Makamu wa Rais: Asema Serikali Kuchukua Hatua Migogoro ya Wakulima na Wafugaji
Na mwandishi wetu-Tunduru Ruvuma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameagiza kuanza mara moja kwa operesheni maalumu ya kuwabaini na kuwakamata watu wanaochochea migogoro ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, huku akitaka kupatiwa taarifa ya hatua zilizochukuliwa akiwa bado katika ziara yake mkoani humo.
Akizungumza Novemba 11, 2026 katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Tunduru, Makamu wa Rais amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imesikia kilio cha wananchi kutokana na migogoro hiyo iliyosababisha vifo vya watu, wakiwemo wananchi, viongozi na askari, na kwamba wakati umefika wa kuchukua hatua madhubuti kurejesha amani.
Ameelekeza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru na Kamati za Ulinzi na Usalama kuwachukulia hatua wote watakaobainika kuchochea migogoro hiyo, bila kujali nafasi zao, nyadhifa au itikadi zao za kisiasa.
Makamu wa Rais amesema baadhi ya viongozi wa vijiji wanadaiwa kushiriki katika uuzaji wa maeneo na kuwaingiza wafugaji katika maeneo yasiyoruhusiwa, hali inayochangia migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji.
Matumizi ya ardhi ya vijiji lazima yazingatie sheria na ushirikishwaji wa wananchi badala ya maamuzi ya watu wachache wenye maslahi binafsi.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutafuta suluhu ya kudumu kupitia timu ya kitaifa na wizara zinazohusika, lakini juhudi hizo zinapaswa kwenda sambamba na hatua za haraka dhidi ya wanaochochea migogoro.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mahmoud amesema Serikali imepokea maelekezo hayo na kwamba Jeshi la Polisi litashirikiana na mamlaka nyingine kuhakikisha wote wanaobainika kuhusika wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Amesema takribani watu 12 wamepoteza maisha kutokana na migogoro hiyo, huku zaidi ya vikosi 20 vya askari vikiendelea na operesheni ya kuwaondoa wafugaji wanaofuga katika maeneo yasiyoruhusiwa kwa mujibu wa mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameagiza kuimarishwa kwa usimamizi wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Songea–Tunduru–Masasi–Mahumbika, akielekeza kubadilishwa kwa meneja wa mradi kutokana na kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wake.
Amesema Serikali tayari imetoa zaidi ya shilingi bilioni 42 kwa mkandarasi, hivyo hakuna sababu ya mradi huo kuendelea kusuasua wakati wananchi wa Tunduru na mikoa ya Lindi na Mtwara wanahitaji umeme wa uhakika kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.
Kuhusu maendeleo ya Wilaya ya Tunduru, Makamu wa Rais ameelekeza kufuatiliwa kwa ombi la ujenzi wa soko la kisasa, ambapo Waziri mwenye dhamana ya TAMISEMI amesema maandalizi ya mradi huo yamefikia hatua ya kuwasilishwa kwa andiko katika Tume ya Mipango, huku Serikali ikitarajia kuanza ujenzi katika mwaka wa fedha 2027/2028.