Karibu!

Tunakukaribisha kwenye tovuti rasmi ya Msemaji Mkuu wa Serikali upate taarifa na habari sahihi zenye kuakisi malengo ya Serikali, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na matarajio ya Watanzania.

Mawasiliano

Tufuatilie

Tanzania Yatangaza Nia ya Kuwania Nafasi Baraza la Usalama la UN

September 23, 2026

Na Mwandishi Wetu – MAELEZO

Tanzania imeweka wazi azma yake ya kuwania nafasi ya uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029–2030, ikiwa na dhamira ya kupeleka katika chombo hicho sauti ya Afrika na kusukuma mbele ajenda ya amani, maendeleo na mageuzi ya mfumo wa kimataifa.

Azma hiyo imetangazwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mjadala wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika jijini New York, Marekani.

Mhe. Ndejembi amesema endapo Tanzania itachaguliwa, itatoa kipaumbele kwa diplomasia ya kuzuia migogoro kabla haijageuka kuwa vita, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani, kuimarisha nafasi ya wanawake katika ulinzi na ujenzi wa amani, kuongeza ushiriki wa vijana katika ajenda za amani na usalama, pamoja na kusukuma mbele mageuzi ya operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani.

Dhamira hiyo imepata uungwaji mkono wa Umoja wa Afrika (AU), huku uchaguzi wa nafasi hiyo ukitarajiwa kufanyika Juni 2028.

Kwa Tanzania, safari ya kuwania nafasi hiyo inakwenda sambamba na hoja pana ya kutaka mfumo wa kimataifa uwe na uwakilishi wenye uwiano zaidi na kutoa nafasi kubwa kwa nchi zinazoendelea kushiriki katika maamuzi yanayogusa mustakabali wa dunia.

Katika hotuba yake, Mhe. Ndejembi amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kuendelea kufanyiwa mageuzi ili kuimarisha misingi ya haki, usawa na uwakilishi, hususan wakati dunia ikikabiliwa na changamoto zinazovuka mipaka ya nchi moja.

Migogoro na vita, mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa, kasi ya maendeleo ya akili mnemba (AI) na changamoto za usalama wa nishati ni miongoni mwa masuala ambayo Tanzania imesema yanahitaji ushirikiano wa kimataifa na taasisi zenye uwezo wa kuitikia mahitaji ya dunia ya sasa.

Katika kueleza msingi wa msimamo wake, Tanzania imeonyesha pia uzoefu wake katika kushughulikia changamoto za maendeleo na ustawi wa jamii.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akihutubia Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA81), kinachofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York nchini Marekani, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Ndejembi amesema Tanzania imepiga hatua katika kuboresha afya ya mama na mtoto, ambapo kiwango cha uzazi unaofanyika katika vituo vya afya kiliongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2015 hadi asilimia 81 mwaka 2022.

Tanzania pia imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama kwa asilimia 80 ndani ya kipindi cha miaka saba, hatua ambayo imehusishwa na uwekezaji katika huduma za afya na kuweka ustawi wa wananchi kuwa sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo.

Uzoefu huo umeendelea kupewa nafasi katika ajenda ya afya ya mama na mtoto barani Afrika, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amekubali jukumu la kuwa kinara wa masuala hayo kwa niaba ya Umoja wa Afrika.

Chini ya ajenda ya “Sifuri Tatu” (Three Zeros), Tanzania inalenga kufikia kutokuwepo kwa vifo vya mama na mtoto vinavyoweza kuzuilika, kutokuwepo kwa uzazi unaofanyika majumbani na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo.

Mhe. Ndejembi amesema kufikia malengo hayo kunawezekana, lakini kunahitaji uongozi thabiti wa kisiasa, rasilimali za kutosha na ushirikiano imara wa kimataifa.

Pamoja na afya, Tanzania imeunganisha azma yake ya kidiplomasia na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi jumuishi, shindani na wenye uwezo wa kustahimili misukosuko kupitia uwekezaji katika watu, miundombinu, teknolojia, ubunifu, wanawake na vijana.

Hata hivyo, Tanzania imesema utekelezaji wa malengo ya maendeleo katika nchi zinazoendelea unaendelea kukabiliwa na changamoto za upatikanaji wa fedha, gharama za mikopo na mazingira ya mfumo wa fedha wa kimataifa huku ikitoa wito wa kuongezwa kwa mikopo yenye masharti nafuu, kuhamasishwa kwa uwekezaji wa sekta binafsi, kurahisishwa kwa upatikanaji wa fedha za maendeleo na tabianchi, pamoja na nchi zinazoendelea kupewa sauti kubwa zaidi katika maamuzi ya kifedha duniani.

Mabadiliko ya tabianchi nayo yamepewa nafasi katika ujumbe wa Tanzania, huku nchi ikieleza wasiwasi kuhusu pengo lililopo kati ya kiwango cha uzalishaji wa gesi chafuzi duniani na fedha zinazotolewa kusaidia nchi zinazoathirika kukabiliana na madhara yake.

Tanzania imesisitiza kuwa nchi zinazochangia kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa gesi chafuzi zinapaswa kubeba wajibu mkubwa zaidi katika kugharamia hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika kueleza hatua zake za mpito kuelekea nishati safi, Tanzania imetaja Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, miradi ya nishati ya jua na upepo yenye jumla ya megawati 650, pamoja na mipango ya kuzalisha megawati 130 za nishati ya jotoardhi.

Tanzania pia imeeleza uwekezaji katika reli ya umeme na lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia hadi kufikia asilimia 80 ya kaya ifikapo mwaka 2034.

Katika masuala ya diplomasia na mahusiano ya kimataifa, Tanzania imeeleza msimamo wake dhidi ya matumizi ya vikwazo vya upande mmoja vinavyowekwa na baadhi ya mataifa dhidi ya mengine.

Kwa mujibu wa Tanzania, hatua hizo zinaweza kuathiri maendeleo, mamlaka ya nchi na uwezo wa wananchi kunufaika kikamilifu na haki zao. Nchi hiyo imetaja mshikamano wake na Cuba, Zimbabwe na mataifa mengine yanayokabiliwa na vikwazo hivyo, huku ikitoa wito wa hatua za makusudi kuelekea kuondolewa kwa vikwazo bila masharti.

Kuhusu migogoro inayoendelea ukanda wa Gaza na Mashariki ya Kati, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kulindwa kwa raia, misaada ya kibinadamu kuwafikia wanaohitaji bila vikwazo na diplomasia kurejeshwa kuwa njia kuu ya kutafuta amani ya kudumu.

Kwa ujumla, ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeunganisha masuala ya amani na usalama na ajenda ya maendeleo ya nchi zinazoendelea.

Azma ya kuwania nafasi katika Baraza la Usalama imekuja ikiwa imejengwa juu ya hoja za kuimarisha diplomasia ya kuzuia migogoro, kutafuta suluhu za amani, kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika amani na usalama, pamoja na kusukuma mageuzi ya mfumo wa kimataifa.

Kwa Tanzania, mjadala wa nafasi ya Afrika katika mfumo wa kimataifa hauishii kwenye uwakilishi pekee. Unaenda sambamba na masuala ya maendeleo, fedha, tabianchi, afya, nishati na amani ambayo yanaathiri moja kwa moja maisha ya watu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *