Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Na Scolastica Sambi – MAELEZO Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu ya ukusanyaji, uhifadhi na usafirishaji wa mazao ili kupunguza upotevu baada ya mavuno na kuongeza kipato cha wakulima nchini. Akizungumza Novemba 9, 2026, jijini Arusha, wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonyesho ya Kimataifa ya Horticultural Logistics Africa 2026, amesema wakulima wamekuwa wakifanya juhudi kubwa kuongeza uzalishaji, lakini sehemu ya mazao yao hupotea kutokana na uhaba wa miundombinu na mifumo bora ya kuyahifadhi na kuyasafirisha. Ametoa mfano wa wakulima wa mananasi katika mikoa ya Tanga, Arusha na Morogoro, ambao baadhi yao hulazimika kuuza mazao yao kando ya barabara, huku mengine yakiharibika kwa kukosa mifumo madhubuti ya ukusanyaji na uhifadhi. Hali kama hiyo pia inawakabili wakulima wa parachichi katika mikoa ya Njombe, Mbeya na Manyara. Tunazalisha sana, wakulima wetu wanajitoa sana, lakini tunapoteza zao lile ambalo tunazalisha,” amesema Makamu wa Rais, akisisitiza umuhimu wa kujenga vituo vya kisasa vya ukusanyaji wa mazao, maghala ya kuhifadhi, mifumo ya ubaridi na kuboresha usafirishaji. Amesema uwekezaji katika maeneo hayo utapunguza hasara kwa wakulima, kuongeza thamani ya mazao na kuhakikisha bidhaa zinafika sokoni kwa wakati na katika ubora unaohitajika. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwaunganisha wakulima na wanunuzi kupitia mikataba ya uzalishaji na ununuzi wa mazao ili kuhakikisha shughuli za kilimo zinaendana na mahitaji halisi ya soko. Makamu wa Rais, amebainisha kuwa uzalishaji wa mazao ya bustani nchini umeongezeka kutoka tani milioni 8.4 mwaka 2023 hadi tani milioni 9.7 mwaka 2025, sawa na ukuaji wa asilimia 15.9. Hata hivyo, amesema ongezeko hilo la uzalishaji linapaswa kwenda sambamba na uwekezaji katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya bustani ili kuongeza kipato cha wakulima, kutengeneza ajira na kukuza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.

Na Mwandishi Wetu London, Uingereza Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake katika ramani ya utalii duniani baada ya kutangazwa kuwa mwenyeji wa hafla ya utoaji wa Tuzo za Dunia za Utalii (World Travel Awards – WTA) kwa mwaka 2026, zitakazofanyika Desemba 12, 2026 katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Tangazo hilo limetolewa Novemba 5, 2026 na Mwanzilishi na Rais wa World Travel Awards, Bw. Graham Cooke, wakati wa hafla maalumu iliyofanyika katika kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya World Travel Market (WTM) jijini London, Uingereza. Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Cooke amesema Tanzania imechaguliwa kutokana na upekee wake katika sekta ya utalii, akibainisha kuwa Serengeti ni moja ya majina makubwa yanayotambulika barani Afrika na duniani kutokana na utajiri wake wa wanyamapori na vivutio vya kipekee. Ameongeza kuwa uwepo wa Mlima Kilimanjaro, ambao ni mlima mrefu zaidi barani Afrika, pamoja na uzuri wa vivutio vya asili na ukarimu wa Watanzania, ni miongoni mwa sababu zilizoifanya Tanzania kuwa chaguo sahihi la kuandaa tukio hilo la kimataifa. Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amemshukuru Bw. Cooke na taasisi ya World Travel Awards kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa hafla hiyo muhimu, akieleza kuwa nchi ipo tayari kuhakikisha wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani wanapata uzoefu wa kipekee wa utalii wa Tanzania. Amesema Serengeti nayo ipo tayari kupokea wageni zaidi ya 500 wanaotarajiwa kuhudhuria hafla hiyo kutoka mataifa mbalimbali duniani, huku akisisitiza kuwa tukio hilo ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania, kuongeza muonekano wake kimataifa na kuimarisha nafasi yake katika soko la utalii duniani. Aidha, Dkt. Kijaji ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi na uongozi wake katika kuifungua Tanzania na kuimarisha diplomasia, akisema kazi kubwa inayofanyika chini ya uongozi wake imechangia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Tanzania na kuiweka katika nafasi nzuri zaidi katika jukwaa la kimataifa la utalii. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Dkt. Thereza Mugobi.

Na Mwandishi Wetu – Geneva, Uswisi Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza na kulinda utu na haki za binadamu kwa watu wote, huku ikiendelea kuweka upatikanaji wa haki na huduma muhimu kwa wananchi kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Serikali. Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Ulega, amesema hayo Novemba 5, 2026, wakati akiwasilisha hotuba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika awamu ya nne ya Mapitio ya Kimataifa ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR), mbele ya Kikundi Kazi cha UPR katika kikao chake cha 53 kinachoendelea jijini Geneva, Uswisi, kuanzia Novemba 2 hadi 13, 2026. Mhe. Ulega amesema Tanzania inajivunia kushiriki katika awamu hiyo ya mapitio, huku akieleza hatua zilizopigwa katika kuimarisha haki za kiraia na kisiasa, ushiriki wa kidemokrasia, uhuru wa msingi na upatikanaji wa haki. Ameeleza kuwa, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, juhudi za kuimarisha haki za binadamu zimeongozwa na falsafa ya Misingi Minne ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Upya. Tunatambua umuhimu wa kuendelea kufanya mageuzi, kuimarisha taasisi na kuhakikisha uwajibikaji katika maeneo yote huku tukiongozwa na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 na misingi ya kutomwacha mtu yeyote nyuma. Hivyo, tunakaribisha mapendekezo yenye kujenga pamoja na ushirikiano unaozingatia kuheshimiana. Tuko tayari kusikiliza, kubadilishana uzoefu na kushirikiana na nchi wanachama katika misingi ya mazungumzo yenye kujenga na kuheshimiana. Aidha, amezitaka nchi washirika wa kimataifa kuheshimu mamlaka ya Tanzania na taratibu zake za kisheria, akisisitiza kuwa ushirikiano katika masuala ya haki za binadamu unapaswa kuzingatia mazungumzo yenye kujenga, kuheshimiana na wajibu wa pamoja wa kulinda na kuendeleza haki hizo. Akieleza hatua zilizopigwa katika kutekeleza haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, Waziri Ulega amesema Tanzania imeendelea kuwekeza katika miundombinu na huduma muhimu zinazoboresha maisha ya wananchi na kupanua fursa za maendeleo. Ametaja uwekezaji huo kuwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa ya SGR yenye urefu wa zaidi ya kilomita 700 na Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme. Ameongeza kuwa vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vimefikiwa na huduma ya umeme, huku kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini kikifikia takribani asilimia 79.5. Vilevile, uwekezaji katika sekta mbalimbali za uzalishaji umewezesha kupatikana kwa fursa za ajira zaidi ya milioni 4.2. Katika sekta ya elimu, amesema bajeti imeongezeka kutoka takribani shilingi trilioni 5.6 katika mwaka wa fedha 2022/2023 hadi shilingi trilioni 6.3 katika mwaka wa fedha 2025/2026. Ameeleza pia kuwa Serikali inaendelea kutoa elimu ya msingi bila ada na kuweka utaratibu unaowawezesha wanafunzi waliokatisha masomo kurejea shuleni, wakiwemo wasichana walioacha masomo kutokana na ujauzito. Katika sekta ya afya, idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya Tanzania Bara imeongezeka kutoka 8,458 mwaka 2022 hadi zaidi ya 10,000 mwaka 2026. Huduma za kliniki kwa wajawazito zimefikia asilimia 98, huku kiwango cha wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya kikiongezeka kutoka asilimia 83 hadi asilimia 98. Aidha, kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi kimepungua kutoka 197 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, huku vifo vya watoto wachanga vikishuka kutoka 25 hadi 19 kwa kila vizazi hai 1,000. Hatua hizo zinaonesha juhudi za Serikali katika kupanua upatikanaji wa huduma za afya, hususan kwa akina mama na watoto. Kuhusu uwezeshaji wa wanawake na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, Waziri Ulega amesema Tanzania imepiga hatua katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na umiliki wa rasilimali. Uwakilishi wa wanawake katika Bunge ulifikia asilimia 39.3 mwaka 2025, huku uwakilishi wao katika Mahakama ukifikia asilimia 36.5. Aidha, uwiano wa wanawake wenye haki za umiliki wa ardhi uliongezeka kutoka asilimia 28.5 mwaka 2020 hadi asilimia 35 mwaka 2025. Akizungumzia utekelezaji wa mapendekezo ya mapitio yaliyotangulia, amesema katika awamu ya tatu iliyofanyika mwaka 2021, Tanzania ilipokea jumla ya mapendekezo 252, ikakubali mapendekezo 187, yakiwemo 20 yaliyokubaliwa kwa sehemu, huku mapendekezo 65 yakikosa ridhaa ya Serikali. Amesema mapendekezo yaliyokubaliwa yamekuwa mwongozo katika kutekeleza mageuzi mbalimbali katika kipindi chote kilichopita, hatua inayoonesha dhamira ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kuimarisha na kulinda haki za binadamu.

Na. Timothy Mwakyenda – MAELEZO Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewataka Watanzania kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini ili kukuza viwanda vya ndani, kulinda ajira, kuongeza mapato ya taifa na kuimarisha uchumi wa wananchi. Ameyasema hayo tarehe 4 Novemba, 2026 jijini Dodoma, alipokuwa akizindua Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Ujasiriamali Mdogo na wa Kati ya mwaka 2003, toleo la mwaka 2025, ambapo alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Amesema kuwa sera hizo zinatarajiwa kuimarisha uzalishaji wa bidhaa nchini, kupanua fursa za biashara na uwekezaji na kuwezesha wajasiriamali kukua kutoka biashara ndogo kwenda za kati na kubwa, hatua itakayochochea upatikanaji wa ajira na kuongeza kipato cha wananchi na kusisitiza kuwa watanzania wana wajibu wa kuunga mkono viwanda vya ndani kwa kununua bidhaa zake. Viwanda vinapopata soko la uhakika vinaweza kuongeza uzalishaji, kuajiri watu wengi zaidi na kuchangia mapato ya serikali kupitia shughuli za kiuchumi. Amesema ni muhimu kubadili mtazamo kuhusu wawekezaji na wafanyabiashara kwa kuwachukulia kama washirika muhimu wa maendeleo ya taifa, badala ya kuwawekea mazingira yanayokwamisha shughuli zao na kueleza kuwa sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika uwekezaji, uzalishaji na ajira kwa vijana. Aidha ameongeza kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, huku akizitaka wizara na taasisi husika kuondoa vikwazo visivyo vya lazima vinavyoweza kudhoofisha shughuli za biashara na kusistiza kuwa kama sheria zinapokuwa kikwazo kwa maendeleo ya wananchi, zinapaswa kufanyiwa marekebisho ili ziendane na mahitaji ya sasa ya uchumi. Pamoja na hayo Dkt. Nchemba amezitaka sekta ya viwanda na biashara, kwa kushirikiana na wizara nyingine na sekta binafsi, kusimamia utekelezaji wa sera hizo kwa kuweka mikakati inayopimika na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mara kwa mara na kusisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na rasilimali nyingine za nchi kabla ya kuuzwa katika masoko ya ndani na nje. Pia, amesema kuwa serikali itaendelea kuboresha miundombinu wezeshi, ikiwemo nishati, maji, barabara na reli, ili kupunguza changamoto za uzalishaji na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kubainisha kuwa mazingira bora ya uzalishaji yatawezesha viwanda kuongeza tija na ushindani, huku wananchi wakinufaika kupitia bidhaa zinazopatikana kwa uhakika na fursa nyingi zaidi za kiuchumi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuimarisha usimamizi wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini kwa kuongeza ufuatiliaji wa masuala yanayohusu haki za wananchi badala ya kutegemea malalamiko pekee. Akizungumza Novemba 2, 2026, alipokuwa akiwaapisha viongozi wateule katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Mhe. Rais amesema Tume hiyo inapaswa kuwa na utaratibu wa kubaini na kufuatilia changamoto za ukiukwaji wa haki za binadamu katika taasisi na sekta mbalimbali na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa. Amesema Tume hiyo pia inapaswa kufuatilia tuhuma na shutuma zinazoikabili Tanzania kuhusu haki za binadamu katika majukwaa ya kimataifa na kutoa majibu kwa kuzingatia ukweli na hali halisi ya ndani ya nchi. Nawaambieni sana ninyi vijana, mna uwezo wa kuperuzi mitandao yote na kuona yanayotokea duniani, mkaona shutuma tunazopewa na mkaweza kuzijibu. Ameongeza kuwa jukumu la Tume hiyo halipaswi kuishia katika kupokea malalamiko ya wananchi, bali pia kufuatilia maeneo ambayo kuna viashiria vya ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili kuhakikisha haki zinalindwa. Katika hatua nyingine, Mhe. Rais amewataka viongozi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Migogoro ya Wafanyakazi kusimamia haki za wafanyakazi na waajiri kwa kuzingatia sheria, akisisitiza kuwa maamuzi yao yanapaswa kutolewa bila chuki, hila wala upendeleo. Amesema ukuaji wa uwekezaji na shughuli za sekta binafsi unaweza kuongeza migogoro ya kikazi, hivyo wanapaswa kujiandaa kukabiliana nayo kwa weledi. Miongoni mwa viongozi walioapishwa ni Bw. Dunford George Mpelumbe, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; Bw. Omar Ali Omar, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo; Bi. Angeline Lubala Mabula, Mkuu wa Mkoa wa Tabora; pamoja na Jaji Mstaafu Wilfred Peter Dyansobera, Mwenyekiti wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Migogoro ya Wafanyakazi, na makamishna wa Tume hiyo. Mhe. Rais amewapongeza viongozi wote walioapishwa na kuwatakia mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa Serikali ina matarajio makubwa ya kuona wanatekeleza dhamana walizopewa kwa uadilifu na kuzingatia maslahi ya wananchi.

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO Serikali inajenga kituo maalum cha wanahabari jijini Dodoma, kitakachojulikana kama Tanzania Media Center, kwa lengo la kuwawezesha waandishi wa habari kupata eneo salama na rafiki kwa ajili ya kuandaa habari, kufanya mahojiano na kutekeleza shughuli zao za kitaaluma wanapokuwa katika majukumu ya kikazi mjini humo. Akizungumza Oktoba 31, 2026, katika Kongamano la Mwaka la Tathmini ya Huduma za Habari na Mawasiliano Vijijini Tanzania, lililowakutanisha wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini (RUJAT), jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kituo hicho kinajengwa eneo la Mzunguni jijini Dodoma na kitakuwa na ghorofa mbili pamoja na maeneo maalum kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wanahabari. Amesema ujenzi wa kituo hicho unalenga kutatua changamoto ya ukosefu wa eneo maalum la kufanyia kazi inayowakabili waandishi wengi wa habari wanapofika Dodoma kwa shughuli za kikazi, hali inayowalazimu kutumia vyumba vya hoteli au maeneo mengine yasiyo rasmi kuandaa habari na kufanya mahojiano, jambo linaloweza kuhatarisha usalama na usiri wa taarifa. Ameeleza kuwa kituo hicho kitakuwa sehemu ya kukutanisha wanahabari, kufanya kazi na kupokea watu wanaohitaji kutoa mahojiano, hivyo kuwawezesha kutekeleza majukumu yao katika mazingira yanayozingatia mahitaji ya taaluma ya habari. Aidha, amesema ukumbi uliopo katika ofisi za Idara ya Habari utaendelea kutumika kutoa huduma kwa waandishi wa habari wanaofika Dodoma kwa shughuli mbalimbali za kikazi. Katika hatua nyingine, Msigwa amewataka waandishi wa habari kuimarisha weledi na kuandika habari zinazogusa maisha ya wananchi, hususan wanaoishi vijijini, akibainisha kuwa sehemu kubwa ya Watanzania wanaishi katika maeneo ya vijijini, lakini vyombo vingi vya habari vimeelekeza nguvu zaidi katika kuripoti matukio ya mijini. Amesisitiza kuwa wanahabari wanapaswa kufanya uchunguzi wa kina na kufuatilia changamoto zinazowakabili wananchi hadi pale zinapopatiwa ufumbuzi. Akitolea mfano, amesema taarifa za habari kuhusu changamoto za upatikanaji wa maji na dawa zimekuwa zikichochea hatua za kutatua matatizo hayo. Vilevile, amesisitiza umuhimu wa mafunzo endelevu, matumizi ya teknolojia na uandishi unaozingatia ushahidi pamoja na maslahi ya umma. Amewataka wanahabari kujiepusha na vitendo vinavyoweza kushusha heshima ya taaluma ya habari na badala yake kuimarisha ushirikiano kati yao na maafisa habari wa Serikali.

Na Baraka Messa – MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kusogeza huduma karibu na wananchi, kurahisisha upatikanaji wake na kuhakikisha huduma za umma zinapatikana kwa ufanisi na usawa katika maeneo mbalimbali ya nchi. Amesema hatua hiyo inaendeleza maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyetangaza mwaka 1973 uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma, kwa lengo la kuimarisha uwiano wa maendeleo na kusogeza shughuli za Serikali karibu zaidi na wananchi. Rais Samia ameyasema hayo Oktoba 30, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo ya wizara na taasisi za Serikali pamoja na barabara zilizojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, iliyohudhuriwa pia na Rais wa Jamhuri ya Angola, João Lourenço. Amesisitiza kuwa ujenzi wa majengo ya kisasa pekee hautoshi kutimiza azma ya Serikali, bali unapaswa kwenda sambamba na utoaji wa huduma bora, kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili taasisi za Serikali ziwasiliane kwa ufanisi, kupunguza urasimu na kurahisisha huduma kwa wananchi. Aidha, amewataka watumishi wa umma kutunza majengo na miundombinu iliyojengwa, kuyatumia kwa ufanisi na kuhakikisha yanakuwa mazingira bora ya kufanyia kazi na kuhudumia wananchi. Ameeleza pia kuwa ukuaji wa Dodoma unahitaji mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi na maendeleo ya mji ili kuendana na hadhi yake kama makao makuu ya nchi. Katika hatua nyingine, Rais Samia ameeleza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Angola, akibainisha kuwa uamuzi wa kuipa barabara moja ya Mji wa Serikali jina la Rais wa kwanza wa Angola, Agostinho Neto, ni ishara ya kuthamini mchango wa viongozi wa mataifa hayo katika historia ya ukombozi wa Afrika. Kwa upande wake, Rais wa Angola, João Lourenço, ameishukuru Tanzania kwa mchango wake katika harakati za ukombozi wa Angola na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo, hususan katika sekta za usafiri wa anga na reli. Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema utekelezaji wa mradi wa Mji wa Serikali ulianza mwaka 2016 katika Awamu ya Tano ya Serikali na kugharamiwa kwa kutumia fedha za ndani, hatua inayoonesha dhamira ya nchi katika kuwekeza kwenye miundombinu ya umma na maendeleo ya taifa. Kwa ujumla, Mji wa Serikali Mtumba ni zaidi ya mkusanyiko wa majengo ya wizara na taasisi za umma; ni hatua muhimu katika kutekeleza azma ya kuifanya Serikali iwe karibu zaidi na wananchi. Mafanikio yake yatapimwa kwa namna miundombinu hiyo itakavyotumika kuboresha huduma, kupunguza gharama na muda wa kuzifikia, pamoja na kuongeza ufanisi wa utendaji wa Serikali.

Na Timothy Mwakyenda – MAELEZO Safari iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço, kwa kutumia treni ya kisasa inayotumia nishati ya umeme kupitia reli ya SGR kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma, Oktoba 30, 2026, ni hatua yenye ujumbe mpana kuhusu maendeleo ya sekta ya usafirishaji nchini Tanzania. Mbali na kuonesha kuimarika kwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, safari hiyo imeonesha uwezo wa Tanzania kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya reli na kutoa huduma za usafiri zinazokidhi mahitaji ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Viongozi hao walianza safari yao katika Stesheni ya Magufuli jijini Dar es Salaam kuelekea Dodoma kushiriki hafla ya uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba pamoja na barabara zake za lami. Matumizi ya SGR katika safari hiyo yanaonesha namna reli ya kisasa inavyoweza kuwa kiungo muhimu katika kurahisisha usafiri wa watu na usafirishaji wa bidhaa, huku ikitoa fursa kwa viongozi na wageni wa kimataifa kujionea maendeleo ya miundombinu ya usafiri nchini. Hatua hiyo pia ni kielelezo cha ukuaji na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya usafirishaji Tanzania, hususan katika kuimarisha usalama, ufanisi na ubora wa huduma za reli. Reli ya SGR ina nafasi muhimu katika kupunguza muda wa safari, kurahisisha usafiri wa wananchi na kutoa huduma inayoweza kukidhi mahitaji ya makundi mbalimbali, yakiwemo wafanyabiashara, watalii na wasafiri wengine. Hivyo, uwekezaji huo una mchango katika kukuza shughuli za kiuchumi na kuimarisha ushindani wa Tanzania kama kitovu cha usafirishaji katika ukanda huu wa Afrika. Akizungumza kabla ya safari hiyo, Rais Samia alisema matumizi ya SGR yanaonesha dhamira ya Tanzania na Angola ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafirishaji, hususan reli, kwa lengo la kurahisisha usafiri wa watu na usafirishaji wa bidhaa kati ya nchi hizo na maeneo mengine ya Afrika. Alisema Tanzania inaendelea na ukarabati wa reli ya TAZARA inayounganisha nchi hiyo na Zambia kupitia Kapiri Mposhi, huku Angola nayo ikiendelea na ukarabati wa reli ya Benguela. Hatua hizo zinatarajiwa kuimarisha muunganiko wa reli na kurahisisha biashara katika ukanda huo. Katika mazungumzo yetu tumekubaliana tuunganishe korido zetu kati ya Benguela na korido ya ukanda wa Kati ya Tanzania ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa. Ndiyo maana tumeamua kutumia usafiri huu kuonesha kwamba inawezekana Kwa mtazamo mpana, matumizi ya SGR kwa viongozi hao ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania katika medani za kimataifa kama nchi inayopiga hatua katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya usafiri. Reli hiyo inatoa taswira ya Tanzania inayowekeza katika teknolojia na huduma zinazokidhi mahitaji ya sasa na zijazo, huku ikiimarisha uwezo wa nchi kuwahudumia wananchi na wageni wanaoitembelea. Aidha, kuunganisha korido za reli za Tanzania na Angola kunaweza kufungua fursa kubwa zaidi za biashara, utalii, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika. Kwa ujumla, safari hiyo imebeba ujumbe kwamba SGR si mradi wa usafiri pekee, bali ni sehemu ya mkakati mpana wa maendeleo ya taifa. Ni miundombinu inayopaswa kuendelea kutunzwa, kuboreshwa na kutumiwa ipasavyo ili kuimarisha usalama, kuongeza ufanisi wa usafirishaji na kuchochea uchumi. Hatua hiyo inaweka msingi wa Tanzania kuendelea kujijengea nafasi kama kitovu muhimu cha usafiri na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Na Neema Kaniki– MAELEZO Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kukuza uchumi na kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050. Amesema hayo Oktoba 25, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa jengo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo jijini Dodoma, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo na ustawi wa wananchi. Msigwa amesema Serikali inaendelea kutekeleza majukumu yake chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ukiwa umeanza kupitia bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa ulioanza Julai Mosi, 2026. Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 imeweka lengo la kujenga uchumi wenye thamani ya Dola za Marekani trilioni moja kutoka takribani Dola bilioni 90 za Marekani, hatua inayohitaji ushiriki na uwajibikaji wa pamoja kutoka kwa Serikali, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo. Mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 yanahitaji uwajibikaji wa pamoja kwa wadau wote, Serikali inatarajiwa kuchangia asilimia 30 ya uchumi huo, huku sekta binafsi ikitarajiwa kuchangia asilimia 70. Amesisitiza kuwa kufikiwa kwa malengo hayo kunategemea uwepo wa mazingira ya amani na utulivu yatakayowawezesha wananchi kujikita katika shughuli za uzalishaji mali, biashara, hususan biashara ya nje, pamoja na kuboresha maisha yao na ustawi wa jamii kwa ujumla. Amesema vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani vinaweza kukwamisha shughuli za kiuchumi, kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi, hivyo kuwataka Watanzania kutokubali kushawishiwa kushiriki matukio yanayoweza kuhatarisha utulivu wa nchi. Natoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kujiepusha na matukio yenye viashiria vya vurugu na uvunjifu wa amani, Watanzania wakatae watu wanaodhani wanaweza kufanikisha ajenda zao kwa kuwahamasisha kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria, pakichafuka hapa, hakuna mjomba wa kutusaidia zaidi ya sisi wenyewe. Aidha, Msigwa amewahakikishia wananchi kuwa Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kusimamia amani na usalama wa watu na mali zao, pamoja na kulinda mipaka ya nchi, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria kwa sababu ya kauli au msimamo wake.

Na Bupe Mwaiseje – MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi majengo na miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Oktoba 30, 2026, katika hatua inayolenga kuimarisha ufanisi wa utendaji wa Serikali na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Akizungumza na waandishi wa habari, katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO jijini Dodoma, Oktoba 25, 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali imewekeza takribani shilingi bilioni 700 katika ujenzi wa mji huo. Msigwa amesema ujenzi wa majengo ya kisasa ya wizara na taasisi za Serikali ulianza mwaka 2021, chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, ukiwa ni sehemu ya utekelezaji wa uamuzi wa kuhamishia shughuli za Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, uliotangazwa mwaka 2016 na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Ameeleza kuwa Mji wa Serikali Mtumba umejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya kiutendaji, ukiwa na takribani kilomita 59 za barabara pamoja na mifumo ya kisasa ya mawasiliano inayowezesha taasisi za Serikali kuwasiliana na kutekeleza majukumu yake kwa njia ya mtandao. Amesema mifumo hiyo itapunguza urasimu na muda wa kushughulikia nyaraka, hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji wa Serikali na kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Faili likifika asubuhi linajibiwa mchana kwa sababu hakuna sababu ya kutuma watu na magari na bodaboda kwenda kusambaza barua. Barua zinatembea kwa mtandao. Aidha, amesema Tanzania imepokea ujumbe kutoka nchi zaidi ya 10 zilizofika kujifunza kuhusu ujenzi na uendeshaji wa Mji wa Serikali Mtumba, akibainisha kuwa miundombinu hiyo ina fursa ya kuwa kivutio cha utalii jijini Dodoma. Msigwa amewahimiza Watanzania kufuatilia uzinduzi huo, akieleza kuwa ni tukio muhimu katika historia ya maendeleo ya Dodoma na utekelezaji wa uamuzi wa kuifanya kuwa makao makuu ya Serikali.