NIDA Iliyoboreshwa Kuimarisha Usalama, Kuongeza Wigo wa Huduma
Na Bupe Mwaiseje- MAELEZO
Serikali imezindua kitambulisho kipya cha Taifa chenye teknolojia ya kisasa kinacholenga kuimarisha usalama, kupambana na utapeli, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupanua fursa za kiuchumi, huku watendaji wa umma wakitakiwa kuwajibika na kuacha vitendo vinavyowasababishia wananchi usumbufu katika kupata huduma.
Akizungumza Novemba 18, 2026 katika uzinduzi wa Kitambulisho cha Taifa Kilichoboreshwa Kibaha, mkoani Pwani, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema uwekezaji huo ni hatua muhimu katika matumizi ya teknolojia kuboresha huduma, kuimarisha utawala bora na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kitambulisho hiki kitarahisisha shughuli mbalimbali, zikiwemo huduma za bima, leseni na safari katika baadhi ya maeneo kadiri makubaliano yatakavyofikiwa na nchi washirika, niwatake wananchi kujitokeza kuchukua vitambulisho vyao vinapokamilika ili wanufaike na huduma zinazotolewa kupitia mfumo huu.
Katika hatua nyingine, amesisitiza “Nataka uwajibikaji wa watendaji wa Serikali, acheni kuwatoza wagonjwa fedha za mafuta ya magari ya wagonjwa na hakikisheni dawa zinazotolewa na Serikali zinawafikia wananchi badala ya kufichwa na kuwaelekeza wakazinunue kwenye maduka binafsi. Magari ya wagonjwa si daladala na mazoea ya kuwachangisha wagonjwa hayapaswi kugeuzwa kuwa utaratibu wa utoaji huduma.”
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi, amesema mfumo wa NIDA ni nyenzo muhimu katika kupambana na uhalifu na utapeli, akipendekeza kampuni za simu za mkononi kudhibiti namba ambazo hazijasajiliwa kwa kutumia taarifa za NIDA ili kuzuia matumizi ya simu katika vitendo vya utapeli.
Aidha, Mhe. Katambi amesema hadi Oktoba 29, vitambulisho 1,832,683 vilikuwa bado havijachukuliwa na wananchi, huku akibainisha kuwa zaidi ya taasisi 72 za Serikali na 85 za sekta binafsi zimeunganishwa na mfumo wa NIDA.
Amefafanua kuwa NIDA inaendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA, uwezo wa uzalishaji na usambazaji wa vitambulisho pamoja na usalama wa taarifa za wananchi, huku vitambulisho vipya vikiwa na vipengele vya kisasa vinavyolenga kupanua matumizi yake katika huduma mbalimbali.
Vitambulisho vipya vitatumika kwa yeyote yule anayejisajili upya lakini haiondio uhalali wa vitambulisho vya awali.
Uzinduzi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kutumia teknolojia kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha utawala bora, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.