushuka kwa uzalishaji. Aidha, amewahimiza wakulima kuendelea kwenda mashambani, akiwahakikishia kuwa Serikali itaendeleza ruzuku na kushughulikia changamoto za pembejeo ili uzalishaji urejee katika kiwango cha awali na hatimaye kufikia tani milioni moja. Akieleza hatua zinazochukuliwa, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema salfa ya unga haikutosheleza mahitaji katika msimu huu, hali iliyolazimu kuletwa kwa salfa ya maji ambayo haikufanya vizuri katika baadhi ya maeneo. Amesema awali kulikuwa na takribani tani 16,000 za salfa ya unga na baadaye zikaongezwa tani 10,000, lakini mahitaji yalikuwa makubwa zaidi. Chongolo amesema timu ya wataalamu kutoka TPHPA, TARI na Wizara ya Kilimo imepelekwa kufanya uchunguzi wa kina kubaini iwapo changamoto ilitokana na viuatilifu, namna ya matumizi au sababu nyingine. Ameahidi kuwa katika maandalizi ya msimu ujao, wizara inalenga kuhakikisha salfa ya unga inafika katika maeneo ya uzalishaji ifikapo Machi mwaka ujao ili wakulima waipate kwa wakati. Amesisitiza kuwa pembejeo za ruzuku ni nyenzo ya kuwakwamua wakulima kiuchumi, na kuwaonya wanaotaka kuzitumia kujinufaisha kwa kuwaumiza wananchi. Katika mkutano huo, Mbunge wa Masasi ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo amepongeza uwekezaji wa Serikali katika elimu, afya na miundombinu, akisisitiza umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya hiyo. Akizungumzia suala la maji, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amekiri kuwapo kwa pengo kubwa la huduma, akisema mahitaji ya Masasi ni lita milioni 16, wakati kiasi kinachofikishwa ni lita milioni sita, hivyo kuacha upungufu wa lita milioni 10. Amesema Wizara ya Maji itatoa fedha za dharura kwa hatua za haraka, huku timu ya wataalamu ikishirikiana na Serikali ya Mkoa, viongozi wa Masasi na wananchi kuandaa ufumbuzi wa muda mfupi na mpango wa kudumu. Waziri huyo ameahidi kuisimamia kazi hiyo kwa haraka, sambamba na maandalizi ya mradi mkubwa utakaokidhi mahitaji ya wananchi wa Masasi kwa muda mrefu.

Na Sidi Mgumia-MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania inaendelea kupanua upatikanaji wa umeme kupitia Mpango wa Taifa wa Nishati (National Energy Compact), huku ikiimarisha maendeleo jumuishi na yanayohimili mabadiliko ya tabianchi kupitia Dira ya Maendeleo ya miaka 25 ijayo. Mhe. Rais Samia ameyasema hayo Novemba 11, 2026, nchini Uturuki , wakati akihutubia ufunguzi wa Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), unaofanyika Antalya, ambapo amesema Tanzania inaendelea kukabiliwa na ukame wa muda mrefu, mabadiliko yasiyotabirika ya misimu ya mvua na kupanda kwa kina cha bahari, hali inayokadiriwa kuigharimu nchi kati ya asilimia mbili na tatu ya Pato la Taifa (GDP) kila mwaka. Tanzania inaipa kipaumbele upatikanaji wa fedha za tabianchi za kutosha, zinazotabirika na zinazopatikana kwa urahisi, pamoja na kuimarisha fursa za masoko ya kaboni katika sekta za usafirishaji, usimamizi wa taka, nishati jadidifu na misitu inayokadiriwa kufunika hekta milioni 48.1. Amesisitiza kuwa juhudi hizo zitaenda sambamba na kuwaandaa vijana kupata ujuzi na ajira katika nishati jadidifu, kilimo endelevu na viwanda rafiki kwa mazingira, pia ametoa wito kwa nchi kushirikiana ili kuhakikisha COP31 inabadilisha ahadi kuwa vitendo na matokeo yanayopimika. Afafanua kuwa umuhimu wa mifumo ya biashara ya kaboni chini ya Kifungu cha Sita cha Mkataba wa Paris kuwa ya uwazi na kuhakikisha manufaa yanawafikia jamii zinazotekeleza miradi hiyo. Kwa upande wake, Rais wa COP31, Mhe. Murat Kurum, amezitaka nchi kuingiza malengo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika mipango ya uwekezaji, bajeti za kitaifa na miradi ya maendeleo ili kuhakikisha ahadi zinazotolewa zinatafsiriwa katika matokeo halisi kwa wananchi. Amesema mabadiliko ya tabianchi sasa yanahusisha masuala ya nishati, viwanda, kilimo, maendeleo na usalama, hivyo yanahitaji mipango inayozingatia mahitaji ya sasa na vizazi vijavyo. Ametolea mfano historia ya Istanbul katika karne ya 16, ambapo Sultan Suleiman alimwelekeza mbunifu Mimar Sinan kutafuta vyanzo vya maji na kujenga mifumo ya kuyasafirisha hadi jijini, akisema hatua hiyo ilihakikisha upatikanaji wa maji kwa wakazi kwa karne nyingi. Amesema mfano huo unaonesha umuhimu wa viongozi kuwekeza katika suluhisho za muda mrefu badala ya kusubiri changamoto zijitokeze. Uturuki inalenga kufikia uchumi usiozalisha hewa chafuzi ifikapo mwaka 2053, sambamba na kuendelea kuunga mkono juhudi za kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzi joto 1.5. Ameeleza kuwa uwekezaji katika matumizi bora ya nishati unaimarisha usalama wa nishati, usimamizi wa maji unaimarisha usalama wa chakula, huku teknolojia safi zikichochea maendeleo ya viwanda na kutengeneza ajira. Aidha, amesema Uturuki imeandaa mpango wa Climate Implementation Bridge unaolenga kuunganisha mipango ya kitaifa ya tabianchi na uwekezaji, ufadhili, teknolojia na utaalamu ili kuharakisha utekelezaji wa ahadi. Ameongeza kuwa kupitia mpango wa 35 by 35 Global Electrification Pledge, nchi hiyo inalenga kuongeza mchango wa umeme katika matumizi ya mwisho ya nishati hadi asilimia 35 ifikapo mwaka 2035, sambamba na kuendeleza mpango wa Zero Waste unaohamasisha matumizi endelevu ya rasilimali.

Na Mwandishi Wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametaja vipaumbele vitatu ambavyo Tanzania inavipa uzito katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku akisisitiza umuhimu wa upatikanaji wa fedha za kutosha, mpito wa haki wa matumizi ya nishati na kuimarisha maendeleo jumuishi yanayostahimili athari za tabianchi. Rais Dkt. Samia ametaja vipaumbele hivyo Novemba 11, 2026, alipokuwa akihutubia Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) unaofanyika jijini Antalya, nchini Uturuki, ambapo amesema Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea, inaendelea kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi zikiwemo ukame wa muda mrefu, mabadiliko yasiyotabirika ya mvua na kupanda kwa kina cha bahari. Rais Samia amesema nchi zinazoendelea zinahitaji fedha za kutosha, zinazotabirika na zinazopatikana kwa urahisi, hususan ruzuku na mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, sambamba na uhamishaji wa teknolojia na kujengewa uwezo. Tanzania ina fursa nyingi za kuchangia katika kupunguza hewa ukaa kupitia sekta za usafiri, usimamizi wa taka, nishati jadidifu ikiwemo umeme wa maji, jotoardhi na upepo, pamoja na misitu inayokadiriwa kufunika takribani hekta milioni 48.1. Hivyo, nasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mifumo ya uwazi ya biashara ya hewa ukaa na utekelezaji wa Ibara ya Sita ya Mkataba wa Paris ili kuhakikisha manufaa yanagawanywa kwa haki na mazingira yanalindwa. Akitaja kipaumbele cha pili, Mhe. Rais Samia amesema kuwa Tanzania inasisitiza umuhimu wa mpito wa haki wa matumizi ya nishati barani Afrika, unaozingatia upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na endelevu kwa wananchi wote huku akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Nishati kwa lengo la kupanua upatikanaji wa umeme nchini, hususan maeneo ya vijijini, huku akitoa wito wa kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi, mikopo yenye masharti nafuu na uhamishaji wa teknolojia. Ameendelea kwa kusema kipaumbele cha tatu kuwa Tanzania inaendelea kuimarisha maendeleo jumuishi na yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi kupitia Dira ya Maendeleo ya miaka 25 ijayo, inayoweka mkazo katika ubunifu, ujenzi wa viwanda na mageuzi ya kiuchumi endelevu. Aidha, ameeleza kuwa Dira hiyo inatambua umuhimu wa kuwaandaa vijana kwa kuwapatia ujuzi wa kijani na fursa za ajira zinazozingatia utunzaji wa mazingira, pamoja na kuendeleza kilimo endelevu, nishati jadidifu na viwanda vinavyohifadhi mazingira. Tanzania ina dhamira thabiti ya kutekeleza malengo ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi na Mkataba wa Paris, ni matarajio yangu kuwa COP31 itaimarisha ushirikiano wa kimataifa katika upatikanaji wa fedha, uhamishaji wa teknolojia na kujenga uwezo ili kuwezesha utekelezaji wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Na Mwandishi Wetu – Songea, Ruvuma Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka viongozi na watendaji wa Serikali wanaosimamia miradi ya maendeleo kuwajibika ipasavyo na kuchukua hatua dhidi ya wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba. Ametoa agizo hilo kufuatia kuchelewa kwa ujenzi wa Soko la Manzese A na B katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, licha ya mkandarasi wa mradi huo kulipwa Shilingi bilioni tatu kama malipo ya awali. Mradi huo ulioanza mwaka 2025 kwa muda wa utekelezaji wa miezi 18, ulitarajiwa kukamilika Septemba 2026, lakini haujakamilika kwa wakati kutokana na changamoto za usimamizi na upungufu wa vifaa vya ujenzi hali iliyosababisha mkandarasi kuongezewa muda wa utekelezaji hadi Machi 2027. Akizungumza na wananchi wa Songea wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma, Makamu wa Rais amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Wakili Bashir Muhoja, kueleza sababu za kuendelea kumuongezea muda mkandarasi huyo licha ya kutoridhisha kwa kasi ya utekelezaji wa mradi. Hebu tubadilike! Tuwajibike katika matumizi ya fedha za umma. Kikao cha ngazi ya juu kinakusaidia nini? alihoji Makamu wa Rais, akisisitiza kuwa vikao vya mara kwa mara havipaswi kutumika kama mbadala wa hatua madhubuti za kuwawajibisha Wakandarasi wanaokiuka masharti ya mikataba. Aidha, amemtaka Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuchukua hatua stahiki dhidi ya mapungufu yaliyojitokeza katika usimamizi wa mradi huo, ili kuhakikisha watendaji wanawajibika kwa majukumu waliyopewa. Katika hatua nyingine, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza kampuni iliyokabidhiwa kazi hiyo, ikiwemo matumizi ya fedha za malipo ya awali, ili kubaini sababu za kushindwa kutekeleza mradi kwa kasi inayotakiwa. Amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia uzembe katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, hasa pale unapochangia kuchelewesha huduma kwa wananchi na kusababisha fedha za umma kutotumika kwa tija iliyokusudiwa. Makamu wa Rais anaendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Ruvuma, ambapo anatarajiwa kutembelea mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.

Na mwandishi wetu-Tunduru Ruvuma Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameagiza kuanza mara moja kwa operesheni maalumu ya kuwabaini na kuwakamata watu wanaochochea migogoro ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, huku akitaka kupatiwa taarifa ya hatua zilizochukuliwa akiwa bado katika ziara yake mkoani humo. Akizungumza Novemba 11, 2026 katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Tunduru, Makamu wa Rais amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imesikia kilio cha wananchi kutokana na migogoro hiyo iliyosababisha vifo vya watu, wakiwemo wananchi, viongozi na askari, na kwamba wakati umefika wa kuchukua hatua madhubuti kurejesha amani. Ameelekeza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru na Kamati za Ulinzi na Usalama kuwachukulia hatua wote watakaobainika kuchochea migogoro hiyo, bila kujali nafasi zao, nyadhifa au itikadi zao za kisiasa. Makamu wa Rais amesema baadhi ya viongozi wa vijiji wanadaiwa kushiriki katika uuzaji wa maeneo na kuwaingiza wafugaji katika maeneo yasiyoruhusiwa, hali inayochangia migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji. Matumizi ya ardhi ya vijiji lazima yazingatie sheria na ushirikishwaji wa wananchi badala ya maamuzi ya watu wachache wenye maslahi binafsi. Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutafuta suluhu ya kudumu kupitia timu ya kitaifa na wizara zinazohusika, lakini juhudi hizo zinapaswa kwenda sambamba na hatua za haraka dhidi ya wanaochochea migogoro. Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mahmoud amesema Serikali imepokea maelekezo hayo na kwamba Jeshi la Polisi litashirikiana na mamlaka nyingine kuhakikisha wote wanaobainika kuhusika wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Amesema takribani watu 12 wamepoteza maisha kutokana na migogoro hiyo, huku zaidi ya vikosi 20 vya askari vikiendelea na operesheni ya kuwaondoa wafugaji wanaofuga katika maeneo yasiyoruhusiwa kwa mujibu wa mipango ya matumizi bora ya ardhi. Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameagiza kuimarishwa kwa usimamizi wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Songea–Tunduru–Masasi–Mahumbika, akielekeza kubadilishwa kwa meneja wa mradi kutokana na kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wake. Amesema Serikali tayari imetoa zaidi ya shilingi bilioni 42 kwa mkandarasi, hivyo hakuna sababu ya mradi huo kuendelea kusuasua wakati wananchi wa Tunduru na mikoa ya Lindi na Mtwara wanahitaji umeme wa uhakika kwa ajili ya shughuli za kiuchumi. Kuhusu maendeleo ya Wilaya ya Tunduru, Makamu wa Rais ameelekeza kufuatiliwa kwa ombi la ujenzi wa soko la kisasa, ambapo Waziri mwenye dhamana ya TAMISEMI amesema maandalizi ya mradi huo yamefikia hatua ya kuwasilishwa kwa andiko katika Tume ya Mipango, huku Serikali ikitarajia kuanza ujenzi katika mwaka wa fedha 2027/2028.